MATUMIZI ya kondomu za kike yamekuwa changamoto kubwa baada ya wanawake mkoani Rukwa kukataa kuzitumia, huku wengine wakibadili matumizi yake kwa kuzivaa kama urembo wa bangili.
Hayo yalibainika hivi karibuni wakati wa ziara ya siku nne ya timu za maofisa wa asasi mbili zisizo za kiserikali za Health Actions Promotion Association (HAPA ) ya Mkoa wa Singida na Resource Oriented Development Initiative (RODI) mkoani Rukwa. Maofisa hao walikuwa wanatembelea miradi inayotekelezwa na Mradi ya Ushirikishaji wa Wanaume katika Afya ya Uzazi na Ujinsi (TMEP) mkoani hapa.
Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Rodi inayohusika na kutoa elimu ya njia sahihi ya kutumia kondomu ili kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Gideon Mpina alikiri matumizi sahihi ya kondomu za kike ni changamoto kubwa mkoani humo.
Alisema kwa kuwa kondomu hizo zina umbo la bangili, baadhi ya wanawake wanazitumia kuvaa mikononi kama urembo kinyume na matumizi sahihi ya kondomu hizo.
“Bangili za kondomu hizo zimekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake. Wanazivaa mikononi kama urembo kwani zinapendeza machoni sababu zikipigwa na mionzi ya jua zinabadili rangi mbalimbali na kuwa kivutio cha aina yake,” alisema Mpina.
Alisema imekuwa changamoto kubwa kwa Rodi kwani licha ya kuisambaza bila malipo, bado baadhi ya wanawake wanazitumia na wengine kuzinunua kutoka kwa wenzao ili tu wapate bangili.
Rodi pia inatoa elimu kuhusu malaria mkoani hapa kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Manispaa.
Naye Mratibu na Mfuatiliaji wa Shidepha+ wilayani Nkasi , Anna Laurent alikiri kuwa wanawake wengi wanakataa kutumia kondomu za kike kwa sababu wanazozijua wao wenyewe, hivyo kusababisha kondomu hizo kudoda ofisini kwake.
“Licha ya kukataa kutumia kondomu hizi za kike, lakini wamekuwa wakichangamkia kuchukua kondomu za kiume kwa wingi na kusababisha uhaba mkubwa … mahitaji ya kondomu za kiume ni makubwa kwani zinachangamkiwa na wote, wanaume kwa wanawake,” alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Sumbawanga, Dk Richard Manumba alibainisha kuwa baadhi ya wanawake mkoani humo hawapendi kutumia kondomu za kike, kwa sababu zinawafanya wasiaminike na wenzao kwa kuwa baadhi yao wanadaiwa kuzitumia zaidi ya mara moja kwa wanaume tofauti.
Post a Comment