WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ametoa tamko kuhusu mustakabali wa nchi kuelekea zoezi la kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu ujao na namna matukio mengi yanavyoweza kuibuka na kuashiria uvunjifu wa amani nchini.
Akizungumza na wanahabari wizarani kwake leo, Chikawe alisema kuwa kila inapofika wakati wa kuelekea chaguzi mbalimbali, kumekuwa kukitokea matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani yanayofanywa na watu ama vikundi vya watu.
Alisema matukio hayo yamekuwa yakisababishwa na hamasa za kisiasa au baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia muda huu kutekeleza ajenda zao za kihalifu kwa kisingizio cha vuguvugu za kisiasa au yote mawili.
Alivitaka vyama vya kisiasa kuepuka kufanya ushabiki wa kubeba wanachama wao kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine wakati wanapoandaa mikutano yao na badala yake wawashirikishe wanachama waliopo katika sehemu wanapotaka kufanyia mikutano hiyo.
Chikawe amesema hivi karibuni kumekuwa na matukio yanayotokana na baadhi ya viongozi wa taasisi za dini kutoa matamko ambayo yanaashiria kuingilia masuala ya kisiasa kinyume cha sheria ya vyama , sura ya 337 na kanuni zake pamoja na katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.
Alitoa mifano ya viongozi wa taasisi za dini wanapokutana na kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao wafuate maelekezo yao kuhusiana na masuala ya Katiba Inayopendekezwa au kuhusu uchaguzi mkuu ujao, matamshi ambayo yanakiuka sheria ya usajili wa taasisi hizo.
‘’Ni kweli kuwa viongozi hao wa dini wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi ila ni kinyume cha sheria kutumia uongozi wao kuwashawishi waumini wao watekeleze matakwa yao ya kisiasa,’’ alisema Chikawe.
Alisisitiza kuwa serikali itachukua hatua kali kwa watu binafsi, vyama vya siasa na taasisi za kidini zitakazobainika kuvuruga usalama na utulivu wa nchi, ikiwa ni pamoja na kufuta usajili wa vyama vya kijamii na vya kidini ambavyo vitakiuka katiba ya kuanzishwa kwao.
Post a Comment