Na January Makamba
Tarehe
25 mwezi huu Oktoba, Watanzania watapiga kura kumchagua rais wao wa
tano, wabunge na madiwani. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umekuwa na
msisimko mkubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi
mwaka 1995. Mengi yamendikwa kuhusu uchaguzi huu, hususan kutokana na
hisia kwamba safari hii Upinzani una nafasi ya kukiondoa madarakani moja
ya vyama vikubwa na vyenye muundo bora barani Afrika, chama tawala,
Chama Cha Mapinduzi (CCM). Matukio mbalimbali kuelekea uchaguzi huo
yameleta shauku inayoweza kutengeneza hadithi ya kusisimua.
Nikiwa sehemu ya Timu ya
Kampeni ya CCM,na kwa manufaa ya wote ambao wangependa kuwa na mtizamo
tofauti, ninatoa sababu 9 kwa nini tunaamini kuwa CCM itaibuka mshindi
na kwanini Dkt John Pombe Magufuli atakuwa Rais ajaye wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
1. Ugombea ‘fyongo’ (flawed) wa Edward Lowassa
Ilishabainika kuwa uchaguzi
huu ungekuwa mgumu kwa CCM bila kujali nani angekuwa mgombea urais kwa
tiketi ya Upinzani. Lakini matokeo ya uchaguzi huu yalielemea upande wa
CCM pale Upinzani ulipomchagua Lowassa kuwa mgombea wao. Ni rahisi kwa
CCM kuchuana na Lowassa kuliko laiti mgombea wa Upinzani angekuwa Dkt
Wilbrod Slaa, ambaye ndiye aliandaliwa kuwa mgombea kabla ya ‘kusukumwa
kando’ na nafasi hiyo kupewa Lowassa. Slaa alikuwa na uadilifu katika
maeneo mengi, na aliaminika. Kwa Lowassa, ni vigumu na inanyima raha
kuchuana na mfumo aliyoshiriki kujenga na ambao ulikuwa sehemu ya maisha
yake hadi Agosti mwaka huu alipohamia Upinzani. CCM ilikuwa na nafasi
ya kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais. Hatukufanya
hivyo kwa sababu rahisi tu kwamba ingekuwa vigumu mno kumkabidhi kwa
wananchi mgombea wa matarajio ya baadaye ambaye ni kiashirio cha yale
yasiyowaridhisha wananchi kuhusu CCM. Kuna wanaoamini kuwa uchaguzi huu
ni mgumu kwa vile Lowassa ndiye mgombea wa Upinzani. Sisi twaamini
kwamba uchaguzi huu ungekuwa mgumu mara kumi zaidi laiti Lowassa
angekuwa ndiye mgombea wetu.
2. Upinzani umesalimisha ajenda yake ya kupinga ufisadi
Kipindi cha miaka 10
iliyopita kimetawaliwa na matukio mbalimbali ya kuwabainisha mafisadi na
kuwachukulia hatua. Vyombo vya habari, taasisi za kiraia na Bunge
vimefanya kazi nzuri kushughulikia suala hilo. Rais Jakaya Kikwete
ameweka historia kwa kuamuru ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kupatikana kwa wananchi na kujadiliwa kwa uwazi
Bungeni. Waziri Mkuu aliyekuwa madarakani, si mwingine bali Lowassa,
alijiuzulu kwa sababu ya kashfa ya rushwa. Mawaziri kadhaa walitimuliwa
kazi na manaibu waziri wawili wanatumikia vifungo jela. Huu ni
uwajibikaji wa hali ya juu japokuwa kuna wanaoweza kudhani ni hatua
ndogo. Umma umeamka.
Upinzani ulijenga hadhi yake
kwa kuongelewa sana kuhusu ufisadi. Kilele cha Upinzani kilijiri mwaka
2007 katika mikutano mkubwa wa hadhara ambapo walitangaza majina 10 ya
watu waliowaita mafisadi wakubwa zaidi, katika kilichokuja kufahamika
kama Orodha ya Aibu (List of Shame). Lowassa alikuwa kinara kwenye
orodha hiyo.
Ilitarajiwa kuwa Uchaguzi
Mkuu huu uwe ‘hukumu’ kwa CCM kuhusu ufisadi. Upinzani ulitarajiwa
kuitumia ajenda ya ufisadi ambayo inawagusa watu wengi. Lakini ghafla,
kwa kumteua mwanasiasa, ambaye kwa jitihada zao wenyewe Wapinzani,
amefahamika zaidi kwa ufisadi, iliwalazimu kuzika ajenda hiyo.
