TWAWEZA
inatangaza uzinduzi wa midahalo iitwayo Mkikimkiki 2015. Midahalo hii
imeanzishwa ili kutoa fursa na jukwaa kwa vyama vya siasa kunadi sera
zao kwa wananchi. Aidha midahalo hii tawapa wananchi fursa ya kuwahoji
na kuwapima wagombea na wataalamu wa vyama vikuu vya siasa.
Mfululizo
huu wa midahalo umekuja wakati muafaka. Utafiti ulidhaminiwa na
Twaweza, uligundua kuwa wananchi 8 kati ya 10 wanafikiri kuwa wagombea
ubunge (78%) na urais (79%) wanapaswa kuwa na midahalo ya pamoja. Mbali
na mikutano ya hadhara ya kampeni, wananchi wana nafasi finyu sana ya
kuwasikiliza na kuwahoji wagombea na vyama vya siasa kuhusu mitazamo,
ilani na sera zao katika nyanja mbalimbali.
Maswali ya wananchi na majibu ya hapo kwa hapo ni fursa muhimu kwa wote kupanua uelewa wa wote kuhusu sera na mipango hiyo..
Wananchi
wote wanakaribishwa kuwasilisha maswali yao kupitia mtandao na ujumbe
mfupi wa simu (SMS). Vilevile, washiriki wa mdahalo na watazamaji
wataweza kuuliza maswali wakati wa midahalo.
Tumeandaa
mfululizo wa midahalo minne itakayojikita kujadili ilani za vyama vikuu
vitano vya siasa. Midahalo hii itahusu: utaifa; uchumi na kukosekana
kwa usawa; huduma za kijamii hususan afya na elimu; na rushwa, utawala
bora na uadilifu.
Vyama
vitano vya siasa tulivyochagua ndivyo vina wagombea wengi zaidi (ngazi
ya ubunge na udiwani) kwenye uchaguzi mkuu ujao. Vimealikwa kutuma
wataalam wao kushiriki midahalo itakayojadili maeneo haya muhimu.
Wawakilishi hawa watahojiwa na jopo la wataalam wa sekta husika.
Aidha,
midahalo mitatu tofauti imepangwa kufanyika kwa ajili ya wagombea
nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa
Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kila
mdahalo utachukua masaa mawili na nusu, na utarushwa moja kwa moja na
Star TV na Radio Free Africa (RFA), vyombo vya habari vya mshirika
wetu, Sahara Media Group. Midahalo imeandaliwa na Compass Communications
na kwenye mitandao ya kijamii itaratibiwa na Jamii Forums.
Ratiba ya midahalo ni kama ifuatavyo:
TAREHE
|
MADA
|
MSHIRIKI
|
30 AGOSTI 2015
|
Utaifa
|
Mdahalo wa masuala la utaifa kuhoji ilani za vyama
|
6 SEPTEMBA 2015
|
Mdahalo wa wagombea Urais wa Zanzibar
| |
20 SEPTEMBA 2015
|
Elimu na Afya
|
Mdahalo wa masuala la elimu na afya kuhoji ilani za vyama
|
27 SEPTEMBA 2015
|
Uchumi, ajira na usawa
|
Mdahalo wa masuala la uchumi, ajira na usawa kuhoji ilani za vyama
|
4 OKTOBA 2015
|
Mdahalo wa wagombea nafasi ya Makamu wa Rais
| |
11 OKTOBA 2015
|
Rushwa/uadilifu/ maadili
|
Mdahalo wa masuala la rushwa na maadili kuhoji ilani za vyama
|
18 OKTOBA 2015
|
Mdahalo wa wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
|
Aidan
Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza amesema " Wakati huu wa
kihistoria nchini Tanzania, ni vyema wananchi wakapata taarifa za
kutosha kuhusu jinsi gani wagombea wa nafasi za uongozi wamepanga
kushughulikia changamoto zetu. Twaweza na washirika wake imedhamini
midahalo hii kuwapa fursa wananchi kuwahoji na kuwapima wagombea, pamoja
na ilani na sera za vyama vinavyoomba ridhaa yao kuwaongoza kwa kipindi
cha miaka mitano ijayo."
"Takwimu
tulizokusanya kupitia utafiti wa Sauti za Wananchi na Uwezo, zinaonesha
kuwa wananchi wameendelea kusisitiza mambo matatu," aliendelea Eyakuze.
"Kwanza, wananchi wana hamu kubwa ya kuona serikali ikifanya kazi
vizuri zaidi. Wananchi wengi waliodai kuwa wabunge wao hawakutekeleza
ahadi za uchaguzi wanasema hawatawachagua tena wabunge hao. Pili,
wananchi wametaja umaskini, na huduma duni za afya na elimu kama
changamoto za msingi zinazowakabili. Tatu, licha ya changamoto hizi,
wananchi wana matumaini makubwa kwamba maisha yao yataboreshwa na
uongozi bora pamoja na juhudi zao. Kushiriki kikamilifu katika uchaguzi
mkuu huu wa kipekee, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wagombea, ni njia
muhimu ya kuchochea mabadiliko chanya. Mkikimkiki 2015 inatoa fursa pana
na ya bure kabisa kwa vyama vya siasa, pamoja na wagombea wao, kukutana
na wapiga kura, na kunadi dira, vipaumbele and sera zao moja kwa moja.
Tunatarajia ushiriki wao mzuri na wenye hamasa kubwa."
Vyombo vya habari vinakaribishwa kushiriki lakini lazima wajiandikishe kabla ili kufanya hivyo. Tafadhali tuma barua pepe kwa pr@compass-tz.com au piga simu +255 768 129974. Hakutakuwa na posho zozote zitakazotolewa kwa washiriki.
Post a Comment