Wakati
kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea kushika kasi, ahadi za mgombea
urais Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa zimeanza
kuichanganya Serikali na jana Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliibuka
na kudai mgombea huyo anaahidi mambo ambayo tayari yanatekelezwa na
Serikali ya CCM.
Ahadi
ambazo zimemshtua Sitta ni ile ya ujenzi wa reli mpya ya kati na
kufufua shirika la ndege la Serikali (ATCL) alizozitoa Lowassa wakati wa
uzinduzi wa kampeni zake.
Akizungumza
na wanahabari jana, Sitta ambaye ni mjumbe katika timu ya kampeni ya
mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli alisema amemsikia Lowassa akisema
atajenga reli ya kati na kufufua ATCL, wakati Serikali ya CCM
ilishaanza utekelezaji wa miradi hiyo.
Hata
hivyo, wakati Sitta akisema Rais Jakaya Kikwete atazindua ujenzi wa
reli hiyo kwa kiwango cha kimataifa itakayogharimu Dola 7.6 bilioni sawa
na Sh16 trilioni, alisema mazungumzo kuhusu mkopo kutoka katika Benki
ya Rolthschild ya Marekani kwa ajili ya ujenzi huo yanaendelea.
“Namshangaa
Lowassa anasema atajenga reli na kufufua ATC wakati hii ni mipango ya
Serikali ambayo ipo katika hatua za utekelezaji,” alisema.
Sitta alisema Rais Kikwete atazindua ujenzi wa reli hiyo Septemba 15, mwaka huu, katika eneo la Soga Mpiji wilayani Kisarawe.
“Hivi
ni mgombea gani wa urais ambaye hafahamu kuwa reli hii inajengwa na
Kikwete, atafute mradi mwingine huu wa reli amechelewa,” alisema Sitta.
Alisema
reli hiyo itakayokuwa na kilomita 2,561, itajengwa na Kampuni ya China
Railways Construction Corporation kutoka Dar es Salaam – Kigoma, Tabora –
Mwanza na Kaliua – Mpanda.
Mradi huo ukikamilika, utawezesha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa treni ya mwendo wa wastani wa kilomita 120 kwa saa.
Alisema
reli hiyo ikikamilika, itakuza uchumi wa Tanzania na nchi za Maziwa
Makuu za Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC).
Alisema
pamoja na kwamba kuna reli inayojengwa kutoka Mombasa, Kenya hadi
Kigali, Rwanda baadhi ya nchi za Maziwa Makuu zitatumia reli ya Tanzania
kwa sababu kijiografia kuna umbali mfupi. Alisema mradi huo utakaoanza
mwaka huu, utakamilika mwaka 2021.
Pia,
alisema itajengwa reli nyingine kutoka Mtwara hadi Mbambabay ili
kuwezesha makaa ya mawe na chuma kusafirishwa hadi katika Bandari ya
Hindi.
Kuhusu ATC
Akizungumzia
ahadi ya shirika la ndege, Sitta alisema hata bila ahadi ya Lowassa,
Serikali italifufua shirika hilo ili liweze kununua ndege nne na kuanza
biashara kama ilivyokuwa zamani.
Alisema
Serikali itachukua madeni yote ambayo shirika hilo linadaiwa ili liweze
kukopesheka... “Unajua shirika likiwa na madeni haliwezi kupata
mikopo,” alisema.
Alisema
Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), italikopesha shirika hilo ili
linunue ndege nne, Boeing mbili na Jet mbili. Alisema ndege hizo
zitakuwa zikifanya safari za ndani na nje ya nchi na zitajiendesha na
kurudisha madeni yake.
“Tunaendelea kuwalipa mishahara marubani wetu ili waendelee kuwa na sifa za kuendesha ndege mara zitakaponunuliwa,” alisema.
Waziri huyo wa Uchukuzi, aliahidi kuwa ndege hizo zitaanza kufanya kazi ndani ya miezi 12 kuanzia sasa.
Ufisadi TRL
Waziri
Sitta pia alizungumzia ufisadi katika ununuzi wa mabehewa 274 ya
Shirika la Reli Tanzania (TRL), kutoka India kuwa watuhumiwa
watafikishwa mahakamani baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
kukamilisha kazi hiyo.
Sitta
alikuwa akijibu hoja za Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyesema
katika uzinduzi wa kampeni za Ukawa na Chadema kuwa mradi huo ni
miongoni mwa matukio saba ya kifisadi yaliyotokea wakati Lowassa hayuko
serikalini.
Hata hivyo, Sitta alisema: “Siwezi kufahamu ni lini watafikishwa mahakamani kwa kuwa suala hilo sasa liko mikononi mwa DPP, kazi yangu nilishaimaliza.”
Alisema
kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo imeshakamilisha kazi yake na
kuonyesha kwamba kulikuwa na uzembe kwa watendaji wa TRL uliosababisha
kununuliwa kwa mabehewa hayo.
Alisema
kamati hiyo ilikwenda hadi India kuichunguza kampuni iliyotengeneza
mabehewa hayo na kubaini zabuni kuwa haikuwa na sifa na hivyo watendaji
TRL walikiuka kanuni za ununuzi ya Serikali kwa kitendo cha kutoa fedha
zote kwa kampuni hiyo kabla ya kupokea mabehewa.
Waliosimamishwa
kutokana na sakata hilo ni Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu,
Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomile Ngosomile, Mhasibu Mkuu, Mbaraka
Mchopa, Mkaguzi wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Ununuzi
Ferdinand Soka.
Azungumzia Richmond
Alipoulizwa
sababu za kuibua upya suala la Richmond juzi kwenye kampeni Mjini
Shinyanga wakati alishalifunga bungeni alipokuwa Spika, Sitta alisema
hawezi kulizungumzia kwa kofia yake ya Waziri wa Uchukuzi akaahidi
kufanya hivyo kwenye majukwaa ya siasa kwa kuwa yeye ni mjumbe wa kamati
ya kampeni ya CCM.
Alisema
pamoja na kuwa Serikali iliachiwa utekelezaji wa maazimio kuhusu kashfa
hiyo, anapopanda kwenye majukwaa ya kisiasa lazima aeleze kile
anachokifahamu kwa sababu anayetafutwa hivi sasa ni mkuu wa nchi.
Kuhusu
wizi wa kura, Sitta alisema Ukawa wanawaaminisha watu kwamba CCM itaiba
kura, akihoji itaiba vipi wakati kila mgombea anakuwa na wakala katika
kila kituo na kufafanua kuwa wanawaandaa wananchi kisaikolojia kukataa
matokeo.
Post a Comment