Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika uwanja wa michezo wa
Jamhuri mjini Dodoma na kuvikwa skafu tayari kuongoza maadhimisho ya
Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu2015 na kumbukumbu ya miaka
16 ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.Kauli mbiu ya mwaka huu ni “ Tumia haki yako ya kidemokrasia
kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Dodoma waliohudhuria sherehe za kilele cha maadhimisho yam bio za mwenge wa Uhuru.
Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika jukwaa malum akipigiwa wimbo wa
taifa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa michezo wa Jamhuri mjini
Dodoma kuongoza maadhimisho yam bio za mwenge.
(picha na Freddy Maro.
Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari,
Vijana, Michezo, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainabu Omar Mohamedi, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto – Zanzibar;
Mheshimiwa Chiku Gallawa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi;
Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa Kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar;
Makatibu Wakuu Kutoka Wizara Mbalimbli Tanzania
Bara na Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika
ya Kimataifa;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama Mbalimbali vya Siasa;
Viongozi Wetu wa Kiroho Kutoka Katika Madhehebu
Mbalimbali;
Vijana Wetu;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nawashukuru
Mawaziri wetu Mheshimiwa Fenella Mukangara wa Serikali ya Muungano na
Mheshimiwa Zainabu Omari Mohamed wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa kunialika kuja kushiriki katika sherehe za mwaka huu za kilele cha
Mbio za Mwenge wa Uhuru. Napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza na
kumshukuru Mheshimiwa Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na viongozi
wenzake na wananchi wote wa Dodoma kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe
hizi na kwa maandalizi mazuri. Tunawashukuru kwa mapokezi mazuri na
kwa ukarimu wenu mkubwa.
Pongezi kwa Wizara na Wananchi
Pia,
nawapongeza Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi waandamizi na maafisa wa
ngazi mbalimbali wa Wizara zetu hizi mbili husika kwa kazi kubwa na
nzuri waliyofanya ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu ya
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2015. Kwa namna ya kipekee pia napenda
kuwatambua, kuwashukuru na kuwapongeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi, Watendaji wa Halmashauri na viongozi wa Majimbo, Kata,
Shehiya, Vijiji na Mitaa kote nchini kwa kuziwezesha Mbio za Mwenge
mwaka huu kufanyika kwa usalama katika maeneo yao.
Nawapongeza
na kuwashukuru wananchi wote kwa jinsi walivyoupokea na kuukimbiza
Mwenge katika maeneo yao. Nafarijika kuona hamasa ya wananchi juu ya
Mwenge iko juu sana na kuwanyima wale wote wenye fikra hasi kuhusu
Mwenge. Mwaka huu, Mwenge umekagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi
kwa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 463.5. Haya ni baadhi tu
ya manufaa ya Mwenge wa Uhuru.
Pongezi kwa Wakimbiza Mwenge
Ndugu wananchi;
Nawapongeza
kwa namna ya pekee vijana wetu waliokimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa
chini ya uongozi mahiri na makini wa Ndugu Juma Khatibu Chum.
Nawapongeza kwa kazi kubwa na nzuri ya kukimbiza Mwenge kwa
siku 168 kupitia Mikoa yote, Wilaya zote, Vijiji vingi na mitaa mingi
kote nchini. Jukumu hili ni zito na lina changamoto nyingi. Linahitaji
watu wenye moyo wa uvumilivu, ustahamilivu na kuwa tayari kujitoa na
kulitumikia taifa. Kwa uzalendo wenu na mapenzi kwa nchi yenu hamkukata
tamaa na kuweza kumaliza mbio hizi na kuufikisha Mwenge mikononi mwangu
salama salmini. Napenda kuwahakikishia kuwa tumeona uongozi ndani yenu
na uzalendo mkubwa. Majina yenu yatabaki katika historia ya nchi yetu.
Nawashukuru
pia, kwa Risala yenu na kwa kunikabidhi Kitabu kikubwa chenye Risala za
Utii za wananchi wa Tanzania. Tutazisoma zote na tutayafanyia kazi
yale yenye kuhitaji hatua za kuchukua.
Umuhimu wa Mwenge katika Taifa letu
Ndugu Wananchi;
Umuhimu
wa Mwenge wa Uhuru katika Taifa letu ni jambo linalolopaswa kurudiwa
kuelezwa mara kwa mara bila kuchoka. Hatupaswi kubweteka maana kazi ya
ujenzi wa moyo wa uzalendo na mapenzi ya raia kwa taifa lao haina ukomo. Kama
nchi kubwa ambazo zimejitawala kwa zaidi ya karne moja zinaendelea na
kazi hiyo seuze sisi nchi yenye umri wa nusu karne?
