TAIFA STARS YAANZA MAZOEZI
KIKOSI
cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kimeanza mazoezi katika
uwanja wa Karume kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa
Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Wachezaji
wa Taifa Stars chini ya kocha wake mkuu Charles Mkwasa watakua
wakijifua mara mbili kwa siku asubuhi na jioni katika uwanja wa Karume
katika kujiweka fit na maandalizi ya mchezo huo.
Kufuatia
baadhi ya wachezaji kuwa na majukumu na timu zao kujiandaa na mchezo wa
Ngao ya Hisani utakaochezwa Agosti 22, Mkwasa amewaongeza wachezji
wengine kumi (10) kutoka katika orodha yake ya akiba.
Lengo
la kambi hii ya awali ya siku tano, ni kocha mkuu pamoja na benchi lake
la ufundi kupata nafasi ya kuwaona wachezaji katika mazoezi hayo kabla
ya safari ya kuelekea nchini Uturuki Agosti 23 mwaka huu kwa kambi ya
siku kumi.
Wachezaji
walioitwa na kuanza mazoezi leo ni Said Mohamed, Vicent Andrew (Mtibwa
Sugar), Mohamed Hussein, Ibrajim Hajibu (Simba SC), Hamis Ali, Juma
Mbwana (KMKM), Tumba Sued (Coastal Unioni), Samuel Kamuntu (JKT Ruvu),
Ibrahim Hilka (Zimamoto– Zanzibar) na Mohamed Yusuf (Prisons).
Wachezaji
wengine waliopo kambini ni Said Ndemla, Hassan Isihaka, Abdi
Banda(Simba SC), Rashid Mandawa (Mwadui FC), Michael Aidan (Ruvu
Shooting), Orgeness Mollel (Aspire Academy) na Abdulhaman Mbambi
(Mafunzo).
TWIGA STARS KUIVAA HARAMBEE STARLETS
Timu
ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) iliyopo kambini
kisiwani Zanzibar, inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya
taifa ya Wanawake kutoka Kenya (Harambee Starlets) Agosti 23, 2015.
Mchezo
huo wa kirafiki utachezwa katika uwanja wa Aman Kisiwani Zanzibar,
ikiwa ni sehmu ya maandalizi ya kikosi hicho kujiandaa na fainali za
Michezo ya Afrika (All Africa Games) zitakazofayika nchini
Congo-Brazzavile kuanzia Septemba 4 – 19, 2015.
Twiga
Stars inaendelea na mazoezi kutwa mara mbili katika viwanja vya Aman na
Fuoni chini ya kocha wake mkuu Rogasian Kaijage kujiandaa na fainali
hizo za michezo ya afrika, wachezaji wote waliopo kambini wapo katika
hali nzuri wakiendelea kujifua na michezo ya Afrika.
USAJILI Dirisha
la usajili limeongezwa toka tarehe 06 Agosti hadi tarehe 20 Septemba,
baada ya muda huo klabu itakayochelewesha kuleta usajili wake itatozwa
kiasi cha shilingi laki tano (Tsh 500,000) kwa kila mchezaji
itakayemsajili mpaka siku ya tarehe 30 Agosti.
Mwisho wa kufanya uhamisho wa kimataifa wa wachezaji kwa njia ya mtandao TMS ni tarehe 6 Septemba.
Kikao
cha kamati ya sheria kitakaa tarehe 28 kwa ajili ya kuupitisha usajili
na kitakaa tena tarehe 8/9/2015 kwa ajili ya kupitisha usajili.
Kuanzia
tarehe 21 hadi 27 itakuwa ni wiki ya pingamizi, ambapo majina
yatabandikwa TFF Karume na kuwekwa kwenye mtandao ili kuwezesha vilabu
vyenye pingamizi kuwawekea wachezaji mapingamizi.
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuanza tarehe 12 Septemba 2015, Daraja
la kwanza (FDL) ikitarajiwa kuanza Septemba 17 na Ligi Daraja la pili
inatarajiwa kuanza Oktoba 16 mwaka huu.
MICHUANO YA COPA COCA-COLA 2015
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) bado linaendelea na mazungumzo na
wadhamini wa michuano hiyo (Coca-Cola). Kutokana na mazungumzo
hayo, ratiba ya michuano hiyo itachelewa kutoka.
