WIZARA ya Ujenzi imeinyang’anya Kampuni ya Agriculture and Animal
Food Industries Ltd (Saafi), inayomilikiwa na mwekezaji mzalendo na
mwanasiasa mkongwe, Dk. Chrisant Mzindakaya nyumba 12 za umma ambazo
ilikuwa imezipanga kibiashara kwa miaka 12.
Nyumba hizo 11 za kuishi na moja ofisi zilizojengwa na Shirika la
Maendeleo la Norway mwaka 1988, zimekabidhiwa rasmi Juni 17 mwaka huu,
kwa Wakala wa Majengo (TBA), mkoani hapa na Wizara ya Ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo wa serikali
baada ya kukagua nyumba hizo juzi, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi
Hilaly (CCM), alisema ana furaha kwani nyumba hizo zilikuwa zikimnyima
usingizi kutokana na maofisa serikalini wakiwemo majaji na baadhi ya
wakuu wa idara kuishi nyumba za kupanga, lakini sasa wataishi nyumba
hizo ambazo ni bora na zenye usalama wa kutosha.
Alibainisha kuwa baada ya kutembelea nyumba hizo na kuzikagua
akiongozana na Meneja wa Wakala wa Majengo Mkoa wa Rukwa, Deocles
Kalikawe, amebaini kuwepo kwa upungufu mkubwa ambao alidai mwekezaji
aliyezipanga kibiashara atalipia gharama zote za ukarabati.
“Nampongeza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa uamuzi mgumu
aliofanya wa kuzirejesha nyumba hizi serikalini kupitia TBA…
Nimemshauri Meneja wa TBA mkoani hapa, moja ya nyumba hizi iwe kwa ajili
ya kufikia viongozi wa kitaifa, kwani iliwahi kutokea tulifikiwa na
wageni wawili kutoka taifani, mmoja alilala Ikulu ndogo, lakini mwingine
alilazimika kulala hotelini,” alisema.
Meneja wa TBA mkoani hapa, Kalikawe, alieleza kuwa mara baada ya
kukabidhiwa rasmi nyumba hizo, waliamua kuweka walinzi wao wakati
wakijipanga kufanya tathmini ya ukarabati ili ziweze kupangishwa kwa
majaji, watumishi wa mahakama na wakuu wa idara.
Baadhi ya wakazi wa mjini hapa waliohojiwa na mwandishi wa habari
hizi, wameipongeza serikali kwa kuchukua uamuzi huo na kwamba utapunguza
tatizo la uhaba wa nyumba.
“Tatizo la uhaba wa nyumba ni changamoto kubwa sana mkoani hapa…
imesababisha baadhi ya watumishi wanaopangiwa kuja kufanya kazi huku
kukataa kuripoti au wanafika lakini wakiondoka hawarudi tena,” alisema
Enos Budodi, mkazi wa mjini hapa.
Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na
shughuli za kijamii na maendeleo (Udeso) kwa mikoa ya Rukwa na Katavi,
Eden Wayimba, alisema uamuzi wa serikali kujireshea mali yake,
utawapunguzia gharama za maisha watumishi wa umma watakaopangishwa.
Kurejeshwa kwa nyumba hizo ni ushindi kwa Aeshi, ambaye tangu awali
amekuwa hana uhusiano mzuri wa kisiasa na Dk. Mzindakaya, ambapo mara
kadhaa alikuwa akihoji uhalali ya nyumba hizo kumilikiwa na kampuni ya
mtu binafsi badala ya kutumiwa na watumishi wa serikali.
Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai uamuzi huo utaongeza
chuki ya kisiasa kati ya wanasiasa hao wawili ambao mara ya mwisho
walikutana Mei mwaka huu kwenye ibada ya kusimikwa kwa Askofu wa Kanisa
la Moravian, Jimbo la Rukwa, Cornad Nguvumali.
Ibada hiyo, ilifanyika kwenye uwanja wa michezo wa Nelson Mandela
mjini hapa, ambapo mkuu wa mkoa aliwataka wazike tofauti zao, lakini Dk.
Mzindakaya alikataa kumsamehe Aeshi kwa madai hakuandaliwa kiroho kutoa
msamaha kwenye ibada hiyo.
Na
Walter Mguluchuma
Post a Comment