Mabango yenye picha ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, yanayoendelea kubandikwa katika maeneo mbalimbali nchini yamezua kizaazaa, baada ya mengine kuondolewa na wale wanaofanya kazi ya kuyaweka kutishwa na hata kuwekwa ndani na Jeshi la Polisi.
Hali
hiyo imejitokeza mkoani Iringa, ambako vijana wanaofanya kazi ya kuweka
mabango hayo waliwekwa ndani na Jeshi la Polisi na jijini Dar es Salaam
ambako bango lililokuwa limewekwa katika Soko la Kariakoo liliondolewa
saa chache tu baada ya kubandikwa na hivyo kuzua mjadala kila kona.
Wakati
wale waliokamatwa mkoani Iringa wakidaiwa kuwekwa ndani pasipokuwa na
sababu yoyote hadi pale walipotolewa na maofisa wa Chadema, Jijini Dar
es Salaam bango hilo liliondolewa na uongozi wa Soko la Kariakoo kwa
madai ya kubandikwa kimakosa.
Juzi
saa 12 jioni wafanyakazi wa kampuni ya Platnum Media Co. Ltd walifika
sokoni hapo na kuanza kubandika bango hilo lililokuwa na picha ya
Lowassa, ikiambatana na maandishi yanayosomeka; ‘Edward Lowassa…Ni
wakati wa mabadiliko’.
Wakati
bango hilo likibandikwa umati mkubwa ulikusanyika karibu na eneo hilo
na kuanza kushangilia, huku wengine wakiimba “Rais…rais…rais”.
Akizungumza
na mtandao huu, Meneja wa Soko la Kariakoo, Florens Seiya, alisema
yeye ndiye aliyetoa amri ya kuondolewa kwa bango hilo kwa kuwa soko hilo
ni taasisi ya umma na hairuhusiwi kuwekwa mabango ya kampeni.
“Ni
kweli tunamfahamu aliyebandika bango hilo, ni mtu ambaye tuna mkataba
naye wa kutumia ubao huo kubandika mabango, lakini hili lilibandikwa
kimakosa bila kutushirikisha,” alisema Seiya.
Alisema
katika mkataba wa soko hilo na kampuni ya Platnum Media Co. Ltd,
kifungu cha sita kinamtaka aonyeshe maudhui yaliyomo katika mabango
kabla ya kubandika, kitu ambacho yeye (Platnum) hakufanya.
“Jana
(juzi) baada ya kufunga ofisi na kuondoka ndipo alipofika na kuanza
kuweka bango hilo, jambo lililofanya watu wakusanyike kwa wingi
utafikiri pana mkutano wa siasa huku wengine wakishangilia,” alisema
Seiya.
Alisema
kutokana na soko hilo kuwa ni taasisi ya umma, hairuhusiwi kuweka
tangazo lolote linalohusu kampeni za kisiasa kwa kuwa wao hawafungamani
na chama chochote.
“Hebu
angalia mwenyewe (huku akionyesha rekodi ya video ambayo inaonyesha
watu walivyojaa huku wakishangilia wakati bango hilo likiwekwa) nani
angeweza kuilinda amani mahali hapa,” alisema.
Aliongeza
kuwa hata hivyo, wamemwandikia barua mteja wao huyo, Platnum ajieleze
kwa nini alivunja kifungu hicho kinachomtaka apeleke maudhui kabla ya
kubandika chochote.
“Kifungu
cha sita cha mkataba kinasema kuwa soko la Kariakoo lina haki ya
kukataa matangazo yasiyoruhusiwa kisheria na tamaduni za nchi… hawa
Platnum tunafanya nao biashara kwa takribani miaka nane na hajawahi
kubandika chochote bila sisi kukiona,” alisema Seiya.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo walisema
kuwa hizo ni njama za wana CCM kwa kuwa watu walijaa na kushangilia
sana.
Mmoja
wa wafanyabiashara hao, Hamisi Napinda, alisema saa 12 jioni wakati
bango hilo likiwekwa, polisi walifika muda huo huo na baada ya wao
kuondoka tu wakaliondoa.
“Jana
(juzi) muda mfupi baada ya kubandikwa bango la Lowassa askari walifika
na difenda mbili walipoondoka tu likabanduliwa, hii ni hujuma
wanazomfanyia,” alisema Napinda.
UKAWA kushitaki
Mwenyekiti
mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amewataka
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuacha kufanya siasa za uchochezi
na badala yake wafanye siasa safi zinazojikita katika hoja.
Umoja
huo pia leo unatarajia kuwasilisha andiko la kisheria kwa Tume ya
Uchaguzi (NEC) ambalo litakuwa na malalamiko kuhusu matukio na hujuma
zinazoendelea katika kipindi hiki cha kampeni.



Post a Comment