Vyama
vya Chadema na CCM vimeingia katika mchuano wa kuwania nafasi ya
kurusha matangazo ya moja kwa moja ya kampeni za wagombea urais katika
televisheni Jumamosi hii.
Wakati
Chadema ikitaka muda wa kurusha matangazo ya uzinduzi wa kampeni za
mgombea wake, Edward Lowassa kutokea jijini Dar es Salaam, CCM inataka
kurusha matangazo ya mkutano wa kampeni ya mgombea wake, Dk John
Magufuli kutoka jijini Mbeya.
Ofisa
Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa kumekuwa na njama
za CCM kutaka kuzuia fursa ya Chadema kurusha kampeni za mgombea wake
kwa kutaka siku hiyo irushe kampeni za Dk Magufuli.
Akizungumzia
madai hayo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikiri
chama hicho kutaka kurusha matangazo ya mgombea wake na kuhoji; “tatizo
liko wapi kama Chadema imechelewa kulipia?”
“Ni
kweli mgombea wetu wa urais akiwa Mbeya tutarusha matangazo ya kampeni
zake moja kwa moja kwenye runinga, sasa ni runinga ngapi siwezi kujua
maana kuna watu wanalifanyika kazi suala hilo. Lakini kama Chadema
walijua wana tukio lao kwa nini wasingewahi kulipia?” alihoji.
Chanzo
cha habari kutoka kituo kimoja maarufu, kimeeleza kuwa kwa nyakati
tofauti, CCM na Chadema waliomba muda wa kurusha vipindi vyao, lakini
CCM ndiyo waliofanikiwa kupata.
“Ninachojua
hao wote walikuja kwa nyakati tofauti kuomba muda na CCM ndiyo
waliofanikiwa kupata,” alidokeza mmoja wa wafanyakazi wa telesheni hiyo
ambaye hakutaka kutaja jina kwa maelezo kuwa siyo msemaji.
Naibu
Mkurugenzi Mtendaji wa Azam TV, Tido Mhando alisema CCM na Chadema
vilikuwa vimeomba kurushiwa matangazo yao na vyote vimelipia. Alisema
kila moja kitapata fursa hiyo kwa kuwa kituo chake kina channel nyingi.
Hata
hivyo, mmoja wa wahariri wa Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1),
alisema: “Sisi tunarusha vipindi vyetu kulingana na matukio na mahitaji
ya jamii, hatuko fixed.” Alieleza kuwa ameamua kutoa jibu hilo rahisi
kwa kuwa alijua kwa nini mwandishi aliuliza.
“Sisi
hatuna utaratibu wa kurusha live (moja kwa moja), wanaofanya hivyo ni
watu wa radio tena huwa hilo linafanywa kibiashara. Kwamba wateja
wanaomba kutangaziwa vipindi vyao na kulipa fedha,” kilieleza chanzo
kutoka kituo kingine.
Habari zimeeleza kuwa kituo kimoja kikubwa cha televisheni kimethibitisha kurusha matangazo ya mgombea wa Chadema.
Awali, Makene alisema hadi jana, chama hicho kilikuwa kimefanikiwa kupata vituo vinne na radio nne.
Post a Comment