RAIS Jakaya Kikwete ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, kuanzisha mara moja mfumo wa ulipaji faini kwa njia ya Benki na mitandao ya simu za mkononi ili kupunguza ushawishi wa vitendo vya rushwa kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani nchini.
Pia,
ameagiza kuanzishwa mfumo wa kuweka alama kwenye leseni za madereva
wanaokiuka sheria na kutumia njia hiyo kuwafungia, ikiwa ni hatua
mojawapo ya kudhibiti wimbi la ajali za barabarani hapa nchini.
Rais
Kikwete alitoa agizo hilo jana katika viwanja vya Tangamano wakati
alipokuwa akizindua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani Kitaifa,
inayofanyika mkoani Tanga, ikiwa imebeba kaulimbiu inayosema ‘Endesha
Salama, Okoa Maisha’.
Alisema
asilimia 56 ya ajali za barabarani, zinatokana na uzembe na ukosefu wa
umakini kwa madereva na kwamba hatua hiyo inasababisha vifo, majeruhi na
uharibifu wa mali na hata kuathiri ustawi wa Kaya na Uchumi wa Taifa.
“Hivi
mpaka sasa Baraza na Kikosi cha usalama barabarani wanashindwaje
kutumia mifumo ya kidigitali kwa nini mpaka leo hakuna kamera
barabarani? Kwanza ingesaidia kudhibiti ajali na uvunjaji wa sheria,
lakini hata vitendo vya rushwa ambavyo navyo vinachangia ongezeko hili
la wimbi wa ajali hapa nchini,” alisema Rais Kikwete.
Alisema
katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2010 hadi 2014, jumla ya
watu 19,264 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani na kwamba
idadi ya ya waliokufa katika kipindi cha mwaka peke yake ni watu 3,534
sawa na idadi ya wanaopeteza maisha kutokana na ugonjwa wa malaria.
Kufuatia
hatua hiyo, amelitaka baraza hilo kufanya mapendekezo ya marekebisho ya
sheria za usalama barabarani hasa pale penye mapungufu ili kuweza
kusaidia kudhibiti wimbi la ajali linalochangia upotevu wa nguvu kazi ya
Taifa.
“Kikosi
cha usalama barabarani kiongeze kasi ya kudhibiti ajali za barabarani
na kuwachukulia hatua za kisheria Askari wanaojihusisha na vitendo vya
rushwa….lakini lisilale katika kutoa elimu ya sheria za usalama
barabarani hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,” alisisitiza Rais Kikwete.
Kwa
upande Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,Naibu
Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mohamed Mpinga alisema lengo kuu la
maadhimisho ya siku hiyo ni kuhamasisha matumizi salama ya barabara
pamoja na kuwakumbusha watumiaji namna rahisi ya kutumia barabara ili
kupunguza ajali zisizo za lazima.
“Tunapoadhimisha
siku hii tunawakumbusha watumiaji kuwa ajenda kuu ya Taifa ni mapambano
dhidi ya ajali za barabarani, jambo ambalo linaweza kuadhibitiwa kwa
sababu ya uzembe na uvunjaji wa Sheria za Barabarani”,alisema Kamanda Mpinga.
Hata
hivyo, alisema katika maadhimisho hayo Baraza limejipanga kufanya
Mkutano Mkuu wa wadau utakaoshirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, sambamba na mafunzo kwa madereva 300 wa daladala na
walimu 200 wa shule za msingi kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu sheria
za usalama barabarani.
Post a Comment