Kilichofuata baada ya hapo ni kituko na kichekesho. Wale mashujaa wa
mapambano dhidin ya ufisadi walijikuta wakilazimika ‘kulamba matapishi
yao.’ Wengi wao waliokuwa mahiri katika mitandao ya kijamii walilazimika
kufuta historia ya baadhi ya waliyoyaandika mtandaoni walipokuwa
wakikemea ufisadi, lakini si kabla ya maandiko yao kunaswa kwa
‘screenshots.’ Ulikuwa ni ukweli wa kushangaza. Ni Dkt Slaa na Professa
Ibrahmi Lipumba, viongozi muhimu wa Upinzani tangu miaka ya Tisini,
walioamua kujiuzulu nyadhifa zao kwa kukerwa na uamuzi wa Upinzani
kumpokea Lowassa.Matokeo yake, Upinzani walijikuta wakichana kadi yao
turufu- ajenda dhidi ya ufisadi. Ni nadra kwao kuongelewa suala hilo, na
wanapojaribu kufanya hivyo, ni kwa kujitetea tu.
Jioni moja mwezi Agosti,
nilimwona Mbunge wa Upinzani, Peter Msigwa, katika mdahalo kwenye
runinga. Aliongelea kitu ambacho kilijumuisha mtizamo wa Upinzani kwa
muda huo, na kiliniacha hoi. Alisema, kabla hawajampokea Lowassa,
walifanya utafiti wao, na “ufisadi sio ajenda muhimu kwa taifa letu.”
Alidai kwamba wenye ushahidi kuhusu ufisadi wa Lowassa wajitokeze
hadharani.Alionekana kusahau kuwa walipomtaja Lowassa katika List of
Shame, walitangaza hadharani kuwa wana ushahidi. Muda si mrefu uliopita,
CCM ilikuwa ikiwaomba Wapinzani kuleta ushahidi kila yalipojitokeza
madai ya ufisadi dhidi ya viongozi wa chama na serikali allegations were
leveled against the party and its leaders. Haikupendeza kuingiza hoja
za kisheria katika masuala ya kimaadili. Upinzani sasa umeamua kwa hiari
yao kuchukua ‘chembemoyo’ wakati ambapo viongozi wa CCM wanaongelea
ufisadi kwa ujasiri na msisitizo.
Uchaguzi huu Mkuu ni muhimu
sana kwa Upinzani. Kimsingi, unaweza kuwa na madhara makubwa. Endapo
watashindwa hapo Jumapili, ‘watapotea’ kwa muongo mzima ujao. Ndio maana
inashangaza kuona wamechukua uamuzi wa kukimbia ajenda yao kuu ya
kupambana na ufisadi ambayo iliwatambulisha na kuwaimarisha. Na kuwapa
nguvu kukubalika kwa wapigakura. Kuona wanatarajia kushinda ni miujiza
mkubwa.
3. Mabadiliko ambayo kamwe huwezi kuyaamini
Ukizinguka jijini Dar es
Salaam utakutana na mabango ya Upinzani yanayodaia “Ni Muda wa
Mabadiliko.” Lakini ukisikiliza mikutano yao ya kampeni, ni porojo na
hasira tu. Wasemaji wakuu katika mikutano hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani
na kada wa muda mrefu wa CCM, Frederick Sumaye na Lowassa mwenyewe. Kwa
pamoja, wamekuwa wana-CCM na katika nyadhifa za juu serikalini kwa
zaidi ya miaka 50. Kwa hiyo inasikitisha kusikiliza kauli zao –
zinazokosa imani na kupalizwa na aibu – wakipambana na mfumo
walioshiriki kujenga, uliojenga tabia zao za kisiasa, na ambao walikuwa
wakiusifu miezi mwili tu iliyopita.
Kutokuwa wakweli na kuweka
mbele maslahi binafsi kwawatuma kudai kuwa CCM haijafanya chochote
katika miaka miaka 50 iliyopita. Inapotokea viongozi wawili waandamizi
wa chama na serikali kwa zaidi ya miaka 30, wote wakiwa walioshika
Uwaziri Mkuu, kudai kuwa hakuna chochote kilichofanyika katika miaka 50
iliyopita, wajihukumu wenyewe. Si kwa muundo, mwonekano au ukweli,
wanasiasa hao wanasimamia mabadiliko. Yayumkinika kuhitimisha
kuwa mabadiliko wanayoongelea ni kuhusu kubadili chombo kilichowaingiza
madarakani, mabadiliko ya sare tu za chama. Hawana habari na mabadiliko
ya maisha ya wananchi wa kawaida. Wapigakura wameanza kushtukia ukweli
huo.
4. Migogoro na mkanganyiko ndani ya UKAWA
Huko nyuma, kila ulipojiri
uchaguzi, Upinzani ulijaribu kuunganisha nguvu ili kuing’oa CCM
madarakani.Na kila mara jitihada za ushirikiano zilishindikana. Mwaka
2014, mjadala kuhusu Katiba Mpya kuataka serikali tatu uliwapatia ajenda
ya kuwaunganisha pamoja. Kisha wakaamua kutafsiri ushirikiano huo kuwa
wa kisiasa, wakaafikiana kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya
urais na kugawana majimbo.
