Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwaziri, Mzee Hassan Nassor Moyo amefukuzwa uanachama wa chama hicho ambacho yeye ni mmoja wa waasisi wake, akiwa mwanachama namba 7.
Mzee Moyo (81) ni miongoni mwa viongozi waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pia wa mwaka huo na mara tu baada ya Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Kufukuzwa kwake kumetajwa kumetokana na kwenda kinyume na maadili ya chama pamoja na matamshi yasiyokubaliana na sera za chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Magharibi, Unguja, Aziza Iddi Mapuri, matamshi mbalimbali ya Moyo aliyokuwa akiyatoa katika mikutano ya hadhara inayofanywa na Chama cha Wananchi (CUF) inaonesha kwamba amekisaliti chama akiwa mzee wa kupigiwa mfano katika CCM.
Katika taarifa hiyo, imetoa mfano kuwa Aprili 30, 2014 katika mkutano wa CUF uliofanyika Kibandamaiti ambapo Katibu wa CUF, Seif Sharif Hamad alimsimamisha Mzee Moyo ambaye alisema serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari wote.
Aidha, katika mkutano uliofanyika Tibirinzi huko Pemba Februari 9, 2014 Mzee Moyo alijitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa maridhiano kutoka CCM ilhali si kweli, kwani Chama cha Mapinduzi hakimtambui kiongozi huyo.
Katika taarifa hiyo imesema CCM baada ya kutafakari kwa kina imebaini kiongozi huyo amekuwa akiongoza upotoshaji wa hali ya juu na hafai kuendelea kuwa mwanachama wa chama hicho tawala nchini.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Mzee Moyo wakati akihutubia kongamano la CUF hapo katika ukumbi wa taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni, alibeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema kwamba mkataba wa Muungano wa Aprili 22 haujulikani uliopo na wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba walikuwa hawajui wanachokifanya.
“Kutokana na matukio yote hayo na matamko anayoyatoa Mzee Moyo amepoteza sifa za kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni mfano wa kutegemewa wa wazee na vijana,” alisema.
Akizungumza na mpekuzi kwa njia ya simu kutoka Tanga, Mzee Moyo alisema hajutii uamuzi huo kwa sababu yeye hakuzaliwa kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi daima.
“Mimi sijutii kufukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi kwa sababu sikuzaliwa kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi milele......natofautiana na CCM katika mambo mbali mbali ikiwemo suala la muundo wa muungano,’’ alisema.
Katika siku za hivi karibuni Mzee Moyo katika majukwaa ya CUF amekuwa akitamka bayana kwamba muungano wa serikali mbili umepitwa na wakati na Zanzibar ipo haja ya kuwa na mamlaka kamili.
Mbali ya uwaziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya awamu ya kwanza, nyadhifa nyingine alizotumikia Mzee Moyo katika serikali ya Muungano ni pamoja na mbunge kwa muda mrefu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameshika nyadhifa mbalimbali tangu mwaka 1964 na kufanya kazi kwa karibu sana na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume kwa kuongoza Wizara ya Kilimo kwa muda mrefu akifanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani ya ASP ya kugawa ardhi kwa wananchi wote.
Ni kiongozi wa mwanzo kuwa mwanachama wa CCM ilipozaliwa mwaka 1977 baada ya TANU kuungana na ASP ambapo katika sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, alikabidhiwa kadi namba 7.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema CCM mkoa wa Magharibi ina uwezo wa kumvua uanachama, hivyo kilichofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni sahihi.
Alifafanua kuwa, kwa wanachama wa kawaida, hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa katika ngazi za chini, bali hali ni tofauti kwa viongozi akitolea mfano diwani, mbunge au mwakilishi ambao maamuzi ya kuwachukulia hatua za kinidhamu yanapaswa kufanywa na vikao vya juu.
“Kwa hiyo ndugu yangu, Halmashauri ya chama ya mkoa ina mamlaka ya kumvua uanachama mwanachama wake wa kawaida, hivyo kilichofanyika kwa Mzee Moyo ni sahihi kwa mujibu wa Katiba…kitakachokuja kwetu ni taarifa.
“Lakini mengineyo, kama kwanini amechukuliwa hatua… watu wa mkoa wa Magharibi wenyewe ndio wanaweza kueleza zaidi, sisi ni watu wa kupokea taarifa kwa kuwa Katiba inawapa nguvu ya kufanya maamuzi ya kinidhamu,” alisema Nnauye.
Post a Comment