Makanisa matatu ya dhehebu la Kipentekoste yaliyopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, yameteketezwa kwa moto usiku wa kuamkia leo na watu wasiofahamika.
Tukio
hilo limehusisha makanisa ya Pentecostal Assemblies of God (PAG)
lililopo Buyekera Kata ya Bakoba, Living Water International na
Evangelical Assemblies of God (EAGT) yote yakiwa eneo la Kashura.
Akizungumzia
tukio hilo Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Athanas, amesema saa 10
alfajiri alipigiwa simu na jirani yake na kuelezwa kanisa linaungua moto
na kumfanya kukimbia kwenda eneo la tukio.
Mchungaji
Athanas amesema baada ya kufika eneo la tukio alikuta moto mkubwa ambao
usingeweza kuzimwa kwa kumwagia maji, hali iliyosababisha vitu vyote
vilivyokuwa ndani ya kanisa hilo kuteketea ikiwa pamoja na viti 60,
meza, mabenchi, vifaa vya ujenzi na madhabahu.
Amesema
hawajafahamu watu waliohusika na tukio hilo, lakini alidai waliponusa
baadhi ya vitu walisikia harufu ya mafuta ya taa hali iliyopelekea
wahisi wachomaji walitumia mafuta ya taa kuteketeza kanisa hilo.
Mchungaji
huyo alisema hilo ni tukio la tatu la makanisa ya EAGT kuchomwa moto,
wakati mara ya kwanza ilikuwa Septemba 2013 na kufuatia lile la Aprili
mwaka jana.
Naye
Mchungaji Alistides Kabonaki wa kanisa la Pentekoste P.A.G, alisema saa
11.50 asubuhi jana, aliitwa na msichana wake wa kazi na kumweleza kuna
moto unawaka kanisani.
Kabonaki
alisema kanisa lote limeteketea pamoja na mali zilizokuwamo ndani huku
waliohusika na tukio hilo akiwa hawafahamu walikuwa na lengo gani.
Amesema
alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa pamoja na polisi, hivyo kwa sasa
anasubiri hatua za kiuchunguzi za jeshi hilo ili kubaini waliohusika na
sababu za kufanya hivyo.
Mchungaji
huyo alisema kabla ya uchomaji wa kanisa hilo, watu hao wasiofahamika
walivamia kanisa lao na kuiba baadhi ya mali zilizokuwamo ikiwamo viti
na vitambaa vya madhabahu.
Akizungumzia
tukio hilo, Regina Bakera, ambaye ni jirani na kanisa la PAG, alisema
kama muumini amesikitishwa na matukio hayo na hawafahamu waliosababisha
hilo.
Bakera
alisema matukio hayo yanadhihirisha kuna kikundi kilichoandaliwa kwa
ajili ya kuchoma makanisa na kuiomba serikali kuyashughulikia kufanya
upelelezi wa kina.
Kufuatia
uchomaji wa makanisa hayo, umoja wa wachungaji katika mkoa wa Kagera,
umepanga kufanya maandamano ya kulaani kitendo hicho mkoa mzima maana
serikali ilishindwa kutatua matatizo yanayowakabili ikiwamo la makanisa
yao kuchomwa moto.
Mwenyekiti
wa Makanisa hayo mkoa wa Kagera, Crodward Edward, alisema kwa sasa
wanachukua hatua ya kujilinda kwa sababu serikali ilishindwa kufanya
hivyo pamoja na vikao ambavyo wamekaa viongozi wa serikali na viongozi
wa makanisa hayo.
Akizungumzia
matukio hayo amesema siku za nyuma yalichomwa makanisa saba katika mkoa
wa Kagera huku moja likihusisha pia mauaji ya muumini mmoja na
waliokamatwa wakiachiwa huru bila kuelezwa kinachoendelea na sasa
yamechomwa matatu kwa siku moja.
Naye
Mchungaji Aneth Sebastian ambaye ni Katibu wa wachungaji katika
manispaa ya Bukoba alisema sasa wanashindwa kuiamini serikali na polisi
kwa sababu watakuwa wanawafahamu wanaohusika na vitendo hivyo bali
wanawakingia kifua.
Tathmini
ya hasara iliyotokana na uchomaji wa makanisa hayo ambayo mawili
yameteketea kabisa bado inaendelea, ili kujua hasara iliyotokana na
uchomaji moto huo.
Akizungumza
kwa njia ya simu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi,
alisema kwa sasa yuko safarini na atatoa ufafanuzi kuhusiana na tukio
hilo baadae.
Post a Comment