Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuzungumza na kusema yupo salama, mke wake, Josephine Mushumbusi amekanusha tuhuma zilizozagaa kuwa ndiye aliyemshauri kiongozi huyo wa Chadema kujiuzulu na kumzuia kushiriki vikao muhimu vya chama.
Tetesi
hizo zilivuma kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya
Dk Slaa kutoonekana katika vikao muhimu vya Chadema na Ukawa, kuwa
Mushumbusi hakupendezwa na kitendo cha Lowassa kupitishwa kuwania urais
chini ya mwavuli wa Ukawa na badala yake alitaka Dk Slaa ndiye awe
mpeperusha bendera.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo ambazo Mushumbusi amezikanusha, aliamua
kumfungia ndani Dk Slaa kama moja ya mbinu za kumzuia asishiriki
shughuli za kichama, tuhuma ambazo amezikanusha.
“Bosi wako akija kukuomba ushauri utamsaidia, lakini akija akakuambia ameshafanya maamuzi unaweza kupingana naye?” alihoji Mushumbusi akianza kutoa maelezo yake na kuendelea:
“Wakati
wa vikao nilikuwa namwona (Dk Slaa) anachelewa kurudi kila siku, siku
moja akaja akaniambia uamuzi aliouchukua na mimi sikuwa na la kusema,
nikachukua shuka nikajifunika.”
Katika
mahojiano yake ya kwanza baada ya kuzagaa kwa tetesi hizo, Mushumbusi
pia alikana kumfungia Dk Slaa ndani ya nyumba, akisema wakati maneno
hayo yalipokuwa yanazagaa, alikuwa nje ya nchi na wala hakujua
kinachoendelea.
“Mwenyewe
najiuliza nini kinaendelea, siwezi kufanya kitu kama hicho. Nyumba
yangu ina milango miwili, nawezaje kumfungia mtu, tena mwanamume, hata
watoto siwezi kuwafungia. Kuna mambo mengine mwanamke huwezi kuyafanya
kwa mwanamume. Mwanamume ni mwanamume tu,” alisema.
Alisema
viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanafika
nyumbani kwake na walikutana na Dk Slaa na kuzungumza naye... “Kama ningekuwa nimemfungia wangezungumza naye vipi?”
Mushumbusi alisema mwanamke anaweza kufanya chochote lakini kuna baadhi ya mambo ambayo mwanamume akiamua ni vigumu kumzuia.
Akifafanua
tuhuma za kumshinikiza Dk Slaa kujiuzulu Chadema, Mushumbusi alisema
kiongozi huyo wa Chadema ana uamuzi wake na yeye ni msaidizi tu ambaye
hana uamuzi wa mwisho kwenye familia.
Hata
hivyo, alisema endapo angeamua kumshawishi, uwezo wa kufanya hivyo anao
lakini yeye ni mwanamke mwadilifu anayependa mafanikio ya mumewe.
“Kwani unanionaje? Mimi ni ‘strong’ (nina nguvu), ningetaka ningefanya hivyo, nisingeshindwa,” alisema.
Pamoja na hayo, Mushumbusi alilalamika kuwa tuhuma hizo dhidi yake zimesababisha asisikilizwe kama ilivyokuwa awali.
Bila
kufafanua kwa undani, alisema kuna kundi linalounda propaganda hizo ili
abadili mtazamo kuhusu mumewe lakini jambo hilo haliwezi kutokea.
“Nilisema
nitampenda kama alivyo, sitajali chochote wala akiwa katika hali gani
au chama gani. Kazi yangu ni kumtia moyo ili kile atakachofanya
kifanikiwe,” alisema.
Mbali
na kukanusha vikali tuhuma hizo, Mushumbusi alisema alikwishajitoa
kwenye masuala ya siasa kwa miaka miwili sasa na badala yake ameamua
kufanya biashara ya kuuza mkaa.
“Nimenyamaza
kimya, nimekaa kando ninaendelea na biashara yangu ya kuuza mkaa, nipo
mbali na siasa na sitaki kujua kinachoendelea, kwanza hata mchakato
wenyewe siujui,” alisema.
Aliwashauri
wanawake kuacha kushabikia masuala yanayotokea ndani ya ndoa yake na
kuwataka wavae viatu anavyovivaa na wajue kuwa anapitia wakati mgumu.
Post a Comment