NA MWANDISHI WETU
WAKATI taifa
likihaha kusaka tiba ya mimba za utotoni ili kuwezesha watoto wa kike
kupata elimu, baadhi ya wauguzi wilayani Newala, Mtwara, wameibuka na
mbinu mpya.
Wauguzi hao
wanadaiwa kuwachoma sindano za uzazi wa mpango wanafunzi wa shule za
msingi, kinyume cha utaratibu kwa lengo la kuwakinga na mimba
zisizotarajiwa.
Hayo
yamebainika kupitia taarifa ya Matokeo ya Ripoti ya Utafiti uliofanywa
na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).
TAMWA
iliendesha utafiti maalumu kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa
kijinsia katika wilaya 10 nchini, kuanzia mwezi Mei, mwaka huu.
Hata hivyo,
utafiti huo umeonyesha kuwa baadhi wasichana walishindwa kuendelea na
masomo kwa sababu ya ujauzito, jambo ambalo kwa sasa wenyeji wa Newala
wamesema limekuwa historia.
Hatua hiyo
inatokana na matumizi ya sindano za uzazi wa mpango, mkakati ambao
umekuwa ukiendeshwa kwenye baadhi ya shule wilayani humo.
“Baada ya kuona
wasichana wengi wanaishia darasa la tano kwa kupata ujauzito, sasa
wanachomwa sindano za uzazi wa mpango na huo ni ushauri wa wazazi ama
wanaume wenye mahusiano nao,” alisema mkazi mmoja wa kijiji cha Luchungu
wilayani Newala.
Ofisa mmoja wa
afya (jina linahifadhiwa) wa Zahanati ya Makote, wilayani humo,
alithibitisha jambo hilo na kusema kuwa wazazi wengi wamekuwa
wakiwapeleka watoto kupatiwa huduma kuwezesha kuhitimu elimu ya msingi.
Akizindua
ripoti hiyo, Mwenyekiti wa TAMWA, Rose Reuben, alisema ripoti
imebainisha kupungua kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia nchini,
ikilinganishwa na miaka iliyopita kutokana na mwamko wa wanawake.
Alisema wanawake wengi wamekuwa wakipatiwa elimu ya masuala kupitia vyombo vya habari nchini, hivyo kupungua kwa matukio hayo.
“Kabla ya
kuanza utafiti huu mwaka 2011, takwimu za idadi ya matukio ya
unyanyasaji wa kijinsia yaliyoripotiwa, hazikuwa sahihi kama ambavyo
matokeo ya utafiti yanavyoonyesha,” alisema.
Mkurugenzi
Msaidizi wa TAMWA, Gladness Munuo, alisema takwimu za ripoti hiyo
zinaonyesha matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa katika maeneo
mengi nchini, isipokuwa wilayani Ilala, Dar es Salaam, ambapo mwaka jana
yalikuwa 124 na mwaka huu yameongezeka hadi 310.
“Katika wilaya
ya Ilala, matukio ya kubakwa ndio yameonyesha kushika kasi zaidi kuliko
aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia, ambapo takwimu zinaonyesha
kuwa watoto watano hulawitiwa kila siku,” alisema.
Akizungumzia
madhara ya dawa za uzazi wa mpango, Dk. Magreth Mathew wa Kituo cha Afya
cha Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, alisema watu wengi wanapotumia, hujiona
wapo huru na salama, hivyo kuruhusu wengine kufanya ngono zembe.
Alisema dawa
hizo zinapoingia kwenye mwili wa binadamu, mpangilio wa homoni
huvurugika hadi muda wake unapokwisha, ndipo mwili hurejea kwenye hali
yake ya kawaida.
“Dawa hizo zina
madhara yake, kwani wengine hawawezi kupata ujauzito katika hali ya
kawaida hadi wapatiwe matibabu. Hii inatokana na miili kutofautiana
homoni, ingawa kwa wengine hurejea baada ya dawa kwisha nguvu,” alisema.
Madhara mengine
ni mtumiaji kuumwa kichwa, tumbo, kupata hedhi kwa wingi bila mpangilio
maalum ama wakati mwingine kutopata hedhi kabisa.
Post a Comment