MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemruhusu Prashant Patel kubadilisha hati ya madai katika kesi aliyoifungua dhidi ya mshirika wake, Hashim Lundenga.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Frank Moshi, amemruhusu Patel kupitia wakili wake Benjamin Mwakagamba wa kampuni ya Uwakili ya BM, baada ya kuiomba mahakama hiyo kufanya hivyo ili aweze kuingiza gharama ambazo zilijitokeza baada ya kufanyika kwa shindano la Miss Tanzania, Oktoba 11, 2014.
Hata hivyo Hakimu Moshi alimtaka Patel kufanya mabadiliko ya hati hiyo ya madai dhidi ya Lundenga na kuiwasilisha mahakamani hapo kabla ya jana Jumatano.
Baada ya kuruhusu Patel kubadilisha hati hiyo ya madai, Hakimu huyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 3 kwa ajili ya kutajwa.
Patel amechukua hatua hiyo baada ya maombi yake ya kutaka kuzuia shindano hilo la Miss Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Jumamosi ya Oktoba 11, 2014 kushindikana.
Mshiriki huyo mwenza wa Lundenga kupitia wakili Mwakagamba, waliyafungua maombi hayo ya kuomba zuio hilo la shindano la Miss Tanzania chini ya hati ya dharura.
Katika maombi yake, Patel anadai Lundenga alikuwa na mpango wa kuendesha shindano hilo kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, kinyume cha sheria na bila hata ya kumwarifu.
Hivyo aliiomba mahakama itoe zuio la kufanyika kwa shindano hilo hadi shauri la msingi alilofungua litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika kesi yake ya msingi, Patel anadai pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa makubaliano ya Februari 20, 2012 na malipo ya Sh19 milioni ambayo hayajalipwa kwa mujibu wa mkataba wao na faida nyinginezo ambazo zimejitokeza hadi Septemba 23, mwaka huu.
Kupitia hati yake ya kiapo inayounga mkono maombi yake, Patel anadai kuwa yeye na Lundenga ndio waanzilishi, waongozaji na waendeshaji wa mashindano ya Miss Tanzania na wamekuwa katika hali hiyo kwa miaka 20 sasa, tangu yaliporuhusiwa tena 1994.
Post a Comment