Jaji Salvatory Bongole amesema Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 aliyoitumia kufungia gazeti hilo lililokuwa linachapishwa kila Jumatano na kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL), inaelekeza kuwa pamoja na hatua nyingine kutaka maelezo ya utetezi kwa mchapishaji.
Katika uamuzi wa shauri lililofunguliwa mara baada ya MwanaHALISI
kufungiwa, Jaji Bongole amesema gazeti hilo liko huru kuchapishwa
kuanzia sasa.
Jaji huyo amesema pamoja na uamuzi huo, kampuni iliyolalamika imepewa
mafao yote iliyoyaomba katika kufungua shauri hilo la mapitio ya uamuzi
wa Waziri – prerogative orders.
Miongoni mwa maombi ya faida ni HHPL kulipwa gharama za kesi pamoja na
fidia kutokana na hasara iliyopatikana kwa muda wote wa gazti hilo kuwa
kifungoni.
Wakati Waziri alipofungia gazeti la MwanaHALISI, alieleza kwamba sababu ni kuandika habari na makala za uchochezi.
Habari hasa iliyoikera serikali hata kujilazimisha kuchukua hatua hiyo
katili, ilikuwa ni iliyohusu uchunguzi wa tukio la kutekwa na kuteswa
hadi karibu na kifo kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari
Tanzania (TMA), Dk. Steven Ulimboka.
Dk. Ulimboka alikumbwa na mkasa huo mnamo Juni 2012 alipotekwa usiku
eneo la Tazara, karibu na viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, ambako
aliitwa na mtu aliyemtaja kuwa ni ofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye
alikuwa na mawasiliano ya karibu naye kwa saa kadhaa siku chache na
usiku huo siku ya tukio.
Daktari huyo aliyekuwa mtumishi wa taasisi ya Marekani nchini, alifika
eneo la Tazara akifuatana na daktari mwenzake aitwaye Deo, ambaye mara
baada ya tukio hilo, wakati wa alfajiri, alimpigia simu Mhariri wa
MwanaHALISI, Jabir Idrissa, kumjulisha kuhusu kutekwa kwa Dk. Ulimboka.
Kufuatia habari za kuachiwa huru kwa MwanaHALISI, Mhariri huyo amesema
amefurahishwa na uamuzi wa mahakama ya Tanzania, kwa kuwa umethibitisha
kosa la serikali la kujichukulia maamuzi mkononi chini ya kuvunja sheria
ilizoahidi kuzilinda.
“NImefurahi sana kuthibitishiwa kwamba serikali ilikosea katika kufungia
gazeti. Uamuzi wa jaji umesema waziri hakufuata hatua za kisheria
alizopaswa kuchukua kabla ya kufungia gazeti, ikiwemo ya kuwapa wamiliki
na mhariri nafasi ya kujitetea,” amsema Idrissa.
“Lakini pia uamuzi huu unatakiwa uwe funzo muhimu kwa utawala kwamba
hauwezi kudumu na kudumu kwa msisitizo wa kuhifadhi na kufurahia sheria
zilizopitwa na wakati ambazo miaka kadhaa nyuma zilishatangazwa kuwa ni
sheria kandamizi,” alisema.
Mhariri amesema anawasiliana na mmiliki na mchapishaji wa MwanaHALISI,
kampuni ya HHPL, kukamilisha taratibu za kuchapisha toleo la kwanza
haraka iwezekanavyo. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa
wiki siku ya Jumatano.



Post a Comment