Ndugu wananchi;
Mwenge
wa Uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza tarehe 9 Desemba, 1961 kwenye
kilele cha mlima Kilimanjaro kutimiza ahadi ya Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika kwamba: “Sisi
tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro, umulike
hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini,
upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”.
Baada
ya Uhuru ndipo utaratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ulipoanzishwa na
kuendelea hadi sasa. Kimsingi mbio hizo zimeendelea kueneza ujumbe wa
amani, umoja, mshikamano, utu na moyo wa uzalendo na kujitolea miongoni
mwa Watanzania. Mambo hayo yamekuwa Tunu zinazolitambulisha nchi
Tanzania na watu wake.
Ni
mambo yasiyokuwa na chama wala itikadi. Sote yanatuhusu, kutugusa na
kutunufaisha. Pamoja na kusema tunu hizo kila mwaka kumekuwepo na
ujumbe maalum unaoakisiwa katika kauli mbiu. Mwaka huu kwa mfano kauli
mbiu ni “tumia haki yako ya kidemokrasia na kupiga kura katika uchaguzi
wa mwaka huu 2015”. Mtakubaliana nami kuwa ni ujumbe muafaka. Aidha
katika Mbio za mwaka huu pia Mwenge hueneza ujumbe kuhusu mapambano
dhidi ya UKIMWI, malaria, dawa za kulevya na rushwa. Masuala hayo
yamekuwa yanazungumzwa kwa miaka kadhaa sasa kwa sababu ya umuhimu wake,
bado yapo na kwamba mapambano yanastahili kuendelea dhidi ya changamoto
hizo. Haya ni masuala ya kutafakari tunaposherehekea Mwenge wa Uhuru,
kutafakari maisha na wosia wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na kuamua juu ya mwelekeo na hatma ya nchi yetu
kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Ndugu Wananchi;
Kama
mjuavyo, katika siku ya leo, sambamba na sherehe za kumaliza Mbio za
Mwenge wa Uhuru, ni siku ya kumbukumbu ya maisha ya Baba yetu wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeaga dunia siku kama ya leo miaka
kumi na sita iliyopita. Hivyo leo ni siku ya kusherehekea maisha yake
na kujikumbusha mchango wake na urithi uliotuachia kama taifa na kama
Watanzania. Hayati Baba wa Taifa alikuwa ni mwalimu wetu. Katika maisha
yake ya uongozi hata baada ya uongozi ameendelea kuwa alama ya ushujaa,
umoja wetu, uadilifu na uongozi uliotukuka. Jambo linalotia faraja ni
kuwa, sote tunakubaliana kuwa Mwalimu Nyerere ndio kipimo cha uongozi
bora katika nchi yetu.
Bahati
nzuri, kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka huu
inaadhimishwa siku 10 tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge,
Wawakilishi na Madiwani nchini kwetu. Hivyo ni wakati muafaka sana
kutafakari kwa wosia wake kuhusu uongozi na uchaguzi katika nchi
yetu.
