Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amefichua mazito baada ya kueleza hadharani kuwa kamwe chama chake na washirika wao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawatakubali matokeo ya uchaguzi mkuu yatakayobainika kuwa yamepikwa.
Kadhalika,
alisema ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na mamlaka za serikali
iliyopo madarakani kuheshimu maamuzi ya wananchi yatakayotokana na kura
watakazopiga kwenye uchaguzi mkuu Jumapili ijayo, kwani kinyume chake
ni kuhatarisha amani iliyopo.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa
aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi wa chama cha
National League for Democracy (NLD) aliyefariki dunia wiki iliyopita,
Mbowe alisema watakubali matokeo ikiwa mchakato wote wa uchaguzi utakuwa
huru, wa haki na usiokuwa na chembe ya mizengwe katika kila hatua.
Chadema
na vyama vingine vinavyounda Ukawa vya Chama cha Wananchi (Cuf),
NCCR-Mageuzi na NLD, vimemsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kuwa mgombea wao wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, huku pia wakishirikiana kusimamisha wagombea wa nafasi za
ubunge, udiwani na uwakilishi.
Akieleza
zaidi, Mbowe aliyekuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi kuhusu
namna walivyojiandaa kupokea matokeo baada ya uchaguzi mkuu Jumapili
ijayo, alisema Ukawa itakuwa tayari kupokea matokeo yatakayotangazwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ikiwa wataridhika kuwa hatua zote za
kisheria na haki za mchakato wa uchaguzi huo kuanzia katika kampeni hadi
upigaji kura zimezingatiwa ipasavyo.
Aliongeza kuwa kinyume chake, wao (Ukawa) hawatakuwa tayari kupokea matokeo yatokanayo na hila za namna yoyote ile.
Akifafanua,
Mbowe alisema Ukawa haiwezi kukataa matokeo kwa sababu ya kushindwa
katika uchaguzi, bali wanachoangalia ni kuzingatiwa kwa haki, sheria na
uwazi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo.
“Kupokea
matokeo ni mchakato ambao unaanzia katika hatua za kampeni, upigaji
kura hadi wakati matokeo yanatangazwa. Siwezi kusema eti tutakataa
matokeo kwa sababu tu Nec imetangaza halafu tukaonekana tumeshindwa… la
hasha. Bali tutapokea matokeo kama haki, uwazi, sheria na taratibu
nyingine zimezingatiwa mpaka kupatikana kwa matokeo,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Sisi
Chadema na Ukawa tunaamini kwamba wananchi watamchagua kiongozi
wanayemuamini. Lakini kama watu wengine wenye mamlaka ndani ya nchi
wakaamua kupindisha sheria na kupindisha maamuzi ya wananchi kupitia
sanduku la kura, kamwe hatutakubali matokeo hayo. Na hapo amani
tunayoihubiri inaweza kuwa ngumu ‘kui-control’ (kuidhibiti),” alisema.
Kuhusiana
na mvutano juu ya wananchi kuondoka vituoni baada ya kupiga kura na
siyo kukaa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kura, Mbowe alisema msimao
wao wa kulinda kura uko pale pale kwa kuwa wana amini kuwa hiyo ni haki
yao kisheria.
“Kura
ni mali na kama hivyo ndivyo ni lazima tuilinde, tumepanga kulinda kura
zetu kwa amani na utulivu nje ya mita 200 kama sheria inavyosema…
tunaomba kila mtu na vyombo vya dola viheshimu,” alisema.
Aliongeza: “Kuhubiri
amani bila haki ni kulishana upepo. Mamlaka zote za taifa zina wajibu
wa kuheshimu sheria za nchi na kuacha kutumia mamlaka zao vibaya na bila
vitisho. Kila mmoja akitekeleza wajibu wake kwa misingi ya sheria, hiyo
amani wala haitatafutwa, itapatikana tu.”
Mbali
na Mbowe, wengine waliojitokeza katika shughuli ya kuuaga mwili wa Dk.
