Picha
ya pamoja ya washiriki wa Warsha ya kujenga uwezo kwa maafisa wa
Serikali kutoka taasisi mbalimbali. Kutoka kushoto (waliokaa) ni Bw.
Styden Rwebangila kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Bi.Anna Shakarova
ambaye ni Mkurugenzi wa Program wa Maendeleo ya Kiuchumi, Bw. Yohane
Masara –Kaimu Mkurugenzi,Divisheni ya Mikataba kutoka Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali(katikati),Bw.Steven Sparling na Bi Clare
Power kutoka Kampuni ya Uwakili ya K&L Gates ambao ni wawezeshaji wa
Mafunzo hayo.
Bi.Anna
Shakarova ambaye ni Mkurugenzi wa program ya Maendeleo ya Kiuchumi ya
ISLP akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo.
Baadhi
ya Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia mada wakati wa mafunzo hayo.Kutoka
kushoto ni Bw.Mikidadi Rashidi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali,Bw.Juma Karibona(kati) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
-Zanzibar na kulia ni Bw.Patric Malogoi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali Tanzania.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano imeendelea kuwajengea uwezo watumishi na
wataalam katika maeneo ya sekta ya madini na gesi asilia kwa lengo la
kuimarisha uwezo wa wataalam hao katika kuandaa, kujadili na kusimamia
miradi mikubwa na mikataba ya gesi asilia nchini.
Hayo
yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba wa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.Yohane Masara wakati akifungua mafunzo
yaliyojumuisha Maafisa kutoka Wizara,Idara na Taasisi mbalimbali za
Serikali yanayofanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 13 hadi 17
Oktoba,2014.
Bw.Masara
ameeleza kuwa eneo la gesi asilia ni jipya kwa nchi yetu na hivyo
mafunzo haya yatasaidia katika kujenga uwezo wa wataalam juu ya namna ya
kufanya majadiliano na kuingia mikataba itakayoleta tija na kuchangia
katika Maendeleo ya Tanzania.
Akisisitiza
Umuhimu wa mafunzo hayo, Bw. Masara alieleza kuwa pamoja na mchango
ambao umekuwa ukitolewa na Sekta hii katika Maendeleo na uchumi wa nchi,
kumekuwepo na malalamiko na hoja mbalimbali za msingi kuwa mikataba ya
uwekezaji katika sekta ya madini ambayo Serikali za nchi nyingi za
Kiafrika zimekuwa zikiingia, ikiwemo Tanzaina haina ulingani
sawa(win-win situation) hivyo kupelekea nchi husika kupata maslahi duni
kutokana na uwekezji huo ambapo pia alieleza kuwa hali hii imekuwa
ikipelekea baadhi ya nchi kuingia katika migogoro ya kiuchumi na mara
nyingine vita vya wenyewe kwa wenyewe katika kugombania rasilimali.
Serikali
ya Tanzania kwa kulitambua suala hilo na katika kutatua Changamoto za
aina hii, imekuwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) ambao wamekuwa wakitupatia msaada wa fedha pamoja na
wataalam wa masuala mbalimbali kuandaa mafunzo maalum kwa Maofisa na
wataalam wa Serikali wa ngazi mbalimbali kwa lengo la kuendelea
kuwajengea uwezo katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inapata utaalam
stahiki hususani katika maeneo mapya ya mafuta na gesi.
Aidha
Bw. Masara aliwataka washiriki kutambua kuwa Tanzania inayo maeneo ya
kipaumbele ambayo ingependa kufaidika nayo kutokana na uwepo wa
rasilimali zilizopo hivyo kuwa makini wakati wa kufanya majadiliano ya
mikataba mbalimbali ambapo aliongeza kuwa mikataba ikijadiliwa vizuri
itachangia katika kuongeza thamani ya rasiliamali tulizonazo kwa njia ya
mitaji,teknolojia na ujuzi,mapato yanayotokana na kodi,fedha za kigeni
zinazotokana na biashara ya rasilimali hizo,kupanua wigo wa ajira na
kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kwa
upande wake, Bi. Anna Shakarova, ambaye ni Mkurugenzi wa Program wa
Maendeleo ya Kiuchumi ya Program ya Kimataifa ya Wanasheria Waandamizi
(International Senior Lawyers Project) alieleza kuwa, Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limekuwa likifanya kazi na nchi za
Kiafrika kupitia Program hiyo katika masuala ya kujenga uwezo na
kuhakikisha kuwa nchi husika zinafaidika na rasilimali zake kwa kutoa
mafunzo kwa maafisa wa ngazi mbalimbali katika maeneo ya
mikataba,masuala ya kodi,uchimbaji wa madini,mafuta na gesi. Bi.
Shakarova aliongeza kuwa Program hii imekuwa ikitafuta walimu na
wataalam kutoka katika kampuni kubwa za Kisheria za Kimataifa ambao
hujiunga na Program hiyo na huwawezesha wataalam hao kufanya kazi katika
nchi mbalimbali duniani zikiwemo nchi za Kiafrika kama Tanzania na
nyinginezo.
Akitoa
ufafanuzi wa maeneo ambayo yatahusika katika mafunzo hayo, Bw. Steven
Sparling ambaye ni mmoja wa waezeshaji kutoka kampuni ya Uwakili ya
K&L ya nchini Marekani,alieleza kuwa maandalizi ya miradi mbalimbali
katika eneo la mafuta na gesi yanahitaji umakini mkubwa na uelewa ili
kuhakikisha kuwa kila upande unaohusika unaridhirika na makubaliano
ambayo yatafanywa na hatimaye kuingia mikataba yenye tija kwa nchi
husika.
Aidha
Bw.Sparling aliwathibitishia washiriki wa mafunzo hayo kuwa atatumia
uzoefu wake wa zaidi ya miaka kumi na tano (15) alionao katika eneo hili
la gesi asilia (liquefied natural gas) kuhakikisha kuwa wanapata mbinu
madhubuti za namna ya kujadili na kusimaia miradi na mikataba katika
eneo hilo.
Naye
Bi.Clare Power,ambaye ni miongoni mwa wakufunzi wa mafunzo hayo
alisisitiza kuwa ni vyema washiriki wa mafunzo wakaonesha ushirikiano
wakati wa kujifunza kwa kuuliza maswali na kuibua mijadala ambayo
itachangia katika kuimarisha uelewa. Bi. Power ,vilevile aliahidi kutoa
ushirikiano na uzoefu wake alionao katika kufanya kazi na Serikali za
nchi mbalimbali duniani katika kuhakikisha kuwa kila mshiriki wa mafunzo
hayo anapata uelewa katika usimamizi wa masuala ya gesi asilia ili
kuhakikisha kuwa mikataba itakayohusika katika maeneo hayo inakuwa na
maslahi kwa nchi na wananchi wake kwa ujumla.
Akihitimisha
hotuba ya ufunguzi,Bw. Masara alisema kuwa mafunzo hayo ya
yanajumuisha maafisa na wataalam kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Tanzania Bara na Zanzibar,Wizara ya Nishati na Madini
(MEM),Wizara ya Fedha (MOF),Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo pia
alitumia fursa hiyo kuwashukuru waandaji wa mafunzo hayo ambao ni Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Nishati na Madini,pamoja na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Program ya
Kimataifa ya Wanasheria Waandamizi (ISLP) ambao wamekuwa wakiipatia
Serikali ya Tanzania msaada na ushirikiano katika eneo la kujenga uwezo
na kuwapatia elimu Maafisa na wataalam mbalimbali wa Serikali ya
Tanzania.
Post a Comment