Baada ya hapo kukajitokeza
unafiki wa wazi. Kuonyesha kuwa matamanio yaliwekwa mbele ya kanuni
zilizopatikana kwa jitihada ngumu, chama ambacho jina lake linajumuisha
maneno ‘demokrasia’ na ‘maendeleo’ kilitemea mate mchakato wake chenyewe
wa kidemokrasia na mshikamano kupata mgombea wake wa urais, na
kukurupuka kumpitisha kada wa muda mrefu wa CCM ambaye jitihada zake
kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho tawala ziligonhga mwamba.
Waliamini kwamba uamuzi wa
Lowassa kuhama CCM ungekiathiri chama hicho tawala, wakitarajia vigogo
kadhaa wangemfuata huo Upinzani. Badala yake, ujio wake huko ukapelekea
kuondoka kwa wanasiasa wawili waliokuwa nguzo muhimu kwa Upinzani, Dkt
Slaa na Prof Lipumba.Kadhalika, wanachama wengine muhimu waliohama na
kujiunga na chama cha ACT- Wazalendo, ambacho hakikujiunga na UKAWA.
Kana kwamba hiyo haitoshi,
makubaliano ya UKAWA kusimamisha mgombea mmoja kila jimbo yalikumbwa na
mushkeli katika majimbo kadhaa na kupelekea malalamiko yaliyosababisha
ugumu katika kampeni za Lowassa.
Huko Masasi, mgombea mwenza
wa Lowassa, Juma Duni, alilazimika kuokolewa jukwaani baada ya
waliohudhuria mikutano wake wa kampeni kupiga kelele kuwa wataipigia
kura CCM. Katika jimbo la Nzega, Lowassa alilazimika kuendesha ‘kura ya
sauti’ kuwauliza waliohudhuria mikutano wake wa kampeni wanamhitaji
mgombea gani kati ya wawili wa UKAWA waliokuwa wanachuana. Mpango mzima
wa ushirikiano miongoni mwa vyama vinavyounda UKAWA umekwenda mrama.CCM
sasa ipo katika nafasi nzuri ya kujinyakulia majimbo ambayo vinginevyo
yangekwenda kwa wagombea wa Upinzani.
Lakini kilele cha unafiki wa
UKAWA ni hiki. Umoja huo uliundwa ili kutetea Katiba Pendekezwa
iliyoshauri muundo wa Muungano wa serikali tatu. Kanuni hiyo ya msingi
iliwekwa kando pale UKAWA walipomchagua mgombea wao wa tiketi ya urais,
Lowassa, ambaye alikuwa mtetezi mkubwa wa muundo wa Muungano wa serikali
mbili. Kwa wengi wasioendeshwa na propaganda, uamuzi wa kutelekeza
suala la msingi lililopelekea umoja wa vyama hivyo, kwa ajili tu ya
imani ya kufikirika ya kushinda urais, yaashiria uchu wa madaraka na sio
mabadiliko yanayohubiriwa kwa wananchi.
5. Lowassa kushindwa kufanya kampeni nchi nzima
Lowassa anaonekana kutokuwa
na uwezo wa kusafiri kwa urefu na upana wa Tanzania kufanya kampeni.
Mara nyingi amekuwa akitumia usafiri wa anga kwenda mikoani ambako
hufanya mikutano mikubwa kwenye makao makuu ya mikoa, kutembelea majimbo
mawili au matatu ya jirani kwa helikopta, na kurejea jijini Dar es
Salaam. Huko Tanga, kwa mfano, alifanya kampeni katika majimbo matatu tu
kati ya tisa mkoani humo. Mkoani Ruvuma, alifanya kampeni katika
majimbo matatu kati ya tisa, Kigoma majimbo mawili kati ya manane, na
Kagera majimbo matatu tu.
Kinyume chake, mgombea wa
CCM, Magufuli amekuwa barabarani tangu Agosti 23, huku akipumzika kwa
siku tatu. Anatumia usafiri wa gari, akitembelea kijiji baada ya kijiji,
na kufanya mikutano kati ya minane hadi 12 kwa siku. Aina hii ya
kufanya kampeni ‘kwa rejareja’ inabaki kuwa nguzo pekee ya
kujihakikishia ushindi kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania, hususan
katika maeneo ya vijijini ambayo usikivu na kuonekana kwa vyombo vya
habari ni mdogo. Wakati Lowassa anavutia wahudhuriaji wengi katika
mikutano yake katika miji mikubwa, Magufuli anajipatia wahudhuriaji
wengi katika kila kona ya Tanzania. Kama idadi ya wahudhuriaji katika
mikutano hiyo ya kampeni inamaanisha wingi wa kura, basi kwa hakika CCM
itashinda. Lakini tofauti na Upinzani, CCM haidanganyiki na wingi huo wa
wahudhuriaji katika mikutano ya kampeni. Rekodi ya mahudhurio makubwa
ilikuwa ikishikiliwa na Agustino Lyatonga Mrema, mgombea maarufu wa kiti
cha urais kwa tiketi ya Upinzani mwaka 1995 (ambaye pia alijiunga na
Upinzani akitokea CCM). Hata hivyo alishindwa kwenye uchaguzi huo. Sie
twategemea kitu kingine.
