MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kiongozi yeyote ndani ya chama hicho ambaye ataruhusu mgombea kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi bila kupingwa atashughulikiwa.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua uchaguzi wa Baraza la
Vijana la Chadema (BAVICHA) uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City,
jijini Dar es Salaam.
Alisema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na chaguzi nyingine
zinazokuja, wakibaini kiongozi wa ngazi yoyote ndani ya chama hicho
kuruhusu mgombea wa CCM kupitishwa kwa kigezo cha kupita bila kupingwa
watamshughulikia.
“Hatutakubali kabisa kiongozi yeyote ndani ya chama kuruhusu mgombea
wa CCM eti kwa sababu tu amepita bila kupingwa, tutamshughulikia.
“Pia wale ambao ni vibaraka ndani ya chama chetu, waendeleze ndoa zao na chama tawala cha CCM,” alisema Mbowe.
Akizungumzia uchaguzi wa BAVICHA, Mbowe aliwataka viongozi ambao
watachaguliwa kuendeleza yale mazuri ambayo yalifanywa na viongozi
waliomaliza muda wao.
Aidha Mbowe alisema endapo watabaini kiongozi yeyote ambaye
hataruhusu chama kikue katika eneo lake, watamng’oa katika nafasi yake
kwa kutumia Katiba yao ibara ya 6.3.4 inayoelezea kukoma kwa uongozi.
Mbowe aliwataka vijana hao baada ya kumaliza uchaguzi huo, wazungumze
na kutoka na azimio la namna ya kuwandaa vijana na wazee ili waweze
kujiandikisha katika daftari la wapigakura.
Awali akimkaribisha Mbowe, Mwenyekiti wa BAVICHA anayemaliza muda
wake, John Heche, aliwataka vijana hao baada ya uchaguzi huo kuvunja
makundi yote yaliyokuwapo wakati wanafanya kampeni.
Post a Comment