Tumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa baraka na rehema zake kwa kutufikisha hapa hii leo
tukiwa na afya njema. Katika kipindi hiki cha kampeni tumewapoteza, kwa
masikitiko makubwa, ndugu zetu kadhaa ambao walikuwa wagombea Ubunge na
udiwani na wengine waliyokuwa wakishiriki katika mchakato huu wa
uchaguzi kwa namna mbalimbali.
Tunamuomba
Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Mzee
wetu Dk. Emmanuel Makaidi, mawaziri Mama Celina Kombani na Dk. Abdallah
Kigoda, vijana wetu Mohamed Mtoi na Deo Filikunjombe, Mchungaji
Christopher Mtikila na Estom Mallah ambao wote walikuwa wagombea ubunge.
Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahala pema peponi. Amen.
Katika
kipindi cha kampeni nimefika katika kila kona ya nchi yetu, ninatoa
shukrani za dhati kwa mapokezi makubwa, mapenzi na ukarimu wa Watanzania
kwangu, kwa msafara wangu na mgombea mwenza, Mheshimiwa Juma Haji Duni.
Aidha
natoa shukrani zangu za pekee kwa wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman
Mbowe, James Mbatia, Twaha Taslima na marehemu Dk. Emmanuel Makaidi kwa
mchango wao mkubwa katika kuchochea mabadiliko na msaada wao kwangu
wakati wa kampeni.
Pia
namshukuru kwa dhati mzee wetu, Kingunge Ngombale Mwiru, Waziri mkuu
mstaafu Frederick Sumaye, viongozi mbali mbali wa CHADEMA na UKAWA ambao
kwa pamoja walijitoa kwa moyo wao wote kungoza harakati hizi za
mabadiliko. Ahsanteni sana
Kwa
namna ya pekee, pia nimshukuru mke wangu mpenzi, Regina Lowassa kwa
upendo, msaada na mchango wake katika kuhamasisha Watanzania na hususan
wanawake wakati wote wa kampeni. Ahsante sana Regina.
Ndugu Watanzania wenzangu
Katika
ziara hizi, nimeshuhudia vuguvugu la mabadiliko, kiu na ari ya
Watanzania kuyapokea mabadiliko hayo. Lakini pia nimejionea shida
zinazowakabili wananchi hao.
Nimesikia
na nyakati nyingine kujionea kilio chao cha kunyanyaswa na kunyimwa
haki zao na watendaji wa serikali na baadhi ya vyombo vya dola.
Nimekisikia
kilio chao cha umaskini, afya na elimu duni. Nimekisikia kilio kikubwa
cha vijana kukosa ajira na matarajio ya kesho bora.
Nimesikia rai za Watanzania na ndoto zao za kupata maendeleo, maji safi, makazi bora na barabara madhubuti.
Nimesikia
malalamiko ya wakulima na wafugaji kukosa maji na ardhi. Nimesikia
kilio cha madaktari, wauguzi, walimu, askari na watumishi wa taasisi za
umma kuhusu mazingira magumu ya kazi, kodi za juu na maslahi duni.
Nimesikia
kilio cha wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu ugumu wa mazingira ya
kufanyia shughuli zao, kodi kandamizi na kukosa mitaji.
Nimesikia
kilio cha wanawake kuhusu haki zao na ushiriki wao mdogo katika
shughuli za kiuchumi. Nimesikia kilio cha wazee na wastaafu wasio na
bima ya afya, wanaolipwa pensheni isiyokidhi mahitaji yao na ugumu wa
maisha yao uzeeni.
Nimesikia
kilio cha Watanzania dhidi ya rushwa iliyokithiri na utawala dhaifu
ulioshindwa kuondoa umaskini au kutetea haki za raia.
Jibu langu ni fupi. Nimeona, nimesikia, nimeelewa na nitatenda.
Uchaguzi
wa mwisho wa wiki hii ndiyo utakaotupa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Rais mpya wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.