Makaidi ni Lowassa, Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi , Waziri Mkuu Mstaafu
aliyehamia kambi ya Ukawa, Frederick Sumaye, Kaimu Katibu Mkuu wa Cuf,
Twaha Tasilima, Katibu Mkuu wa NLD, Tozzy Matwanga na Makamu Mwenyekiti
wa CCM, Philip Mangula.
Wengine waliokuwapo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee.
Jaji Mkuu Ataka Mahakama Iachiwe Swala la Mita 200
Wakati
Mbowe akisisitiza msimamo wa kuwataka wafuasi wa Ukawa kutorudi
nyumbani baada ya kupiga kura na badala yake kukaa umbali wa mita 200
kutoka vituo vya kupigia kura ili kulinda kura zao, Jaji Mkuu Othman
Chande alikataa kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka mahakama
iachiwe ili itoe uamuzi wake kwa haki.
Jaji
Chande aliyasema hayo jana wakati alipoulizwa na waandishi baada ya
kufungua mafunzo kwa majaji na Wasajili Mahakama Kuu Jijini Dar es
Salaam, juu ya wajibu wa mahakama katika uchaguzi mkuu na namna ya
kukabiliana na changamoto zilizopo katika kusimamia kesi za uchaguzi,
yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Tayari
Mahakama Kuu imeshapanga majaji watatu kushughulikia suala hilo
lililoibua mvutano mkali hivi karibuni baina ya viongozi wa Ukawa na
wakuu wa Nec na Jeshi la Polisi. Kesi hiyo itaanza kunguruma rasmi leo.
Katika
hatua nyingine, Jaji Chande alikiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wenye
mchuano mkali na kwamba mahakama zimejiandaa kumaliza kesi
zitakazotokana na uchaguzi huo kabla ya miezi sita inayotajwa kisheria.
Alisema
mwaka 2010 kulikuwa na kesi 44 za uchaguzi kwa ngazi za Ubunge na kati
yake, 17 zilikwenda hadi hatua ya mwisho baada ya kutolewa ushahidi huku
nyingine zikiisha katika hatua za awali.
“Ushindani
ni mkali katika uchaguzi huu, tunatarajia kupokea kesi nyingi za
uchaguzi. Tumejiandaa kupokea, kusikiliza kwa haraka ili kuwezesha
wapigakura kujua mshindi halali ni yupi,” alisema.
Akieleza zaidi, alisema sheria imeweka wazi kuwa anayestahili kufungua kesi siyo mpigakura bali wagombea wenyewe.
Mratibu
THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema wameshirikiana na Ofisi ya Jaji
Kiongozi kuandaa mafunzo hayo kwa kutambua kuwa ni wadau muhimu katika
kushughulikia kesi za uchaguzi ili kuwezesha haki kutendeka kwa haraka
Goodluck Jonathan Akiri Ushindani Ni Mkali Kati Ya CCM na UKAWA
Mkuu
wa Jopo la Waangalizi kutoka Jumuiya ya Madola na aliyekuwa Rais wa
Nigeria, Goodluck Jonathan, amekiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu nchini
Tanzania una ushindani mkali kutokana na namna vyama vilivyojiandaa
lakini akawataka wagombea wote wa nafasi za urais kujiandaa kukubali
matokeo kwa maslahi mapana ya taifa lao.
Wagombea wanaochuana kwa karibu ni, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Lowassa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili
nchini, Jonathan aliyekubali kuondoka madarakani Mei mwaka huu na
kumpisha Muhammad Buhari baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu nchini
mwake, alisema katika uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa na
hivyo wagombea wajiandae kwa matokeo yoyote ili kuiacha nchi yao ikiwa
salama.
Alisema
ijapokuwa ushindani ni mkali, Jumuiya ya Madola inaamini kuwa uchaguzi
utakuwa huru na haki na kwamba imani yao kubwa ni Tanzania kusimamia
demokrasia iliyokuwapo wakati wote tangu ipatre uhuru wake mwaka 1961.
Jonathan anaongeza jopo lenye waangalizi 14 kutoka mataifa mbalimbali yaliyo wanachama wa Jumuiya ya Madola
Post a Comment