Mamia ya wanachama na mashabiki wa Chadema jana walifika katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni Dar es Salaam kumsubiri Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa baada ya kuenea habari kuwa angeingia ofisini.
Hata
hivyo,wanachama hao waliokuwa na shauku ya kumwona kiongozi huyo,
hawakufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa Dk Slaa asingefika katika ofisi
hizo kinyume na taarifa zilizokuwa zimetolewa kuhusu kurejea kwake.
Juzi mzee Philemon Ndesamburo na makada wengine wa chama walikwenda
nyumbani kwa Dk. Slaa kwa ajili ya mazungumzo, na kwamba alikubali
akasema angerejea ofisini jana
Kwa
muda mrefu Dk Slaa hakuonekana kwenye matukio muhimu ya Chadema na yale
ya Ukawa, kama wakati wa kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya chama
hicho, wakati Lowassa alipochukua kadi na alipochukua fomu ya kuwania
urais.
Kadhalika
kiongozi huyo hakuonekana katika Baraza Kuu la Chadema, mkutano wa
Kamati Kuu na Mkutano Mkuu uliompitisha kwa kauli moja kuwa Lowassa
aipeperushe bendera ya urais chini ya mwamvuli wa Ukawa.
Akihutubia
Baraza Kuu la chama hicho wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe alisema kuwa chama kiliridhia Dk Slaa apumzike wakati
mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ukiendelea baada ya Katibu Mkuu huyo
kutofautiana katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa.
Baraza
Kuu lilipiga kura ya wazi na kushauri kuwa endapo atafikiria kubadili
uamuzi wake, anaweza kuendelea na harakati za chama hicho kuelekea Ikulu
chini ya muungano wa Ukawa.
Mwandishi
wetu aliyefika katika ofisi za Chadema zilizopo katika Mtaa wa Ufipa,
Wilaya ya Kinondoni, alishuhudia idadi kubwa ya wanachama wakiwa
wamekusanyika katika vikundi wakijadili masuala mbalimbali huku
wakimsubiri Dk Slaa.
“Nimesikia
taarifa kuwa kuna watu hapa wanamsubiri Dk Slaa nikaja kushuhudia, watu
wanaongea mambo mengi kama vile Ukawa imevunjika wakati kila kitu
kinakwenda sawa hapa,” alisema Ali Mundu mmoja wa wananchama hao.
Post a Comment