Mgombea
urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward
Lowassa amesema kama Watanzania watashindwa kufanya mabadiliko kwa
kupiga kura kuing’oa CCM madarakani mwaka huu, hawataweza kufanya hivyo
tena, huku akihoji kama vyama tawala mbalimbali katika nchi za bara la
Afrika vimeng’oka madarakani: “Kwa nini isiwe CCM”.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara wa kampeni katika Uwanja wa Gangilonga Iringa
Mjini uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa mji huo, Lowassa
aliyeambatana na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alisema vyama
tawala vilivyokuwa rafiki na CCM vimeshang’oka madarakani na kwamba hivi
sasa ni zamu ya chama hicho tawala kuondolewa.
“Nataka
kura nyingi ili hata wakiiba tushinde, asilimia 90 ziwe zetu hizo 10
waache waibe. Msipoiondoa CCM mwaka huu hatutaiondoa tena, CCM na Tanu
walikuwa na marafiki zao lakini karibu wote wameondoka.
“Chama
cha Kanu cha nchini Kenya kimeshaondoka madarakani, kile cha Malawi
(Malawi Congress Party) nacho kimeondoka, UNIP (The United National
Independence Party cha Zambia) nacho imeondoka na kile chama cha Mzee
Obote (Dk Militon) cha Uganda kimeondoka, tunaona pia jinsi Rais wa
Zimbabwe (Robert Mugabe) anavyohangaika,” alisema Lowassa.
Katika
mkutano huo, Lowassa alirudia vipaumbele vya ilani ya uchaguzi ya
Ukawa, huku akimponda mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi
ya CCM, Frederick Mwakalebela kuwa hawezi kushinda kwa maelezo kuwa
amepanda gari bovu.
Sumaye
alieleza ufisadi mbalimbali uliotokea tangu Lowassa alipojiuzulu mwaka
2008, huku akihoji yalipo majina ya wauza dawa za kulevya na majangili
ambayo alidai kwa nyakati tofauti Rais Jakaya Kikwete amenukuliwa
akisema kuwa anayo.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na idadi kubwa ya wananchi ambao walianza kufika
uwanjani saa nne asubuhi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Baada
ya kumalizika kwa mkutano huo saa 11.58 jioni, baadhi ya wananchi hao
walilisukuma gari la Lowassa na mgombea ubunge wa Iringa Mjini kwa
tiketi ya Chadema, Mchungaji Peter Msigwa hadi katikati ya mji huo kabla
ya magari hayo kushika kasi na kuwaacha wakiendelea kukimbia barabarani
huku wakiimba nyimbo mbalimbali.
Baadhi
yao walionekana kubeba kitu mfano wa jeneza na kukivisha bendera ya CCM
huku wakisema mwisho wa chama hicho tawala ni Oktoba 25.
Aomba kura milioni 10
Akiwa
Mafinga Mjini, Lowassa alisema anahitaji Watanzania wampigie kura si
chini ya milioni 10.2 ili awe rais na kumaliza kilio cha wakulima
nchini.
Akiwa
katika siku ya kwanza ya kampeni zake mikoani hapa, Lowassa aliwaeleza
wananchi wa Mafinga kuwa amechoshwa na manyanyaso ambayo wakulima
wanaendelea kuyapata ikiwamo kukopwa mazao yao na kutozwa ushuru na
Serikali bila ya wao kupata faida yoyote.
Lowassa
alisema mara atakapochaguliwa kuongoza nchi, kitu kikubwa
atakachokifanya kuwasaidia wakulima ni kufuta ushuru wote wa mazao na
kuhakikisha wananufaika na jasho wanalolitoa wakati wa kilimo.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Wambi, Mjini Mafinga, Lowassa alisema:
“Nakataa wakulima kuendelea kukopwa mazao yao na kutozwa ushuru,
kuendelea kufanya hivi ni kuwanyonya na kutaka waendelee kuwa maskini
wakati wao wanafanya kazi kwa kujituma sana.”
Alisema
hayo yatafanyika iwapo wananchi watampigia kura za kutosha na kuzilinda
huku akigusia madai kwamba CCM ni wezi wa kura na kubainisha kuwa
maneno hayo si ya kubeza wala kuyafumbia macho.