Ni uchaguzi muhimu na wa kihistoria kwetu sote.
Nawaomba
nyote mliyojiandikisha mjitokeze kwa wingi kutimiza haki na wajibu wenu
wa Kikatiba. Sehemu muhimu ya mabadiliko tunayodhamiria kuyaleta ni
kujitokeza kupiga kura.
1.
Ipo dhana potofu inayojengwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwamba
wafuasi na wanachama wa vyama vyetu vinavyo unganishwa na UKAWA wataleta
fujo wakati wa kupiga kura. Ni maneno ya kipuuzi.
• Hata hivyo nawaomba nyote muwe wastaarabu, muheshimu sheria zilizopo. Tukusanyike na kupiga kura kwa amani na utulivu.
•
Katika kampeni zetu nchini kote hadi hivi sasa tumedhihirisha kwamba
vyama vyetu vya upinzani na wanachama wake hatuvunji, hatujavunja na
hatutavunja sheria.
• Hatuna sababu ya kufanya hivyo. Nia na dhamira yetu ni kushinda Uchaguzi huu na kuing’oa CCM madarakani.
2.
Dhana na fikra zingine potofu zinazojengwa na uongozi wa CCM kwa nia ya
kuwaogopesha Watanzania ni kwamba eti Watanzania wakichagua upinzani
nchi itaingia kwenye machafuko. Wapuuzwe wenye fikra hizi wameshasahau hata historia ya hivi karibuni ya nchi tunazopakana nazo.
•
Wote ni mashahidi kwamba chama cha UNIP cha Zambia kilipoondolewa
madarakani kwa kura za ndugu zetu wa Zambia, hapakutokea fujo zozote
Zambia. Ukweli ni kwamba Mzee wetu mpendwa Mzee Keneth Kaunda aliyekuwa
anaongoza chama tawala wakati huo yuko Zambia na anaendelea kufurahia
maisha yake wakati Wazambia wakipiga hatua katika maendeleo ya Taifa
lao.
•
Chama cha Malawi Congress Party pia kiling’olewa madarakani kwa kura za
ndugu zetu wa Malawi. Malawi kwa miaka yote imeendelea kuwa tulivu.
•
Chama cha KANU Kenya pia kiliondolewa madarakani mwaka 2002. Ukweli ni
kwamba matatizo yaliyojitokeza Kenya miaka mitano baadaye hayakutokana
na kuondolewa kwa KANU. Yalikuwa ni madai yaliyotokana na taarifa za
kuwepo kwa udanganyifu katika matokeo ya uchaguzi mkuu. La kujifunza
hapa ni kwamba udanganyifu uliwaletea wenzetu wa Kenya matatizo. Ni
lazima watanzania tuepuke udanganyifu wa aina hiyo.
•
Wako hata wanaotuogopesha sisi Watanzania kwa kutulinganisha na
Walibya. Hawa wapuuzwe na waonewe tu huruma kwa kuwa wamesahau misingi
na uimara wa nguzo za Taifa letu ambazo uongozi wa Baba wa Taifa Mwal.
Julius Kambarage Nyerere aliotujengea. Kwanza hawajui hata kwa nini
Libya wanapigana. Ukweli ni kwamba machafuko yao hayakutokana na
uchaguzi. Yalisababishwa na watawala kung’ang”ania madaraka na kugawana
rasilimali za taifa kwa misingi ya familia zao.
•
Kama ilivyotokea Zambia, Malawi na Kenya, Watanzania wamedhamiria
kuleta mabadiliko kidemokrasia na kuiondoa CCM madarakani kwa kura zao.
Ndugu zangu,
CCM
imekuwa madarakani kwa miaka mingi mno – zaidi ya nusu karne. Haina
jipya; imechoka na haina pumzi ya kuongoza Taifa letu tena. CCM imebaki
kuonyesha jeuri na kubeza tu. Imeishiwa nguvu ya hoja.
