Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Machala, Christopher Rutuku, aliyewahi kufaulisha wanafunzi wote, anadaiwa kuhamishwa shuleni hapo baada ya kutuhumiwa kuruhusu waandishi wa habari kupiga picha shule iliyojengwa kwa udongo na makuti huku ikiwa taabani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Rutuku alisema alipewa barua ya uhamisho bila kulipwa posho ya uhamisho.
Alidai kuwa uhamisho huo unatokana na tuhuma zinazotolewa na Mratibu wa Elimu Kata, Saidi Mnaguzi, kuwa aliruhusu waandishi wa habari kuandika taarifa za shule hiyo bila kupata kibali chake.
Aidha, alisema kitendo cha kutoka taarifa hizo, kilisababisha mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya kufika shuleni hapo kujionea wenyewe hali ya shule hiyo.
"Mratibu ananituhumu kuwa ziara za wakuu hao zingepaswa kuratibiwa na yeye lakini kutokana na habari zilizotoka magazetini, ziliwafanya viongozi hao kufanya ziara ya ghafla," alisema.
Mwandishi alipotaka kujua ukweli wa tuhuma hizo kutoka kwa mratibu huyo, alisema hatua ya kumhamisha mwalimu huyo inatokana na kutohudhuria kazini kwa muda unaotakiwa na pia hata kitabu cha kusaini muda wa kuingia na kutoka.
Alikanusha madai kuwa amehamishwa kwa sababu ya kuruhusu waandishi kuandika habari za shule hiyo.
Aidha, alisema mwalimu huyo amekuwa akitumia vibaya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo.
Wakati mwalimu huyo akihamishwa, wazazi wa wanafunzi wanaosoma shule hiyo wamepinga kitendo hicho na kutaka mwalimu huyo asihamishwe.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza, alitembelea shule hiyo baada ya kupata taarifa kuwa iko katika hali mbaya huku ikiwa na mwalimu mmoja tu.
Mahiza alitoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati na pikipiki itakayomwezesha mwalimu kufika shuleni kwa urahisi.
Naye Afisa Elimu wa Wilaya ya Bagamoyo Abdul Buhety, alisema mwalimu huyo alihamishwa kutokana na kutokuelewana na mratibu.
Alisema mwalimu Rutuku alijitahidi kufundisha katika mazingira magumu na kufanikisha kufaulisha watoto wote.
Shule ya Msingi Machala ilianzishwa mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 200 ambapo mwaka jana wanafunzi wa darasa la saba 12 waliweza kufaulu wote kuingia kidato cha kwanza.
Post a Comment