Baba
wa Taifa Mwalimu Nyerere ametuachia wosia muhimu kuhusu watu wanaofaa
kuchaguliwa kuongoza nchi yetu katika hotuba zake na maandishi yake
mbalimbali. Kimsingi alitutaka Watanzania tutambue kuwa hatima ya nchi
yetu inategemea aina ya viongozi tulionao. Alisisitiza umuhimu wa kuwa
na viongozi watakaojenga umoja wa taifa letu na uadilifu. Kwa ajili hiyo
alituusia kuchagua viongozi watakaodumisha Muungano wetu na kuwawezesha
Watanzania kuishi pamoja kidugu wakiwa na mshikamano na ushirikiano
licha ya tofauti zao za dini, rangi, kabila au mahali
watokako. Alisisitza sana uadilifu wa viongozi kwa ajili hiyo alituasa
bila kumung’unya maneno kuwaogopa kama ukoma watu wanaotaka kwenda Ikulu
kwa kutumia agenda za utanganyika na uzanzibari, udini, ukabila,
ubaguzi wa rangi na kwa kutumia rushwa.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;
Leo
hii baada ya zaidi ya wiki sita za kampeni za uchaguzi na zinapoingia
katika siku 10 za mwisho tumeshapata nafasi za kuwasikiliza watu
wanaoomba kutuongoza na vyama vyao. Bila ya shaka tunawatambua nani ni
nani? Naomba tuutumie Uchaguzi Mkuu huu kumuenzi Baba wa Taifa kwa
vitendo kwa kuwakataa viongozi ambao wamekiuka wosia wake. Badala
yake tuwachague viongozi watakaosaidia kuziba zile nyufa kuu nne za
taifa letu alizozizungumzia kabla ya uchaguzi wa mwaka 1995. Kwa kufanya
hivyo, tutakuwa si tu tumemuenzi bali tumejinusuru sisi wenyewe na nchi
yetu dhidi ya laana na majuto yanayoweza kutupata tukiupuuzia wosia
wake. Wapo wagombea wanaodiriki kuomba kuchaguliwa kwa sababu ya kuwa
dini fulani au madhehebu fulani. Wapo wapiga debe wa mgombea fulani
waliothubutu kuomba watu wa kabila fulani kumpigania na kumpigia kura
mgombea fulani ati kwamba wanamaslahi na mgombea huyo. Hatuchagui
mgombea wa kunufaisha kabila bali Watanzania wote. Wapo wagombea ambao
wameshindwa kukemea rushwa je tunawaelewaje? Wako tayari kupambana na
rushwa? Hapana. Bila ya shaka wao ni sehemu ya tatizo. Bila ya shaka
pia wao wanatumia rushwa kupata uongozi. Tarehe 25 Oktoba, 2015
tuwakatae.Watu wa aina hii ni balaa na janga. Tuliepushe taifa na watu
wa aina hiyo.
Uchaguzi Mkuu
Ndugu wananchi;
Jukumu
lililo mbele yetu sote tuliojiandikisha ni kujitokeza bila ya kukosa
kupiga kura tarehe 25 Oktoba, 2015 tukiwa na vitambulisho vyetu vya
mpiga kura mkononi. Bila ya hivyo hutapiga kura yako. Napenda kutumia
nafasi hii kuwakumbusha kutunza vitambulisho vyenu kwani bila kuwa navyo
hutapiga kura. Nasikitishwa sana na taarifa kuwa wapo watu wanaouza
vitambulisho vyao. Natamani habari hiyo iwe ni uvumi tu. Lakini kama ni
kweli nawashangaa sana watu hao. Kwa nini ukubali kupoteza haki yako ya
msingi ya kuchagua kiongozi wako umtakae? Nawashangaa zaidi wale
wanaonunua. Hivi hiyo ndiyo maana ya kudumisha demokrasia huko? Naomba
wajue kuwa wanatenda kosa la jinai. Vyombo vya dola vinawasaka
watakapopatikana watafikishwa mbele vya vyombo vya sheria. Na hili
litawahusu wote waliouza na kununua. Kipengele cha 2.3.1 (e)
kinasema; “kila chama cha siasa kinachoshiriki katika uchaguzi kina
wajibu wa kufuata na kutekeleza maamuzi na maelekezo ya Tume”.
Amani na Usalama wakati wa Uchaguzi Mkuu
Ndugu wananchi;
Napenda
kuwakumbusha kuwa zoezi la uchaguzi linasimamiwa kwa mujibu wa Katiba
na Sheria za nchi ambazo zinaelekeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndizo pekee zenye mamlaka ya
kuendesha na kusimamia uchaguzi. Nawaomba ndugu zangu tuheshimu kauli
na maelekezo ya tume hizo. Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama
vya upinzani wametoa maelekezo kwa wafuasi wao kutaka wakishapiga kura
wakae mita mia kulinda kura zao. Tume ya Uchaguzi imetoa tamko kwamba
kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. Wameeleza kwa usahihi kabisa
kwamba wanaosimamia na kulinda kura za wagombea na vyama vyao kwa mujibu
wa sheria ni mawakala wa wagombea na si mtu mwingine yeyote. Wao wapo
ndani ya vyumba vya kupigia kura kwa ajili hiyo. Hivyo basi wafuasi wa
vyama vya siasa msikubali kuchuuzwa na viongozi wenu kwa kuwaambia
msiondoke vituoni kwa madai ya kulinda kura zenu. Kwanza mnazilindaje,
kura zinazopigwa na kuhesabiwa ndani ya chumba cha kupigia kura.
Hapana
shaka wenzetu wana dhamira mbaya na wanachotaka ni kuhamasisha uvunjifu
wa sheria. Wana lao jambo lenye shari ndani yake. Hebu tujiulize, hivi
ikiwa wapiga kura 22,751,292 wa bara na 503,193 wa Zanzibar watabaki
kituoni kulinda kura za vyama vyao, je patatosha?