• Watanzania wamechoshwa na ahadi hewa za CCM za miaka nenda, miaka rudi. Tusiruhusu CCM kuendelea kurubuni na kuhadaa wananchi.
• Watanzania sasa wanataka MABADILIKO; mabadiliko ya kweli na ya uhakika.
• Tarehe 25 mwezi huu tuhakikishe tunaing’oa CCM madarakani na kuanza safari mpya ya kuleta mabadiliko.
•
Nini maana ya haya mabadiliko endapo mtanipa ridhaa yenu ya kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Yapo maeneo manne ya msingi katika
mabadiliko tunayodhamiria kuyaleta katika kuliongoza Taifa letu katika
zama mpya:
1. Kwanza kabisa, ni ukombozi mpya wa Mtanzania. Hakuna maendeleo bila uhuru na haki.
•
Mtanzania hana budi kuwa na madaraka ya Kikatiba juu ya maisha yake na
kuweza kujisikia ana haki kamili na yuko huru katika nchi yake.
•
CCM ilikwamisha ukombozi huu baada ya kuikataa Rasimu ya Katiba
iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba. Tusisahau kwamba hii Rasimu
imetokana na juhudi za wengi na Jaji Warioba akiwa tu ni mmoja wao.
• Nikichaguliwa kuwa Rais, suala hili la Katiba mpya yenye maslahi kwa mwananchi litapewa kipaumbele.
2.
Pili, ni ukombozi katika hali za maisha ya mwananchi. Wananchi hawawezi
kuboresha hali za maisha yao kupitia takwimu nzuri za Pato la Taifa
zinazopambwa na CCM ambazo hazionyeshi maisha halisi ya Mtanzania.
•
Watu hawali takwimu. Watanzania wanataka milo mitatu yenye lishe bora;
wanataka huduma bora za elimu, afya, maji safi na salama; wanataka umeme
vijijini na ajira toshelezi kwa vijana;
• Wanataka mapinduzi katika kilimo chenye tija na bei bora za mazao.
• Watanzania wamechoka na umaskini.
•
Haishangazi kusoma katika taarifa ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015
kuhusu hali ya furaha ya wananchi katika nchi mbali mbali katika mwaka
2013, kwamba kati ya nchi 156 zilizofanyiwa utafiti, Tanzania inashika
nafasi ya chini kabisa ya 151 ikidhihirisha kwamba watanzania hawana
furaha kabisa.
• CCM na Serikali yake imeshindwa kuwapa wananchi wake hali bora ya maisha na hivyo kuwanyima furaha.
•
Mwanasiasa maarufu wa Marekani Marehemu Seneta Hubert Humfrey aliwahi
kusema kwamba kipimo maalum cha maadili na dhamira ya Serikali yeyote na
hata haki ya Serikali hiyo ya kutawala ni jinsi inavyowajali na
kuhudumia watu wafuatao:
• Wale wanaoingia duniani kwa mara ya kwanza – yaani watoto;
• Wale ambao wanafikia mwisho wa maisha yao baada wa kutumikia jamii – wazee; na,
• Wale waliomo kwenye hali na mazingira ya maisha hatarishi –Hawa ni wagonjwa, wenye mahitaji maalum, na walemavu
• Kwa vipimo hivi vitatu, Serikali ya CCM imeshindwa vibaya sana. Imefilisika!
•
Baada ya zaidi ya miaka 50 ya Uhuru tunashuhudia wakina mama wengi
wanaotuzalia watoto wa taifa hili na vichanga vyao vikizaliwa sio kwenye
kitanda kilichotayarishwa bali sakafuni;
•
Tanzania katika mwaka wa 2015 inashika nafasi ya 91 kati ya nchi 96
zilizofanyiwa utafiti na Taasisi ya Dunia iitwayo HelpAge kuhusu hali ya
wazee wenye umri zaidi ya miaka 60. CCM na Serikali yake imeshindwa
kutekeleza wajibu wake. CCM haiwajali wazee wetu.
