MAHAKAMA Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, jana imetupilia mbali pingamizi la awali
lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya kesi ya
kikatiba inayohoji uhalali wa Bunge Maalumu la Katiba iliyofunguliwa na
Mwandishi wa Habari, Said Kubenea.
Aidha,
mahakama hiyo hiyo ilitupilia mbali pingamzi kama hilo lililowasilishwa
na AG dhidi ya kesi ya kikatiba ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika
(TLS) na hivyo kutoa kibali kwa chama hicho kufungua kesi ya kupinga
vikao vya bunge hilo pamoja na mwenendo wa bunge hilo.
Katika
kesi ya Kubenea, Jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Augustino
Mwarija, wengine ni Aloysis Mujulizi na Dk Fauz lilitupilia mbali
pingamizi la AG jana baada ya kukataa hoja zake na kupanga kesi hiyo
ianze kusikilizwa leo asubuhi.
Kubenea
alifungua kesi hiyo kupitia Wakili wake Peter Kibatala, akiomba
Mahakama itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba, kwa
kuzingatia kifungu cha 25 (1) na (2) cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba
Namba 83 ya mwaka 2011.
Aidha,
anaiomba Mahakama itamke kama bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha
maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kwa kiwango gani.
Kabla
kesi hiyo haijaanza kusikilizwa AG aliwasilisha pingamizi la awali
akiomba Mahakama itupilie mbali kesi hiyo kwa kuwa imefunguliwa
isivyostahili, hivyo haina mamlaka ya kuisikiliza.
Kesi
ya TLS Jopo hilo lilitoa kibali kwa TLS kufungua kesi hiyo baada ya
kutupilia mbali pingamizi la AG na kusikiliza ombi la wanasheria hao
waliokuwa wakitaka Mahakama iwape kibali cha kufungua kesi.
Hata
hivyo, jopo hilo lilikataa ombi la TLS la kutaka Mahakama imuamuru
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wawasilishe bungeni muswada wa
Mabadiliko ya Sheria ya Katiba.
Jopo hilo lilisema hakuna ushahidi kwamba waleta maombi waliwaomba wanasheria hao kuwasilisha muswada huo wakakataa.
Wakati
wa usikilizwaji wa maombi hayo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
George Masaju akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata
waliomba Mahakama isitoe kibali kwa kuwa ombi hilo halina msingi
kisheria.
Aidha,
alidai Mahakama haina mamlaka ya kutoa kibali hicho kwa kuwa ombi la
TLS linahusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lakini sheria waliyoitumia kuwasilisha
ombi hilo inatumika Tanzania bara pekee.
Waliongeza
kuwa kifungu cha sheria ya mabadiliko ya Katiba wanachoomba
kirekebishwe kinahusu pande zote mbili na hawana uhakika kama wanasheria
wa Zanzibar wamehusishwa, hivyo Mahakama haiwezi kutoa uamuzi
unaozihusu pande zote mbili wakati upande mmoja haupo.
(CHANZO TOVUTI YA HABARI LEO)
Post a Comment