Narudia
kusisitiza: Unailindaje kura yako ukiwa umbali wa mita mia moja wakati
kura zinapigwa na kuhesabiwa ndani ya vituo vya kupigia kura? Mlinzi wa
uhakika wa kura ni wakala wa Chama chake aliyeko ndani ya chumba cha
Kupigia Kura. Tume imeshaelekeza kuwa aliyekwishapiga kura aondoke
kituoni, naomba agizo hilo liheshimiwe. Anayekaidi hatavumiliwa, hatua
za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila ya kusita. Msilazimishe
Serikali kufanya yale ambayo yasiyopendeza. Lakini hapana budi na kwa
maslahi ya taifa hatutoacha kutimiza wajibu wetu.
Ndugu Wananchi;
Hizo
ni njama za kuleta vurugu na kutaka kuwazuia watu wengine kupiga kura.
Nataka kuwahakikishia kuwa njama zao na nia yao ovu zimeshajulikana na
katu hazitofanikiwa. Sisi kwa upande wetu wa vyombo vya ulinzi na
usalama tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa agizo la Tume linatekelezwa
kwa ukamilifu. Wale wanaotaka kufanya fujo watadhibitiwa ipasavyo bila
ajizi wala kuonewa muhali. Upo usalama na ulinzi wa kutosha kuhakikisha
kuwa kila mmoja mwenye sifa ya kupiga kura atapiga kura bila ya
bughudha. Wale wenye nia ya kufanya fujo na kukaidi maelekezo halali
wana hiyari ama ya kutiii sheria na taratibu au kukabiliana na mkono wa
sheria kwa nguvu ile ile watakayoitumia wao. Kamwe hatutaruhusu,
demokrasia kutekwa nyara. Kamwe hatutawapa nafasi ya kuivuruga nchi
yetu. Wahalifu hawana kinga.
Mapambano dhidi ya UKIMWI
Ndugu Wananchi;
Ujumbe
wa Mwenge umeendelea kusisitiza mapambano dhidi ya UKIMWI. Mwaka huu,
kauli mbiu ni “Vijana wa leo na UKIMWI- Wazazi Tuwajibike”. Ni ujumbe
unaokumbusha wajibu wa wazazi na walezi katika vita dhidi ya maambukizi
mapya. Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wangu, tumepata mafanikio
ya kutia moyo katika vita dhidi ya UKIMWI.
Maambukizi
ya VVU/UKIMWI yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2007 hadi asilimia
5.1 mwaka 2012. Tumeongeza uwezo wetu wa kupima na kutambua virusi vya
UKIMWI ambapo leo tuna vituo vya upimaji wa hiyari na ushauri nasaha
(VCT) 2,929 ikilinganishwa na 96 mwaka 2005. Watu waliopima VVU/UKIWMI
kuanzia 2005 mpaka sasa wamefikia 25,048,908. Hali kadhalika idadi ya
wanaofaidika na huduma ya dawa za kufubaza (ARVs) nayo imeongezeka
kutoka 16,167 mwaka 2005 hadi 1,904,000 mwaka 2015. Huduma ya kuzuia
maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto imeongezeka kutoka vituo 544 mwaka
2005 hadi 5,361 mwaka 2015.
Ndugu wananchi;
Mafanikio
haya hayatupi sababu ya kubweteka maana maambukizi mapya bado yapo na
yanaathiri zaidi vijana na hasa vijana wa kike. Inakadiriwa kuwa tunao
wagonjwa wa UKIMWI milioni 1.4 nchini. Wito wa ujumbe huu wa mwaka huu
ni kuwakumbusha wazazi na walezi wajibu wenu. Mnapaswa kuvunja ukimya na
kuzungumza na vijana wenu kuhusu hatari inayonyemelea ujana wao,
kuwaelemisha juu ya kujitunza na kuepuka mitego ya maisha inayoweza
kuwaingiza katika tatizo hili. Huu ni wajibu ambao hamna mtu mwingine wa
kumkasimisha, maana vijana wetu wanaishi katika kaya zenu.