•
Wagonjwa hawapati dawa hospitalini nahata wanaojiweza lazma wakatibiwe
nje ya nchi; wenye mahitaji maalumu ya kibinadamu na ambao hawana njia
ya ajira hawayapati; huduma za walemavu ni finyu na, pamoja kuendelea
kwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
3.
Tatu, wananchi wanataka mabadiliko ya uongozi na mfumo; wanataka
uongozi wenye fikra mpya, utendaji wa kuaminika; na uongozi wa
uwajibikaji na uongozi shirikishi.
•
Wanataka uongozi makini wenye ubunifu, wenye upeo mpana na unaongozwa
na nidhamu na hasa ile ya matumizi mazuri ya fedha za Serikali.
•
Serikali ya CCM imeingiza nchi katika deni kubwa katika historia ya
nchi. Deni hili ni karibu shilingi trillioni 35 hivi sasa. Deni hili
limetokana na matumizi mabaya ya Serikali ya CCM ya Rais Kikwete.
•
Ni kazi kubwa kulipa deni hili. Na ndiyo maana Watanzania wanalazimika
kuing’oa Serikali ya CCM na kuleta mabadiliko ya kiuchumi yatakayo
wapunguzia kizazi hiki na kijacho mzigo wa madeni ambayo Serikali ya CCM
inaendelea kuwalimbikizia kutokana na matumizi yasiyo na busara
•
Nataka kuwahakikishia kwamba uongozi wangu na ule wa mwenzangu visiwani
Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, si wa kuyumba au kuyumbishwa; ni
uongozi wa kuthubutu katika utatuzi wa matatizo ya wananchi; ni uongozi
wa uchapa kazi na wa kuchukua maamuzi magumu kwa manufaa ya kizazi
kilichopo na kizazi kijacho.
• Ni uongozi wenye dhamira ya kuwaunganisha watanzania bila kujali madhehebu, rangi au makabila yao.
• Ni uongozi utakaojenga Taifa linalojitegemea, siyo la omba omba kama ilivyo hivi sasa.
4. Nne, Uongozi wangu na wa wenzangu utaheshimu, utalinda na kutetea Katiba ya nchi.
Nitakuwa mfano wa uadilifu; nitapiga vita vitendo vyote vya rushwa na
ufisadi; Nitahakikisha kwamba rushwa hakika inakuwa adui wa haki na
maendeleo yetu.
Ndugu watanzania wenzangu,
Baada
ya kufafanua maeneo haya manne ya msingi kuhusu mabadiliko nitakayo
yaleta na kuyasimamia, sasa naomba niingie kwa undani kuhusu mambo
ambayo Serikali nitakayounda itatekeleza ni mambo 16.
1. Kwanza, Serikali nitakayoongoza itapambana na umaskini, ujinga na maradhi kikamilifu.
•
Itaboresha elimu kama hatua ya kwanza ya kuwapa Watanzania uwezo wa
kujikomboa. Kila Mtanzania atapata elimu bora itakayogharimiwa na
serikali kutoka ngazi ya elimu ya awali hadi Chuo Kikuu.
•
Tutapiga marufuku michango kama vile ya kujenga maabara na tutaboresha
maslahi na vitendea kazi kwa waalimu na kurudisha posho ya kufundishia.
•
Tutapanua wigo wa mafunzo ya kijeshi na kujitegemea yanayotolewa katika
Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuongeza idadi ya wanaojiunga mara tano
zaidi kuliko ilivyo sasa ili kuboresha mafunzo ya stadi za maisha,
ufundi na ujasiriamali.
2. Pili,
tutaondoa kodi zote za kero kwa wafanya biashara hususani wafanya
biashara wadogo wadogo, mama lishe, boda boda, na machinga.
•
Aidha, tutaondoa kodi zote za mazao kwa wakulima, wafugaji, na wavuvi
wadogo wadogo ili tuongeze kipato na uwezo wao wa kuwekeza na
kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula na lishe bora.