Hivyo, tunawaomba kuwa na uvumilivu wakati mchakato wa mazungumzo hayo yanayokaribia ukingoni ukiendelea.
UAMUZI
WA KAMATI YA RUFAA YA TFF JUU YA RUFAA YA DR. DEVOTA JOHN MARWA,YA
MAAMUZI YA KAMATI YA UCHAGUZI WA SOKA LA WANAWAKE (TFF)
Mwomba
rufani, Dr. Devota John Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika
taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri katika kitengo kinachojihusisha na
taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiamini kwamba
anakidhi vigezo vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea uenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Miguu wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba kugombea
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho.
Maombi
hayo yalikumbana na pingamizi zilizoletwa na wakereketwa wawili wa soka
la Wanawake, Bi. Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja
walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni za
ugombea wa nafasi ya Mwenyekiti.
Waleta
mapingamizi walidai kuwa Mrufani hakuwa na sifa zilizoainishwa katika
Kanuni za Uchaguzi za T.F.F. (TFF Electoral Code) Ibara ya 9 (tisa)
kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na uongozi
wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Aidha
Ibara ya 28 (ishirini na nane) kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka
mgombea awe amejihusisha japo miaka 2 (miwili) katika shughuli za
maendeleo ya mpira wa miguu nchini. Kamati ya Uchaguzi iliridhia
mapingamizi hayo na kuliondoa jina la Mrufani katika orodha ya wagombea
wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti. Rufani hii ni matokeo ya uamuzi huo wa
Kamati ya Uchaguzi uliotolewa taraehe 22 Julai, 2015.
Kwa
ujumla, sababu za kupinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zinaweza
kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni iliyojikita juu ya hitilafu katika
kuamua kwamba Mrufani hakuwa na uzoefu katika uongozi wa soka kwa muda
ulioainishwa. Sabau nyingine ni kwamba Kamati ya Uchaguzi illibua sababu
ambayo haikuwa katika Hati ya pingamizi iliyoletwa na Mleta pingamizi.
Wakati
ambapo Mleta pingamizi alijikita katika kipengele cha 28(3), Kamati
iliibua kipengele cha 28(8), cha Katiba ya TWFA kinachomtaka mgombea awe
ametimiza uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, ambacho hakikuwemo katika
hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mleta pingamizi.
Katika
kufikia uamuzi wake, Kamati ya Rufani ilizipitia sababu za Mrufani kama
zilivyoletwa, na baada ya kusikiliza maelezo ya Mrufani na hoja za
Mwakilishi wa TFF, Wakili Msomi Edward Augustino, na imeamua kama
ifuatavyo. Tutaanza na hoja ya mwisho.
Je,
Kamati ilikuwa sahihi kuibua kipengele ambacho hakikuletwa katika hati
ya mapingamizi? Kamati inaweza kuibua kipengele hicho endapo kwa kufanya
hivyo, itakuwa imejielekeza katika nia njema ya maslahi ya suala
linalozungumziwa.
Sharti
jingine ni kwamba hoja hiyo inyoibuliwa isiwe na athari
hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika suala hili hata hivyo, hoja
iliyoletwa na Mleta pingamizi, yaani hoja chini ya kifungu cha 28 (3),
imeainisha kipindi kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na Kamati inahitaji uzoefu wa miaka 5.
Endapo
Mrufani angekuwa na uzoefu wa miaka 3 hadi 4, bado angekwama kutokana
na hoja iliyoibuliwa na Kamati. Hii kwa vyovyote ingekuwa ni athari hasi
(negative impact) katika harakati za Mrufani. Ni vema
Kamati
zinazosikiliza malalamiko zikajikita kwenye malalamiko yaliyoletwa na
wahusika wenyewe. Kama pigamizi lingekuwa liko juu ya kipengele hicho
tu, tusingesita kukubaliana na sehemu hii ya rufani. Hata hivyo, takwa
la uzoefu wa miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara ya 9 (3), ambayo
ilikuwa ni sehemu ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya
mapingamizi.
Kwa
sababu hiyo, Kamati ya Rufani haioni kama hoja hiyo ina mashiko.
Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani ya rufaa hii ni je, Kamati ya
Uchaguzi ilijielekeza vema kuhusu suala la uzoefu wa uongozi
ulioainishwa na Katiba?
Mrufani
ameieleza Kamati ya Rufani mlolongo wa shughuli ambazo amekuwa
akizifanya, nyingi zikiwa zimejikita zaidi katika taaluma. Miongoni mwa
shughuli hizo ni kuandaa Mpango Mkakati wa kuendeleza soka la wanawake.
Mpango huu uliridhiwa na kuwasilishwa Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira
Duniani, yaani FIFA.
Maelezo
mengine ni kushiriki katika kuongoza timu mbali mbali kule Chuo Kikuu,
zingine zikiwa za watoto wadogo ambao baadhi ya matunda yake ni
wachezaji walioibukia kwake kama vile Simon Msuva. Alisema zaidi kuwa
alishiriki kuandaa warsha ilizoandaliwa kwa ushirikiano kati ya FIFA na
TFF.
Aidha.
Alisema kuwa amekuwa kiongozi tangu akiwa bado kwenye vyuo vya ualimu,
na baadaye alipohitimu na kufanya kazi kama Mwalimu, kabla ya kujiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliko mpaka sasa. Akasema, hata
alipokuwa Sweden kwa masomo ya juu pia lijihusisha na programu za
maendeleo ya soka la wanawake.
Wakili
msomi wa TFF akijibu hoja hizo, alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi kuwa Mrufani hajaonesha popote kwamba amewahi kuongoza soka,
akasema Mrufani ni mtaalamu tu kama msomi, jambo linaloweza kufanywa na
msomi yoyote. Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya Rufani za Uchaguzi
kuitupilia mbali rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.
Tofauti
na Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani imeona kuwa kwa maslahi mapana
ya mchezo wa soka katika ujumla wake, ni vema kuweka tafsiri pana (wide
interpretation) juu ya sifa zinazozungumzwa, badala ya kuweka tafsiri
finyu (restricted/narrow interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya
Uchaguzi.
Baada
ya kufanya hivyo, kuhusiana na Mrufani, Kamati imeona kuwa ana sifa
zinazostahili. Kupitia sababu alizozitoa, na vielelezo vyake, Kamati ya
Rufani haina wasiwasi kuwa Mrufani ana uzoefu mbali mbali sio katika
soka tu, bali pamoja na michezo katika ujumla wake.
Tumeshuhudia
katika maelezo yake kwetu kwamba ushiriki wake katika hatua mbali
mbali, japo hakuwahi kuchaguliwa, sio ushiriki wa kitaaluma tu, kama
msomi mwingine yeyote. Ni ushiriki wenye dhamira ya dhati ya kuleta
mabadiliko/maendeleo katika soka la wanawake. Maelezo
yake
kuwa aliaandaa programu ya maendeleo ya soka la wanawake, hayakupingwa.
Kamati ya Uchaguzi ingeangalia namna ambavyo “visheni” iliyomo katika
programu ile ambavyo ingeweza kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa. Kwa hiyo,
katika hoja hii, Kamati inakubaliana kuwa Mrufani
anazo
sifa stahiki, na kukatwa kwa sababu hii, Kamati ya Uchaguzi
haikujielekeza vema. Kwa hiyo, Mrufani ameshinda rufaa yake? Kamati ya
Rufani inachelea kujibu swali hili moja kwa moja. Utaratibu wa
kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa kisiki.
Chini ya Ibara ya 13 (1) cha Kanuni ya
Uchaguzi
(Electoral Code), mgombea ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha
rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.
Kipengele
cha 3 (tatu) cha ibara hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na
uhalali endapo rufaa yake imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo.
Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa
ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe
28 Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa
na kanuni, na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.
Japo
katika mwenedo na maamuzi yake Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi
na taratibu za kimahakama, suala la muda wa kuwasilisha rufani sio
miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza kutoyazingatia. Kwa sababu
hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti na zile za Kamati ya
Uchaguzi.
Pamoja
na uamuzi huu, Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya
kipekee kumpongeza Mrufani kwa jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia
TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa hatokata tama, na kwamba atakuwa
tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia taalum yake, kushirikiana na
wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la akina mama lililo na
changamoto lukuki.
Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Post a Comment