Vita dhidi ya Malaria
Ndugu Wananchi;
Tuliendesha
Mapambano dhidi ya malaria kwa nguvu kubwa na mafanikio ya kutia moyo
katika miaka 10 ya uongozi wangu. Nafurahi kuwa kutokana na jitihada
zetu tulizofanya na hatua tulizochukua zikiwemo usambazaji wa vyandarua
vyenye dawa; kupulizia dawa ukoko majumbani na matumizi ya dawa mseto
tumeweza kupunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia 18 mwaka 2007
hadi asilimia 10 mwaka 2012, na vifo vitokanavyo na malaria kutoka
watu 41 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2004 hadi watu 12 kwa vizazi
hai 100,000 mwaka 2014. Kwa upande wa Zanzibar, kutokana na jitihada
kama hizo, haswa ila ya kupulizia mazalia ya mbu, wameweza kutokomeza
malaria ambako sasa kiwango cha maambukizi ni asilimia 0.2.
Ndugu wananchi;
Jambo
muhimu tulilofanya ambalo litatupa ushindi wa kudumu dhidi ya malaria
ni kujengwa kwa Kiwanda cha Kutengeneza Madawa ya Viuadudu pale Kibaha.
Kiwanda hiki kitazalisha madawa ya kupulizia kwenye mazalia ya mbu na
hasa kuua viluviluvi vya mbu. Tutang’oa mzizi wa fitina wa malaria kwani
hatimae mbu hawatakuwepo.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tunaendelea
kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Haya ni
mapambano makali ambayo hatuna budi kupambana kweli kweli mpaka
tushinde. Dawa hizi za kulevya zinaathiri zaidi vijana wetu na
kudhoofisha nguvu kazi muhimu ya taifa la leo na kesho. Aidha, ni
kichocheo kikubwa cha vitendo vya uhalifu.
Ndugu wananchi;
Bahati
nzuri, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, sasa walioathirika na dawa za
kulevya wanaweza kupata matibabu na kupona. Nafurahishwa na kauli mbiu
ya Mwenge mwaka huu isemayo, “Uteja wa Dawa za Kulevya Unazuilika na
Kutibika; Chukua Hatua”. Inahamasisha watumiaji wa dawa za kulevya
kuchukua hatua na kupata tiba. Hali kadhalika, inakumbusha wajibu wetu
sote kuwasaidia wale walioathirika kwa kuhakikisha kuwa wanapata ushauri
nasaha na tiba ambazo zinatolewa katika vituo vya serikali tena bila
gharama yoyote.
Serikali
imeendelea kutoa huduma katika vitengo vya afya ya akili vilivyopo
Mirembe na Lutindi. Vitengo kama hivi vimeanzishwa pia katika hospitali
Muhimbili, Mwananyamala na Temeke. Sasa tunajenga Kituo cha Matibabu cha
kisasa cha Waathirika Madawa ya Kulevya hapa Itega, Dodoma ambacho
kitakuwa kituo kikubwa kuliko vyote nchini. Kutokana na juhudi hizi,
nchi yetu imekuwa nchi ya kwanza Kusini mwa jangwa la Sahara kuanzisha
huduma hii kwenye mfumo wa afya ya jamii (public health).
Ndugu wananchi;
Upande
wa pili wa mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya yaliendelea
kwa nguvu. Huku nako tumepata mafanikio ya kutia moyo. Kati ya mwaka
2010 mpaka 2014 jumla ya kesi za dawa za kulevya 40,930 zilitolewa
taarifa polisi. Kati yake kesi 22,167 zilifikishwa
Mahakamani, kesi 18,763 zinaendelea kufanyiwa uchunguzi na
kesi 1,082 zimekamilika. Kati ya mwaka 2005 na 2014 tumefanikiwa
kukamata watuhumiwa 1,704 wa cocaine, wahutumiwa 2,149 wa heroine na
watuhumiwa 5,462 wa mirungi. Mafanikio makubwa kuliko yote ni yale
kukamatwa kwa kilo 211 za heroine mkoani Lindi mwaka 2012 kikiwa ni
kiasi kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa Barani Afrika.
Ndugu Wananchi;
Tumekwenda
mbali zaidi kukabiliana na mtandao wa uuzaji na usafirishaji wa dawa za
kulevya. Naweza kusema kuwa tumewadhibiti kwa kiasi kikubwa mtandao
huu na sasa wamebanwa kweli kweli. Tumeongeza uwezo wetu wa kupambana na
biashara ya madawa ya kulevya kwa kuipitia upya na kuibadili Sheria ya
Kudhibiti Biashara ya Dawa za Kulevya ya mwaka 1995 na kutunga Sheria
mpya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015,
iliyoanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo pamoja
na kuongeza makali ya adhabu ya makosa ya madawa ya kulevya, imeanzisha
Mamlaka mpya yenye uwezo wa kupeleleza, kupekua na kukamata watuhumiwa
wa dawa za kulevya. Awali, Tume kwa muundo wake, ilitegemea zaidi
ushirikiano wa Polisi na mamlaka nyingine kutekeleza wajibu wake.
