Wizara imesikitishwa na taarifa za uongo zilizotolewa katika vyombo vya habari kuwa Mhe. Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uongozi wake wa miaka 10 ametumia Shilingi trilioni 4 kwa ajili ya safari za kikazi nje ya nchi, ambazo ni wastani wa bajeti nzima ya wizara kwa miaka mitano (5).
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kutoa ufafanuzi
kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, kiasi kikubwa kabisa cha bajeti
kuwahi kutengwa kwa ajili ya safari za Viongozi Wakuu yaani Rais, Makamu
wa Rais na Waziri Mkuu ni shilingi bilioni 50 ambazo zilitengwa kwa
Mwaka wa Fedha 2014/2015 kwa ajili ya Idara ya Itifaki. Kwa miaka
mingine yote wastani umekuwa ni kati ya shilingi bilioni tano hadi 25
kulingana na mahitaji ya idara hiyo.
Ifahamike
kuwa kiasi hicho cha shilingi bilioni 50 ni bajeti nzima ya Idara ya
Itifaki, ambapo kuna fungu maalum kwa ajili ya ziara za viongozi. Fungu
hilo linagharamia makundi makuu matano kama ifuatavyo:
1.Kundi la Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
2.Kundi la Makamu wa Rais wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
3.Kundi la Waziri Mkuu wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
4.Kundi la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nje ya nchi wanapotembelea Tanzania; na
5.Kundi la Wajumbe Maalum wanaokuja nchini kuleta taarifa muhimu kwa Rais.
Makundi
yote haya hugaramiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ndani
ya bajeti ya Idara ya Itifaki kifungu cha Ziara za Viongozi.
Aidha
uandaaji wa bajeti ya Wizara chini ya Idara ya Sera na Mipango
unahusisha wadau wengine nje ya Wizara kama vile Kamati ya Bunge ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa na hupitishwa kila mwaka na Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Tunapenda
kuwaatahadharisha wananchi juu ya watu wanaotoa taarifa za uongo kwa
madhumuni ya kujenga chuki dhidi ya Serikali. Ikumbukwe kuwa ziara za
viongozi zinazoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje zina mafanikio makubwa
kwa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Wizara
inaandaa taarifa ndefu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara,
changamoto na mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka kumi
ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambayo itatolewa kwa umma kwa
lengo la kutoa elimu zaidi.
MWISHO.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
17 Septemba 2015
Post a Comment