Timu ya Uwazi kipindi chote cha mvua ilikuwa mitaani na kubaini kuwa hadi juzi watu zaidi ya kumi walipoteza maisha kutokana na mvua hiyo na baadhi ya miili iliyopatikana haijatambulika na ndugu zao na waliotambuliwa wameshazikwa na kuacha vilio.
Aidha, waandishi wetu walishuhudia jeshi la polisi likitoa maiti moja katika Mto Msimbazi uliyoko Magomeni jijini Dar es Salaam, hata hivyo haikuweza kutambuliwa hivyo kuaminika kuwa ilisombwa na maji kutoka mbali.Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova aliliambia Uwazi kuwa maiti kadhaa zilikuwa zimehifadhiwa Hospitali ya Muhimbili na ndugu walikuwa hawafahamiki na kuwataka waliopotelewa na ndugu zao kwenda kuzitambua.
Waandishi wetu katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, walibaini athari kubwa za maji yaliyoingia katika majumba ya watu hasa maeneo ya Jangwani, Kigogo, Kinondoni na wakazi wake kuachwa wakiwa hawana makazi ya kuishi, hivyo familia kusambaratika.
Maeneo ya Jangwani ilionekana kama kisiwa kwani nyumba nyingi zilizingirwa na maji na kuhamwa na wakazi wake, huku wengine wakilalamika kuwa wamepoteza mali zao ambazo zimesombwa na maji na mbwa wa polisi walitumika kusaka maiti.
Neema Laulence mkazi wa Magomeni Makuti, alisema kuwa kutokana na mvua hiyo, watu wamekosa makazi baada ya nyumba zao kujaa maji, hata hivyo alisema serikali haipaswi kulaumiwa kwa sababu viongozi wa mkoa wamejitahidi sana kuelimisha wanaoishi mabondeni ili wahame lakini wamekuwa wabishi.
Abdallah Hamis alisema: “Mvua hii ni kubwa na haijawahi kutokea na walioathirika wajilaumu wenyewe maana serikali ilishatoa viwanja Mabwepande lakini baadhi yao waliviuza na kurudi mabondeni.”Naye Mwanaisha Hamisi maarufu kwa jina la mama Kabang, alisema serikali itumie nguvu kuwahamisha watu wanaokaa mabondeni kwa sababu wanapofariki taifa linapata aibu.
“Ni aibu serikali kushindwa kuwadhibiti watu wanaong’ang’ania kuishi mabondeni. Iwahamishe kwa nguvu,” alisema Mwanaisha.Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dk. Agnes Kijazi akizungumzia hali ya mvua nchini alisema: “Maeneo ambayo hali ya mvua inaweza kuyaathiri zaidi na kukumbwa na vimbunga ni pamoja na kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa Pwani hivyo wananchi wachukue tahadhari.”
Nyumba ikizingilwa na maji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alisema anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya watu kuilaumu serikali wakati miaka mingi imekuwa ikiwahimiza wanaoishi mabondeni kuhama.
“Ukweli ni kwamba safari hii hatuwapi hifadhi kwa sababu wamekuwa jeuri na pia baadhi yao wameishitaki serikali mahakamani, sasa tufanye nini?” alihoji
“Ukweli ni kwamba safari hii hatuwapi hifadhi kwa sababu wamekuwa jeuri na pia baadhi yao wameishitaki serikali mahakamani, sasa tufanye nini?” alihoji
Post a Comment