•
Tutahakikisha kuwa elimu inatolewa kwa makundi haya ili kuinua kiwango
cha uzalishaji kwa kusimamia shughuli zao kitaalam kwa kutumia
teknolojia ya kisasa.
•
Vile vile, tutayawezesha makundi haya kwa mikopo ya riba nafuu kutokana
na benki mahsusi itakayoanzishwa kusimamia sekta ya ufugaji na uvuvi.
3. Tatu,
tutakuza na kulinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa
Watanzania upendeleo wa maksudi ili waimarike na waweze kuhimili
ushindani.
• Tutawapa upendeleo katika zabuni na manunuzi ya serikali na kuwajengea mazingira mazuri zaidi ya biashara.
•
Serikali nitakayoongoza itajenga uhusiano wa karibu na wawekezaji
katika biashara na viwanda katika kuhakikisha sera na mikakati ya
Serikali haipingani na mazingira ya uzalishaji na mienendo ya biashara.
•
Tanzania ina kodi nyingi kuliko nchi zote Afrika ya Mashariki na zile
za SADC. Tutaweka mfumo wa kodi utakaotuwezesha kushindana kimataifa.
• Kazi hii ni nzito kwa sababu Serikali ya CCM imeacha dosari kubwa katika mazingira yanayovutia uwekezaji.
•
Ukweli ni kwamba Tanzania imepoteza uwezo wa ushindani katika soko la
ndani na la nje kutokana na ubovu wa miundombinu pamoja na urasimu hali
ambayo imesababisha gharama za usafiri na usafirishaji kuwa kubwa kupita
kiasi.
•
Taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2015 ambayo hupima ubora wa
miundombinu ya usafiri kwa madhumuni ya biashara inaonyesha kwamba kati
ya nchi 160 zilizofanyiwa utafiti, Tanzania imeshika nafasi ya chini ya
138.
•
Hata nchi zinazopitisha bidhaa zao Tanzania (landlocked) kama vile
Malawi, Rwanda na Burundi zimeshika nafasi za 73, 80 na 107. Kenya
inashika nafasi ya 74.
4.
Nne, tutakuza viwanda vidogo vidogo ili viwe mhimili wa uchumi wa nchi.
Lazima tuimarishe uzalishaji na kusindika mazao yetu ili kuongezea
thamani na kutengeneza vyanzo vya ajira.
5. Tano, tutaimarisha mfumo wa afya ya msingi na kuboresha huduma za kinga ili kuepukana na gharama kubwa za tiba.
•
Serikali nitakayoongoza itaandaa taratibu na mifumo ya kuwapatia
wananchi wote huduma za afya na matibabu kupitia bima za gharama nafuu
na mifuko ya hifadhi ya jamii.
•
Tutaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa
ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na kuepukana na gharama
kubwa za tiba za nje ya nchi.
•
Wazee na wananchi wasiojiweza watapewa posho ya kujikimu inayokidhi
mahitaji ya msingi ili waishi kwa heshima ndani ya familia na jamii zao.
6. Sita, tutadhibiti matumizi serikalini
na katika mashirika ya umma kama vile kupiga marufuku matumizi ya
magari ya anasa, kupunguza safari za ndani na nje,usafiri wa anga wa
daraja la kwanza na semina na makongamano yasiyo ya lazima.
7. Watanzania watapewa fursa maalum ya kushiriki katika uwekezaji katika
sekta ya mafuta na gesi. Sambamba nahili, Serikali yangu itaanzisha
Wizara maalum itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta.
8. Nane tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika au makampuni yote ambamo serikali ina hisa na kuipa ofisi hiyo mamalaka kamili.
• Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu.
9. Tisa, tutadhibiti vitendo vya rushwa iliyo kithiri katika bandari zetu, ukwepaji
kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela
ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki.
