Siku
moja baada ya kunaswa mashine zilizosadikiwa kuwa ni za uandikishaji
wapiga kura kwa njia ya kielektroniki (BVR), zilizokuwa zikiandikisha
wafanyakazi wa Kiwanda cha MM Steel jijini Dar es Salaam, Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) imeibuka na kueleza kuwa mashine hizo ni 'feki' na
wala hazihusiani kwa namna yoyote na vifaa vyao.
Jaji
mstaafu Damian Lubuva akizungumza na viongozi wa Chadema. Kutoka kulia
ni Wakili wa chama hicho, John Malya na Reginald Munisi.
Mkurugenzi
wa NEC, Ramadhani Kailima, ndiye aliyetoa ufafanuzi huo wakati
akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na mashine hizo ambazo zilikamatwa
juzi wakati zikiendelea kutumiwa kwa shughuli ya uandikishaji wa
wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo katika eneo la Mikocheni.
Wakati
Polisi wakizikamata jana kwa ushirikiano na maofisa kadhaa wa NEC,
tayari mashine hizo zinavyofanana na BVR zilishaandikisha wafanyakazi
zaidi ya 100 wa Kiwanda cha MM Steel.
Akielezea
zaidi kuhusiana na tukio hilo, Kailima alisema kuwa, mara baada ya
kupata taarifa za kuwapo kwa mashine hizo, walienda kuzikagua na kubaini
kuwa hazina uhusiano na zile za Biometric Voter Registation (BVR),
zilizotumiwa na wao (NEC) kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
“Hakuna
ukweli wowote kuwa zile ni mashine za BVR na tumebaini ni feki, tena ni
sawa na zile zinazotumika kwenye ofisi mbalimbali kuandikisha
wafanyakazi wake... hawa waliosema ni mashine za kuandikishia wapiga
kura hawako sahihi... si kweli,” alisema Kailima.
Alisema
endapo watu wataendelea kuwa na shaka juu ya namna NEC inavyofanya kazi
kwa sababu tu ya kuona mashine kama hizo, basi wanaweza pia kukamata
mashine za ofisi nyingi zikiwamo za kwenye viwanja vya ndege, hospitali
na hata manispaa kama ya Kinondoni ambayo hutumia mashine kama hizo kwa
shughuli zake mbalimbali.
“Mashine
tulizozikuta kwenye hiyo ofisi jana (juzi) ni computer mpakato (laptop)
na mashine za kuchukua alama za vidole. Hata wale wafanyakazi
tulipowahoji walibainisha kuwa wanazitumia kuorodhesha wafanyakazi wao
kwa ajili ya usalama wa ofisi... na tena zipo ofisi nyingi zinatumia
mashine hizo,” alisema Kailima.
Kailima
alitoa tahadhari kwa wataalamu wanaovishauri vyama vya siasa kuwa
makini na kuacha kupotosha kwa kuwaleza mambo yasiyo na ukweli, hasa
kuhusiana na NEC kwani wao wanafanya kazi zao kisayansi zaidi na hakuna
fursa ya kuwapo kwa ubabaishaji wa aina yoyote.
Aliongeza
kuwa hawafanyi kazi zao kwa misikumo ya kisiasa, bali huzingatia
utaalamu na hivyo wanaotumiwa kwa ushauri na vyama waache kuwadanganya
wanasiasa.
“Hawa wanasiasa wanadanganywa na watu wanaojiita wataalamu... mashine hizi (zilizokamatwa) hazihusiani na BVR," alisisitiza.
CHADEMA WAHUSISHWA UCHUNGUZI
Akieleza
zaidi juu ya hatua walizochukua baada ya tukio la juzi, Kailima alisema
kuwa (jana) walifanya uchunguzi wa mashine hizo kwa kushirikiana na
wawakilishi kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao
ndiyo walitoa malalamiko kwao kuhusiana na madai ya kuwapo kwa mashine
kama BVR zinazotumiwa kuandikisha watu.
“Wataalamu
wao (Chadema) walikuja na tukathibitisha (wote) zile ni feki na
hazihusiani kabisa na mashine zetu za BVR,” alisema Kailima.
Kwa
upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) John Mnyika, aliitaka NEC ivikabidhi vyama vya siasa nakala za
daftari la kudumu la wapiga kura ili kuepukana na njama za wizi wa kura
alizodai zinaweza kufanywa na chama tawala -- Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Akizungumia
tukio la juzi kuhusu kukamatwa kwa vifaa vinavyofanana na mashine za
BVR, Mnyika alisema suala hilo walilikabidhi kwa maofisa wa NEC na Jeshi
la Polisi ambao wanalichunguza kwa kushirikiana na maofisa wa Chadema
ili kubaini ukweli.
Kadhalika,
Mnyika aliitaka NEC kushughulikia suala hilo haraka na kutishia kuwa
wasipotoa majibu ya kina ndani ya siku tatu, atashauri wanachama wenzake
kuishinikiza ifanye hivyo ili kuondoa shaka iliyopo.
Hata
hivyo, Mnyika aliyasema hayo kabla ya kutolewa kwa maelezo ya Kailima
kuhusiana na uchunguzi walioufanya kwa mashine hizo zilizokamatwa
Mikocheni.
Juzi,
Chadema walipata taarifa kutoka vyanzo vyao vyao kuwa kuna mashine
zinazofanana na BVR zinaandikisha watu na hivyo wakashirikiana na Polisi
na NEC kuvikamata kabla ya kwenda kuvichunguza. Meneja Mawasiliano wa
MM Steel, Aboubakar Mlawa, alieleza kuwa kampuni yao imeamua kuandikisha
wafanyakazi wao kwa nia ya kudhibiti usalama vitendo vya wizi, na
kwamba tayari walishaandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 kati ya 900
waliokuwa wakitarajiwa kutoka kwenye viwanda vyao saba.
Post a Comment