Serikali itaendelea kuiwezesha Mamlaka hii kufanya kazi yake ipasavyo.
Tunachoomba kutoka kwenu ni ushirikiano wenu. Vita hii tutashinda.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea
na mapambano dhidi ya rushwa na mafanikio yameendelea kupatikana katika
kipindi cha miaka 10. Hatua za kisera na kisheria tulizochukua ikiwemo
kubadilisha Sheria iliyokuwapo ya Kupambana na Rushwa, kuongeza idadi
ya makosa kutoka 4 hadi 24, kujenga uwezo wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mafunzo, rasilimali watu na vitendea
kazi kwa pamoja zimeongeza kasi ya kupambana na rushwa. Katika kipindi
cha miaka 10, zimefunguliwa kesi 2,185 Mahakamani,
watuhumiwa 611 wametiwa hatiani na fedha kiasi cha shilingi bilioni 93,
410,572, 117 kimeokolewa na kesi 658 zinaendelea Mahakamani.
Nafurahi
kuwa nimejenga msingi mzuri wa vita dhidi ya rushwa. Sina mashaka kuwa
katika awamu ijayo vita hii itashika kasi zaidi hasa ikiwa mgombea wa
Chama changu atashinda kwani amezungumzia kupambana na rushwa na kuahidi
kuunda Mahakama Maalum ya Rushwa. Sina mashaka kuwa, uchaguzi huu
tutachagua wale wagombea wanaozungumza lugha ya kupambana na rushwa kwa
maneno, nyuso zao na vitendo. Viongozi wasioionea rushwa haya. Hii ndio
siri ya kuikabili rushwa. Inawezekana, timiza wajibu wako tarehe 25
Oktoba, 2015.
Wiki ya Vijana
Ndugu Wananchi;
Nimepata
fursa ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya shughuli za vijana katika
viwanja vya barafu. Nimeguswa sana na ubunifu wao na ari yao ya
kujikwamua kwa kujiajiri badala ya kungoja kuajiriwa. Mahitaji yao
makubwa ni kuwezeshwa tu ili waweze kupanua shughuli zao na kuajiri
vijana wenzao.
Katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita tumejitahidi kutoa fursa kwa vijana na
kuchochea maendeleo yao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Mwaka 2005
Mfuko huu ulikuwa na kiasi cha shilingi milioni 100,000,000 mwaka 2005
na sasa bajeti yake imefikia shilingi bilioni 6,000,000,000 na
umefaidisha vijana 10,241. Mwaka jana katika sherehe za Mwenge kule
Tabora, nilizikumbusha Halmashauri zote za Wilaya na Miji kutekeleza kwa
ukamilifu agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa mwaka kwa
ajili ya shughuli za maendeleo ya Vijana na Wanawake. Nafurahi kuwa
zimejitahidi kufanya hivyo na mwaka huu wa fedha zilitengwa kiasi
cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya mfuko huo. Natambua kuwa mahitaji
ya fedha yameongezeka sana kutokana na mwamko ulioko sasa. Nina imani
serikali ijayo italipa jambo hili kipaumbele zaidi. Muhimu vijana
msikilize wagombea na vyama vyao kwa makini kisha mfanye maamuzi sahihi.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Sherehe
hizi za Mwenge ndizo zitakuwa sherehe za mwisho kwangu kushiriki nikiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nafurahi kuwa katika kipindi
chote cha uongozi wangu, Mwenge wa uhuru umeendelea kuwa na mafanikio na
kuleta nuru zaidi, mshikamano zaidi matumaini zaidi na maendeleo zaidi
kote ulikopita. Ninapoondoka rai yangu kwenu ni kuwa namna moja ya
kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni kuudumisha
Mwenge huu wa Uhuru ambao aliuasisi yeye mwenyewe.
Nitumie
pia fursa hii kuwasisitiza tena kujitokeza kupiga kura ili kuchagua
viongozi mnaowataka. Narudia kuwahakikishia kwa mara nyingine tena
usalama katika kipindi chote cha uchaguzi. Kila mmoja na atimize wajibu
wake wa kulinda amani ya nchi yetu katika kipindi hiki.
Nawatakia kila la kheri katika shughuli zenu za kila siku.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment