Sheria Mpya ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015 imeendelea kuonyesha meno yake kufuatia kijana Israel William (20), kufikishwa katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo, akishitakiwa kwa makosa mawili ya kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo dhidi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akisoma
mashitaka dhidi ya mtuhumiwa huyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi
Renatus Rutatinisibwa, Mwendesha Mashitaka wa serikali Estazia Wilson,
amesema kijana huyo alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya
Septemba 10 na Oktoba 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Estazia
amesema mshitakiwa aliandika na kusambaza katika mtandao wa Facebook
taarifa zisizo sahihi, kuwa wafanyakazi wa TCRA wamekuwa wakilawitiwa,
akijua kuwa taarifa hizo sio sahihi na ni kashfa.
Mshitakiwa huyo amekana mashitaka hayo na upande wa mashitaka umesema uchunguzi wa suala hilo bado haujakamilika.
Mtuhumiwa huyo amepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Israel
anakuwa mhanga wa pili wa sheria hiyo mpya ya makosa ya mtandaoni,
kufuatia pia kufikishwa mahakamani kwa mwanafunzi wa Chuo cha DIT
Benedict Ngonyani, kwa kusambaza taarifa za uongo kuwa Mkuu wa Majeshi
ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF) Jenerali Adolph Mwamunyange
amelishwa sumu.
Mwanasheria
Mkuu wa TCRA Kalungula, kwa mara nyingine amewaonya vijana dhidi ya
matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kuwashauri kufuata kanuni na
taratibu za mawasiliano na matumizi ya mitandao hiyo kwa mujibu wa
sheria.
Amesisitiza kuwa hakuna mtu atakayeachwa kwa kutumia vibaya mitandao ya kijamii na kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni.
Post a Comment