•
Sambamba na hayo, tutarahisisha utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa
kero na mazingira ya rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi tutaweza
kupata fedha zaidi za kugharimia huduma za msingi kikamilifu.
10. Kumi, tutaimarisha utendaji na uwajibikaji katika sekta ya umma na kuhakikisha kuwa rushwa, urasimu na kero zinazodumaza maendeleo ya wananchi zinakomeshwa.
• Sambamba na hayo, tutaboresha maslahi na vitendea kazi kwa wafanyakazi wa Serikali na sekta ya umma.
11. Kumi na moja, tutahakikisha tunatengeneza vyanzo vipya vya ajira kwa kukuza sekta za kilimo, viwanda na utalii.
12. Kumi na mbili, tutaimarisha miundombinu na kujenga mtandao wa reli tukianza kwa kujenga upya na kwa viwango vya kisasa Reli ya Kati na Reli ya Tanga-Arusha-Musoma.
• Pia tutajenga barabara za viwango vya juu kuliko sasa zikiwemo za vijijini ili kuchochea biashara na maendeleo.
•
Tutaboresha bandari za baharini na maziwani na kujenga zingine mpya
kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa
bandari za nchi jirani. Tutanunua meli mpya za usafiri wa watu na mizigo
kwa ajili ya usafiri katika ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
• Tutajenga upya Shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida.
•
Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha misongamano ya magari hasa
katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha
•
Tutasimamia uzalishaji na usambazaji wa umeme mijini, vijijini ili
kufikia zaidi ya asilimia sabini na tano ya Watanzania ifikapo mwaka
2020.
• Tutasimamia upanuzi na usambazaji wa umeme wa uhakika na kufanya mgao wa umeme kuwa historia hapa nchini.
13. Kumi na tatu, tutahakikisha Katiba ya wananchi inakuwepo ili kujenga misingi ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na kuwapa nafasi asasi za kiraia, vyombo vya dola, Bunge na wananchi kusimamia uwajibikaji nchini.
•
Tutasimamia utawala bora kwa kuamini kuwa kama nchi itaendeshwa kwa
misingi ya sheria na utawala bora, haki itatendeka, rushwa itadhibitiwa,
barabara bora zitajengwa kwa viwango, shule na hospitali bora
zitajengwa na kupewa vifaa na kwamba mashirika yetu yataendeshwa kwa
tija.
14. Kumi na nne, tutaimarisha mchango wa wataalam wetu, wanawake na vijana, katika kuandaa sera na kusimamia uchumi na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja na mafao.
•
Serikali nitakayoongoza itaunda Tume Maalum ya Kupendekeza mishahara ya
watumishi Serikalini, sekta ya umma na binafsi kwa maana ya kima cha
chini cha mshahara.
15. Kumi na tano, tutaimarisha Muungano wetu ikiwa ni pamoja na umoja, usalama na udugu wa Watanzania kwa misingi ya haki na usawa.
16. Kumi na sita, tutaimarisha uhusiano na kuongoza ushirikiano
na nchi nyingine ndani ya Jumuia ya Afrika ya Mashariki, SADC, Umoja wa
Afrika, Umoja wa Mataifa na Taasisi nyingine za Kimataifa.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Napenda
kusisitiza kwamba ili haya yote tunayokusudia yaweze kufanikiwa, ni
lazma tuimarishe mihimili ya Taifa letu na vyombo vyake maalum.
Serikali
ina wafanyakazi wengi mahiri, wadilifu na wenye weledi mkubwa. Ili
kuhakikisha ufanisi mzuri wa Serikali na taasisi zake, mishahara ya
wafanya kazi wa Serikali itaboreshwa, ushauri wao wa kitalaamu utawekwa
maanani na vitendeakazi vyao vitatiliwa mkwazo;
Ulinzi
wa taifa utaimarishwa kwa kuzingatia mahitaji na maslahi askari wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na Magereza ikiwa ni pamoja
na kuboresha vitendea kazi vyao.
