SERIKALI imelitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuunganishia wateja umeme ndani ya siku kama watalipa kabla ya saa nne asubuhi.
Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga wakati akizungumza na menejimenti ya Tanesco mkoa wa Mwanza katika ziara yake ya kukagua miradi ya umeme.
“Baada ya Februari mwakani, mtu akija akalipia huduma ya kuunganishiwa umeme kabla ya saa nne asubuhi, saa nane mchana awe amefungiwa umeme,”alisisitiza.
Alisema ni vema mameneja wa vituo husika kuhakikisha mahitaji yaliyo muhimu ya kutendea kazi yanakuwepo, ikiwa ni pamoja na nguzo za umeme na wale ambao wanashindwa kuweka mahitaji hayo ili kuwahudumia wateja kwa wakati, basi waachie ngazi.
Alisema ni vema kila meneja kufanikisha kazi hiyo ya kutoa huduma kwa muda unaofaa na kuongeza kuwa iwapo nguzo za umeme zipo na wateja amelipia, ni vema isizidi siku tatu mteja huyo awe amewekewa nguzo na kufungiwa umeme.
“Na hili ni elekezo kwa nchi nzima. Kama kuna meneja hawezi, basi ni vema kuacha kazi. Tunahitaji kila meneja ajue Tanesco tunataka kufanya kazi kibiashara. Hawa wateja wanatuletea fedha, ni lazima tuwasikilize na tuwahudumie,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imekuwa inajitahidi kuhakikisha inaboresha miundombinu ya kila sekta na kwa hilo, Tanesco haina sababu ya mteja alipie huduma na asipate huduma hiyo haraka.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alishangazwa na mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya kwanza kutokamilika katika wilaya ya Ukerewe akihoji ni kwa nini wananchi wa wilaya hiyo hawajakamilishiwa huduma hiyo wakati awamu ya pili iko mbioni kuanza.
Alisema hali hiyo haikubaliki na kuongeza kwamba kama mkandarasi hawezi kazi, ni vema mkataba wake ukasitishwa ili kazi hiyo apewe mkandarasi mwingine.
“Kama mtu hawezi kazi, mnakaa naye vipi? Ikifika mwishoni mwa mwaka huu hajamaliza kazi, ni vema mkataba wake uvunjwe na apewe mtu mwingine,” alisistiza.
Akijibu kuhusu kuchelewa kwa huduma hiyo wilayani hapo, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mwanza, Stella Hiza alisema mkandarasi aliyepewa kazi hiyo alicheleweshewa malipo lakini tayari ameahidi kukamilisha kazi hiyo ifikapo Desemba mwaka huu.
Post a Comment