UMOJA wa Madereva Tanzania umegomea tamko la Serikali kwa madai kuwa hoja zao za msingi hazijajibiwa kama vile walivyoagiza.
Aprili tisa madereva hao walifanya mgomo wa nchi nzima kwa masaa saba wakiishinikiza serikali kutatua madai yao ya miaka mingi ambayo hayajapatiwa majibu.
Akizungumza na MPEKUZI Katibu Mkuu wa Umoja huo, Rashid Salehe, alisema wanalipinga tamko hilo kutokana na kuwa majibu yake hayajajibu hoja zao za msingi na kwamba halionyeshi utekelezaji wake utaanza lini.
Alisema tamko hilo walikabidhiwa na Naibu Waziri wa Kazi, Makongoro Mahanga April 18 walipoenda katika wizara hiyo kwaajili ya kukutana na mawaziri walioomba kukutana nao kwaajili ya kutatuliwa hoja zao lakini hawakuwakuta.
“Tulikuwa tumeomba kukutana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Ujenzi na Miundo Mbinu pamoja na Waziri wa Kazi lakini wote hao hatukuwakuta na badala yake tumemkuta Naibu Waziri Kazi ambaye ndiye aliyetukabidhi tamko hilo ambalo halionyeshi limetokea wapi kutokana na kuwa halina muhuri wala utambulisho wowote unaoonyesha kuwa limetoka serikalini,” alisema Salehe.
Alisema pia linapingana na tamko la Waziri wa Kazi, Gaudensia Kabaka alilotamka kwenye mkutano wa hadhara wa madereva aliposema kuwa hawataenda shule kama walivyotakiwa kufanya hivyo kila baada ya miaka mitatu wanapokwenda kurudisha leseni zao.
“Sisi kama madereva hatukubaliani nalo na tunaliona kama la kitoto kwani hoja tunazodai hazijajibiwa kama vile tunavyotaka pia mawaziri wote tulioomba kukutana nao hatukuwaona wala hawajajibu hoja zetu na hata majibu tuliyopewa katika ule mkutano yalikuwa ya kututawanya,” alisema Salehe.
Alisema pia hawana Imani na kikao kilichofanywa kati ya waajiri na serikali kilichofanyika April 17 kwa madai kuwa waajili hawakuwa na madai yoyote kwa serikali hivyo katika kikao hicho uwezekano wa kukandamizwa ni mkubwa.
Alisema kuwa jana Kamati Kuu ya madereva ilikutana kujadili tamko hilo na kwamba wanatarajia kukutana na madereva wenzao April 26 maeneo ya Kimara Resort kwaajili ya kuwapa mrejesho ikiwa ni pamoja na kutoa tamko lao.
Katika mkutano na madereva uliofanyika katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo Waziri Kabaka, alisema kuwa hakutakuwa na tochi barabarani, vituo vya ukaguzi wa magari (Check Point) pia hawatatakiwa kurudi shule wataendelea na utaratibu wa zamani.
Hata hivyo katika tamko lililotolewa na serikali linasema madereva ni wafanyakazi kama walivyo wengine hivyo ni muhimu wakapata mafunzo wakiwa kazini kwenye chuo chochote kinachotambuliwa na serikali.
Post a Comment