Maboresho
hayo yatahusisha pia taasisi zote zenye dhamana ya masuala ya ulinzi na
usalama wa nchi, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(PCCB).
Katiba tutayoipitisha itakuwa ni ya kuimarisha Mhakama kwa kiasi kikubwa pamoja na Bunge letu
Serikali yetu itahakikisha suala la michezo, utamaduni na sanaa linapewa kipaumbele maalum.
Pamoja
na kwamba Tanzania kwa sasa inazidi kung”aa kupitia wasanii wa muziki
wa kizazi kipya, lakini bado juhudi kubwa haijawekwa katika kukuza na
kuendeleza sanaa, utamaduni na michezo.
Timu zetu za mpira bado hazifanyi vizuri kimataifa na zimeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu.
Kuodokana na hali hiyo, Serikali yetu itafuta kodi zote za vifaa vya michezo.
Itafuta kodi za sanaa kwa wasanii chipukizi.
Itajenga
shule za kukuza vipaji vya soka (Youth Academies) na michezo mingine
ili kuhakikisha ndani ya miaka mitano, Tanzania inashiriki kwa ushindi
katika mashindano ya kimataifa ya soka, riadha na michezo mingine.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo:
1.
Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua kuwa Rais wenu, nitaienzi
dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka na kwa uadilifu mkubwa.
2.
Mimi nawaheshimu Watanzania na namuogopa Mungu. Nawaahidi kwamba
nitawatumikia Watanzania kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote.
3. Mabadiliko yanaendana na kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua.
4. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM na ndiyo nyenzo yao kuwakandamiza Watanzania. Tukatae. Tuchague mabadiliko
5. Mabadiliko ni fikra. Ni mabadiliko ya kufikiri na kutenda tofauti na hali ilivyo.
6.
Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kana kwamba hatuna dharura ya
maendeleo. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila
kutegemea wafadhili.
7.
Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja.
Tujifunze kutoka kwao.Tanzania pia itaweza; tukichagua Mabadiliko.
8.
Tuwe taifa linalotumia rasilimali zake kwa ufanisi zaidi kujiendeleza
na siyo kwa kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika
nchi yao.
9. Tuache kuwa taifa ombaomba. Tuache kuukubali na kuuvaa umaskini kama vile ni joho la fahari. Hakuna faraja katika umaskini.
10.
Mabadiliko hayawezi kuletwa na CCM. Miaka zaidi ya hamsini ya utawala
wake watanzania bado ni maskini. Tusitegemee kuwa wanalo jipya hii leo.
11.
Kama alivyosema Baba wa Taifa “maendeleo ni watu”. Magorofa marefu
yanapendeza na tuendelee kuyajenga. Lakini maendeleo ya watu ndiyo
msingi.
12.
Kwa kuwa CCM imeshindwa kuwakomboa Watanzania kimaisha, basi imepoteza
haki na haina sifa ya kuendelea kutawala. Tuikatae CCM. Tuchague
mabadiliko.
13. Watanzania wameichoka CCM.
14. CCM imethibitisha pasipo na shaka kwamba ipo tu kwa maslahi ya wachache.
15. CHADEMA na UKAWA hatuna ajenda nyingine bali kuwahudumia Watanzania katika kuharakisha maendeleo yetu.
16. Mimi, CHADEMA na UKAWA tunaamani kwamba tutashinda uchaguzi kwa sababu Watanzania tupo pamoja katika kuleta mabadiliko.
17.
Hivyo basi, kura ya kila mmoja wetu inayonichagua mimi na mgombea
mwenza, Mheshimiwa Juma Haji Duni, mgombea urais Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad, wabunge, wawakilishi na madiwani ndiyo itakayokuwa
mkombozi wetu.
18. Tuhakikishe tunapiga na kulinda kura zetu. Wakati wa mabadiliko ni sasa.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Post a Comment