JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kumkamata Ofisa Usalama wa Taifa feki ambaye amekuwa akijipatia fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwa kuwahusisha na makosa yanayohatarisha usalama wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam; Kamishna Suleiman Kova, alimtaja ofisa huyo feki kuwa ni Saimoni Meena (40) mkazi wa Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Kova alisema mtuhumiwa huyo pia anatuhumiwa kuwasumbua wafanyabiashara mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa kuwasingizia au kuwatuhumu kwamba wanahusika na makosa yenye kuhatarisha usalama.
Alisema kwa muda mrefu Jeshi lake limekuwa likimtafuta mtu huyo kutokana na malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza na uchunguzi umebaini kuwa jina lake haliko katika orodha ya watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Alisema mtuhumiwa huyo alifanya tukio la mwisho ambalo limesababisha kukamatwa kwake alipomtishia mfanyabiashara mwenye asili ya Kisomali, Abdul Mohamed.
Alisema alimtaka ampatiwe fedha kiasi cha sh. milioni 25 vinginevyo angechukuliwa hatua chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa. Alisema mlalamikaji alitoa taarifa Polisi ndipo mtuhumiwa huyo alipokamatwa na polisi. Alisema uchunguzi zaidi unaendelea.
Katika hatua nyingine polisi wamefanikiwa kukamata bastola moja aina ya Blowning namba zake zilifutwa ikiwa na risasi 11 ndani ya magazine.
Alisema awali Polisi walibaini kundi la majambazi tisa waliokuwa wamevamia duka kwa lengo la kupora mali ambapo walifanikiwa kumkamata mlinzi wa duka hilo, Juma Adam (32) ambapo walijaribu kumfunga kwa kutumia kamba.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limeunda jopo la wapelelezi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam, Costantine, kuchunguza na kutoa taarifa sahihi kuhusu kifo cha Lebaratus Damiani, ambaye anadaiwa kifo chake kimesababishwa na polisi.
Akizungumzia kifo chake alisema kuwa, kabla ya mauti yake alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili akiwa chini ya ulinzi wa askari wa Kituo cha Stakishari.
Alisema taarifa za awali zinaonesha kwamba marehemu alikuwa na ugomvi na uhasama mkubwa kati yake na mtu aitwaye, Hamisi Magoma, ambapo katika matukio mbalimbali walikuwa wakishambuliana kila walipokutana. Alisema mara ya mwisho Damiani alikamatwa kwa kosa la kumjeruhi Magoma kwa panga.
Post a Comment