RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali imekusudia kupunguza gharama huduma za kutuma pesa katika mitandao ya simu kutoka nje ya nchi ili kuwawezesha Watanzania waishio ughaibuni (DIASPORA) kutumia fursa ya kijamii na kiuchumi zilizopo nchini ili kuliletea taifa maendeleo ya haraka.
Alisema
utaratibu huo utawezesha Watanzania hao kumudu gharama za ununuzi na
uendeshaji wa rasilimali mbalimbali nchini, hatua itayosaidia kukuza
wigo wa sekta ya uwekezaji nchini.
Rais
Kikwete aliyasema hayo alhamisi (Agosti 13, 2015) Jijini Dar es Salam
katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe wakati wa ufunguzi wa kongamano
lililohusisha Watanzania waishio Nje (Diaspora) na Taasisi binafsi na
Umma katika kubaini mchango wa Viwanda vidogo na vya kati katika
kuongeza wigo wa uwekezaji na ajira nchini.
“Kwa
sasa tuna huduma za Tigo pesa, M-Pesa, Airtel Money na Easy Pesa katika
mitandao yetu ya simu, hii ni hatua kubwa kimaendeleo, Watanzania
waliopo nje wanaweza kutuma kwa ndugu na jamaa kwa ajili ya kupata
huduma mbalimbali nchini” alisema Rais Kikwete.
Akifafanua
zaidi Rais Kikwete alisema lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha
Watanzania hao kubaini fursa zilizopo nchini katika sekta za umma na
binafsi na hivyo kusaidia kutengeneza wigo wa masoko katika mataifa
wanayoishi.
Aidha
Rais Kikwete aliwataka DIASPORA kuchangamkia fursa za uwekezaji
zilizopo nchini ikiwemo ardhi, ambapo kwa sasa Serikali kupitia Wizara
ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imeanzisha dawati maalum la kuwasaidia
DIASPORA kupata viwanja vitakavyopangwa kuuzwa na Serikali katika sehemu
mbalimbali nchini.
“Taifa
letu limepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika Nyanja mbalimbali,
nawaomba mtumie ujuzi na maarifa mliyonayo katika kuongeza zaidi
maendeleo haya, kwa mfano hivi karibuni tulipokea madaktari Watanzania
waishio nchini Marekani walioendesha huduma za matibabu katika hospitali
za hapa nchini” alisema Rais Kikwete.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula alisema Watanzania waishio Ughaibuni
ni rasilimali katika maendeleo ya nchi, kwa kutambua umuhimu Serikali
imeboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo uimarishaji wa mifumo ya
biashara na uchumi.
Balozi
Mulamula alisema Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Kimataifa cha
Biashara kimeandaa kongamano hilo ili kuwawezesha Diaspora kwa
kushirikiana na taasisi za uzalishaji mali nchini katika kukuza biashara
ndogondogo na kati.
Naye
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Filiberto Sebregondi alisema Umoja
huo upo tayari kushirikiana kwa karibu zaidi na Tanzania katika
jitihada za kukuza uchumi kupitia jumuiya za Watanzania waishio
Ughaibuni (Diaspora).
Kongamano hilo linatarajia kumalizika siku ya Jumamosi tarehe 15 Agosti, 2015 limebeba kauli mbiu ya “mtu kwao,wekeza nyumbani”
Post a Comment