WANAJESHI wawili waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya
kupatikana na hatia ya kumuua Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa ndugu
wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira, wamekata rufaa kupinga adhabu
hiyo.
Wanajeshi hao ambao ni ndugu , MT 75854 Koplo Ally Ngumbe wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067
Koplo Mohamed Rashid (JKT Mbweni), wamewasilisha rufaa hiyo katika
Mahakama ya Rufani.
Katika rufaa yao, wanajeshi hao wana hoja tatu wakipinga hukumu ya
kunyongwa hadi kufa iliyotolewa Novemba 20, 2012 na Jaji Zainab Mruke wa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika hoja zao, wanajeshi hao wanadai Jaji alikosea kisheria kutoa
uamuzi kwa kutozingatia kanuni za kuthibitisha mashitaka pasipo kuacha
shaka yoyote, ambalo ni jukumu la upande wa mashitaka.
Aidha, wanadai Jaji alikosea kisheria kwa kutoa hukumu inayoegemea
ushahidi wa kimazingira, bila kuzingatia ushahidi wa utetezi wa wakata
rufaa. Katika hoja nyingine wanadai alishindwa kuchanganua itirafu
katika majina kwenye taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo.
Awali, wakati hukumu hiyo inatolewa walihukumiwa washtakiwa watatu
akiwemo aliyekuwa MT 1900 Sajenti Roda Robert wa Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) Kikosi cha Mbweni, ambaye alifariki dunia mwaka jana mkoani Dodoma
wakati akisubiri utekelezwaji wa hukumu hiyo.
Katika hukumu hiyo, Jaji Zainab alisema upande wa mashitaka
umethibitisha kesi yao bila shaka na hivyo Mahakama imeona kuwa
washitakiwa wote wana hatia na walimuua marehemu Fundikira kwa
kukusudia.
Hata hivyo, alisema hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa aliwaona
washitakiwa wanavyomuua Swetu, bali mashahidi watatu walithibitisha
kuwaona washtakiwa wakiwa na Swetu kabla ya kukutwa na mauti.
Alisema anawatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa
kwa kuwa ushahidi wa mazingira umeowanyooshea kidole washitakiwa kuwa
wanahusika na mauaji hayo.
Ilidaiwa Januari 23 ,2010 katika eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa hao walidaiwa kumuua marehemu Fundikira.
Post a Comment