Siri ya kipigo kizito ilichokipata klabu ya Manchester United kutoka
kwa klabu iliyopanda daraja msimu huu ya Leicester City imefichuka.
Taarifa zilizozagaa nchini Uingereza zinadai kuwa wachezaji na
viongozi wa klabu ya Leicester City walifanyiwa maombi maalumu kutoka
kwa mmoja kati ya viongozi wa dini ya Kibudha waliokuwepo uwanjani King
Power Stadium kwaajili ya kazi hiyo maalumu.
Wachezaji wa timu hiyo walifanyiwa maombi maalumu na kupewa mikono ya
baraka ambayo inaaminika ndio iliyowasaidia kuupata ushindi huo wa
kihistoria dhidi ya Manchester United kutoka kwa makasisi hao wa dini ya
Kibudha waliofanya kazi hiyo kwenye dimba la King Power Stadium.
Taarifa zinadai kuwa wafungaji wa magoli ya Leicester City David
Nugent na Jamie Vardy walivalishwa mavazi maalumu ya Kibudha mara baada
ya ushindi huo wa jumla ya magoli 5-3 wakati meneja wa timu hiyo Nigel
Pearson alishindwa kuzizuia hisia zake mara baada ya mcheazo huo pale
alipokwenda kuwakumbatia viongozi hao wa kidini ikiwa ni ishara ya kutoa
shukrani kwao kwa kuwa sehemu ya ushindi huo na kuwaambia kuwa
wanakaribishwa uwanjani hapo kila mara timu hiyo itakapokuwa inacheza
ili waweze kufanya maombi hayo.
Mmiliki wa klabu hiyo ambaye ni raia wa Thailand Vichai
Srivaddhanaprabha alisafiri na viongozi hao wa kidini kutokea mashariki
ya mbali na mara alipofika nao nchini Uingereza walikwenda kwenye
kiwanja cha mazoezi cha timu hiyo na mara moja maombi maalumu yakaanza
kwaajili ya mchezo huo dhidi ya Manchester United.
Wiki moja kabla ya msimu kuanza mahema maalumu yalifungwa kwenye
uwanja wa mazoezi wa timu hiyo na viongozi hao wa kidini wakafanya
maombi maalumu kwa viongozi na wachezaji wa timu hiyo yenye malengo ya
kuwapa baraka ambapo inasadikika kuwa maombi hayo yameisaidia sana timu
hiyo kuto kupoteza mchezo wowote ule wa nyumbani dhidi ya vilabu vya
Everton, Arsenal na hatimaye Manchester United.
Mara baada ya kutawazwa kuwa mabingwa wa ligi daraja la kwanza nchini
Uingereza (Championship) wachezaji na viongozi wa timu hiyo walizuru
kwenye eneo la Phra Maha Mondop mahali ambapo majumba ya ibada za
Kibudha kwenye mji wa Bangkok yalipo kwaajili ya kutoa shukrani kwa
maombi waliyofanyiwa mpaka wakaweza kuwa mabingwa na hatimaye kupanda
daraja.
Post a Comment