“Mimi
nataka kila mtu akihifadhi vizuri kichinjio chake (kadi ya kupigia
kura) na siku ya kupiga kura ikifika nawaomba wanawake kwa wanaume
wajitokeze kwenda kupiga kura ila kina baba ninawaomba mkishapiga kura
fanyeni kazi ya kuzilinda kura zenu,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Kweli CCM ni wajanja sana kazi tunayotakiwa kufanya ni kuziba mianya
yote, hata kama tukipigwa chenga wawe wamepata asilimia 10 ili asilimia
90 zibaki kwetu.”
Sumaye: Tunataka wabunge 300
Akizungumza
katika mkutano huo, Sumaye aliwataka wananchi wa Mafinga kutokuwa na
shaka na Ukawa kwa sababu wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata
ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 25, licha ya CCM kujipanga kupata
ushindi wa goli la mkono.
“Tunawaomba
Watanzania wachague Ukawa kwa sababu umefika muda wa mabadiliko,
tunataka tupate wabunge 300, hizo nafasi nyingine wagawane vyama vingine
vilivyo nje ya Ukawa,” alisema Sumaye.
Alisema
Serikali ya sasa ni dhaifu kwa sababu wamekuwa wakipeana nafasi ya
uongozi kindugu na ushikaji, hali inayofanya wananchi kuendelea kupata
shida.
“Tumemwambia
Lowassa akichaguliwa anatakiwa kuunda Serikali inayowajibika kwa umma
tofauti ya Serikali iliyopo sasa madarakani, chama kinapokuwa madarakani
kwa muda mrefu kinajenga kiburi na dharau kwa wananchi wake na ndivyo
inavyofanya CCM sasa, ni muda wake kuondoka madarakani,” alisema Sumaye.
Sumaye
alisema amekuwa akisikia CCM wakisema Magufuli hana utani na rushwa
wakati amekuwa waziri wa ujenzi kwa miaka kadhaa na bado kumekuwa na
tuhuma za rushwa katika sekta ya ujenzi.
“Nataka
kumuuliza Magufuli, yeye ni waziri wa ujenzi, ameshindwa kitu gani
kuondoa rushwa katika wizara yake halafu anakuja kusema akiwa rais
ataweza?” alihoji Sumaye.
Katika
mkutano wa pili wa Lowassa uliofanyika katika Uwanja wa Maendeleo wa
(FDC), Ilula katika Jimbo la Kilolo, aliwataka wananchi wamchague ili
awaondolee kero zinazowakabili ikiwamo ya ukosefu wa maji.
Katika
uwanja huo uliofurika huku wananchi wakiwa na mabango mbalimbali
yanayoeleza kero zinazowabali, Lowassa aliwataka wasiwe na hofu na yeye
katika kutatua kero za maji na kama wanabisha wawaulize wananchi wa Mkoa
wa Shinyanga ambao walihangaika kwa muda mrefu na kero ya maji lakini
aliwezesha mkoa huo kupata maji kutoka Ziwa Victoria.
Alisema atahakikisha elimu inapanda kwa kasi ili kupunguza umaskini. “Najivunia
na ujenzi wa shule za kata nchini kwani Mkoa wa Iringa ulikuwa maarufu
kwa kutoa wasichana wanaokwenda kufanya kazi za majumbani, lakini kwa
sasa kuwapata imekuwa shida baada ya kupatikana shule hizo ambazo
zimeleta mapinduzi hayo,” alisema Lowassa.
Kuhujumiwa
Lowassa
alisema Ukawa wamekuwa wakihujumiwa katika mchakato wa uchaguzi ikiwamo
kukataliwa kufanya mambo kadhaa na kukatwa umeme pindi mikutano ya
hadhara ya chama hicho inapokuwa ikirushwa moja kwa moja na televisheni.
“Hata
wakikakata umeme, CCM hawatatuweza, wamezoea kutuhujumu ila tarehe 25,
mwezi Oktoba hawawezi kukata umeme kwenye vichwa vya watu wanaotaka
mabadiliko."
Post a Comment