Na Waandishi Wetu
NI
kweli, ukweli ni huu! Wakati maelfu ya watu nchini wakiamini
kutoonekana hadharani kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa kunatokana na kuchukizwa na
kitendo cha kukaribishwa kwa waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na
kupewa fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho, ukweli wa jambo hilo
umeibuliwa, Uwazi linakupa zaidi.
Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, aliyeomba hifadhi ya
jina lake, ameliambia gazeti hili kuwa, madai yanayotolewa na watu
mitaani na katika mitandao ya kijamii yakisema Dk. Slaa amekasirishwa na
kitendo hicho ni ya uongo.
ALIANZA DK. SLAA, MBOWE MH!
Mjumbe huyo alisema kuwa, Dk. Slaa ndiye mtu wa kwanza ndani ya Chadema
kutoa wazo na hatimaye kushiriki kikamilifu katika vikao vya kumwezesha
Lowassa kujiunga na chama hicho.
“Kwa taarifa yako, Dk. Slaa ndiye aliyemtaka Lowassa ajiunge Chadema.
Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa Taifa Chadema) hakumtaka kabisa huyu jamaa
aje kwetu. Kwa sababu hakuona jinsi gani wangewaeleza wananchi juu
yake, lakini mzee ndiye aliyeshawishi na vikao vya kumjadili vikaanza
mfululizo. Ukiangalia picha za awali, Dk. Slaa yupo.”
MTOA HABARI ASHIRIKI VIKAO
“Mimi ninayekwambia ni Mjumbe wa Kamati Kuu, nimeshiriki zaidi ya vikao
14 vilivyokuwa vikimjadili Lowassa na vyote hivyo, Dk. Slaa alikuwepo.
Huyu jamaa hajakaribishwa kwa utashi wa mtu mmoja kama mnavyosikia huko
nje na wala mzee Mtei (Edwin, mwasisi wa chama hicho) hahusiki na
chochote,” alisema mjumbe huyo.
WABUNGE WAKOROFI WALIAFIKI
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, ili kuondoa dhana kuwa, Lowassa anapelekwa
Chadema na uongozi, wabunge wote ‘wakorofi’ ndani ya chama hicho
walikaribishwa kushiriki vikao 14 vya kumjadili ili pia wamuulize
maswali na yapate majibu kitu ambacho kilifanyika kwa ufanisi wa hali ya
juu.
Aliwataja baadhi ya wabunge hao ‘wakorofi’ na majimbo yao kwenye mabano
kuwa ni pamoja na Godbless Lema (Arusha Mjini), John Mnyika (Ubungo),
Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Halima
Mdee (Kawe), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Joshua Nassari (Arumeru),
Ezekiel Wenje (Nyamagana), David Silinde (Mbozi Magharibi) na Highness
Kiwia (Ilemela).
“Unajua, kwa vyovyote vile, vikao kama vingefanywa na viongozi wa juu
peke yao, hawa wabunge wakorofi wangesumbua sana, lakini wote
walishiriki na hakuna ambacho hawakijui. Ndiyo maana wote wamekaa kimya
kwa sababu taratibu zote zilifuatwa,” alisema mjumbe huyo.
UKWELI ULIVYO
“Hapa lazima nikueleze ukweli. Kinachotokea kwa Dk. Slaa ni shinikizo
kutoka familia yake. Kuna watu walikuwa na matumaini makubwa ya
kufaidika endapo yeye angegombea tena na kushinda urais mwaka huu, hivyo
wameamua kununa kwa sababu kilichotokea hakina masilahi kwa familia.
YADAIWA DK. SLAA ALITAKIWA KUCHAGUA MOJA
Mjumbe huyo alikwenda mbali kwa kusema kuwa, wakati wa mchakato wa Dk.
Slaa kutaka Lowassa aingie Chadema baada ya kukatwa jina na Kamati Kuu
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma, hakuiambia familia yake mpaka
dakika za mwisho, ikajulikana.
“Ndipo familia ikamweka chini na kumwambia achague moja. Aendelee na
siasa za Chadema au aachane na siasa hizo ili aangalie familia yake
kwani kitendo chake cha kuwa mstari wa mbele kumtaka Lowassa kiliashiria
kuwa, yeye hatagombea tena urais hivyo kuua matumaini ya familia. Ndiyo
maana yupo kimya na hafiki ofisini.”
CHADEMA YAPANGA SAFU YA KUMSHAWISHI
“Sasa dokta ni mtu mzima. Hawezi kuliamua hilo kirahisi kama
unavyofikiria. Ni lazima aende nalo taratibu ili kuziridhisha pande zote
mbili. Na kwa kutambua hilo, chama kimeunda jopo la watu, wakiwemo
mapadri, mashehe na marafiki zake ili wamshawishi arejee Chadema lakini
akiiweka familia yake katika kuridhia na kumwelewa,” alisema mjumbe huyo
wa Kamati Kuu.
LOWASSA AANIKA UKWELI KUHUSU RICHMOND
Kuhusu madai ya muda mrefu ya chama hicho yanayomtaja Lowassa kuwa ni
fisadi, mjumbe huyo alisema kiongozi huyo aliwaeleza kwa ufasaha kuhusu
utajiri wake na wakaridhika. Kwa upande wa Richmond, aliwaeleza kuwa
alishataka kuuvunja mkataba huo, lakini mamlaka ya juu ikamzuia.
TAASISI TOKA NJE YATUA NCHINI KUTAFITI
Juu ya nafasi yao kushinda urais wakiwa na Lowassa, mjumbe huyo alisema
kabla ya kuafiki kumtangaza kugombea, kwa gharama za Chadema, walikodi
taasisi ya utafiti kutoka nchini Ujerumani kuja Tanzania ili kufanya
utafiti nchi nzima kama Lowassa anakubalika.
Alisema utafiti ulipokamilika, ikaonesha kuwa, kama uchaguzi mkuu
ungefanyika Julai 2015, Lowassa alikuwa mbele ya wagombea wenzake kwa
asilimia 65.
SLAA KIMYAAA!
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, Dk. Slaa hajajitokeza kuelezea
kilichosababisha ukimya wake huku akiwa hapokei simu ya Uwazi kitu
kinachozidisha kwa kasi maneno mitandaoni juu ya hatima yake ndani ya
chama hicho kikuu cha upinzani.
Alhamisi iliyopita gazeti dada na hili, Uwazi Mizengwe linalotoka kila
Ijumaa, waandishi wake walishinda nyumbani kwa Dk. Slaa, Mbweni nje
kidogo ya Jiji la Dar lakini walishindwa kuongea naye licha ya
kumpelekea karatasi yenye ujumbe wa kumuomba kuzungumza naye,
waliambulia kumuona kwa mbali akiwa ndani ya geti la nyumba yake.
Post a Comment