6. Mfumo imara wa CCM katika uhamasishaji kuanzia ngazi ya chini kabisa.
Katika Tanzania, vyama
vichache mno vinavyoweza kuchuana na uwezo wa CCM kuhamasisha wananchi.
Wakati Wapinzani huhadaiwa na ‘mahaba’ wakati wa kampeni za uchaguzi,
mahudhurio makubwa kwenye mikutano yao ya kampeni na vichwa vya habari
magazetini, CCM hutumika nguvu yake ya kimuundo na kuwasha ‘mashine zake
za kisiasa,’ kuanzia ngazi ya mtaa (ujumbe wa nyumba kumi) kwa nchi
nzima. Kimuundo, jumiya ya wanawake wa CCM (UWT) pekee ni kubwa kuliko
Chadema, chama kikuu cha upinzani. CCM Haihitaji kusafiri ili kufanya
kampeni. CCM ipo kila mahala, ikifanya kampeni katika makundi madogo,
vijijini na mitaani, kila siku na mbali ya upeo wa vyombo vya habari.
Kwa wanaofahamu muundo wa chama hicho, ushindi kwake si jambo la
kushangaza.
Kwenye miaka ya 1950s,
wakati wa harakati za kusaka uhuru kutoka kwa mkoloni, uwezo wa TANU
kuhamasisha ulikuwa nguzo muhimu kwa Tanganyika kupata uhuru wake.CCM
imerithi vinasaba vya TANU. Mwalimu Nyerere aliijenga CCM kuwa imara kwa
nyakati kama hizi. Mwaka jana, huku umaarufu wake ukiwa umepungua, CCM
ilimudu kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa kwa asilimia 80 dhidi ya
umoja Huohuo wa Upinzani inaokabilina nao katika uchaguzi huu
Mkuu.Tofauti haipo kwenye nini kinachoonekana kwenye vyombo vya habari
au mitandao ya kijamii bali jinsi gani makada wa chama hicho tawala
walivyofanya uhamasishaji katika kila mtaa na kijiji. Uchaguzi huo wa
serikali za mitaa, ambao hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu,
hutoa dalili nzuri kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu.
7. Umahiri wa Dkt Magufuli
Mwaka jana, baadhi ya
waandishi wa habari walikiri kwamba ni vigumu mno kumshambulia na
kumshinda Dkt Magufuli. Ana rekodi imara ya usafi, uchapakazi na
anayetaka kuona matokeo sahihi. Hajawahi kuvutiwa na harakati za
kisiasa, na ilikuwa mshangao alipotangaza kuwania urais. Na
alipotangaza, hakufanya mbwembwe wala kijitangaza kwenye vyombo vya
habari. Alizingatia kanuni za chama kwa ukamilifu. Dkt Magufuli analeta
kumbukumbu za mgombea mwingine aliyekuwa hajulikani mwaka 1995 -
Benjamin Mkapa. Wakati umaarufu wa CCM ukiwa chini, huku ikikabiliwa na
upinzani kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu aliyehama kutoka chama hicho
tawala, CCM ilimchagua turufu yake ambayo ilikuwa ngumu kuikabili.Miaka
20 baadaye, ikikabiliwa na upinzani wa Waziri Mkuu maarufu wa zamani
aliyehama chama hicho na kujiunga na Upinzani, CCM imefanya tena ‘vitu
vyake.’ Siku zote, CCM hujua ‘kufanya pigo la haja.’
8. Ufanisi wa CCM katika maeneo ya vijijini
Mimi ni Mbunge wa jimbo
lisilo mjini, lenye idadi ya wastani ya wapigakura. Mwaka 2010, katika
uchaguzi ulionekana kuwa mgumu, CCM ilishinda jimbo langu kwa asilimia
80., na kitaifa kwa asilimia 61. Hivi sasa, tunatarajia ushindi wa CCM
kuwa wa asilimia 90 hivi. Tanzania ina majimbo kadhaa yaliyo kama jimbo
langu. Upinzani hupenda kuwapuuza wananchi katika majimbo yasiyo ya
mijini, kama jimbo langu, kwa kudai kuwa wanaichagua CCM kutokana na
ujinga wao. Wasingeweza kukosea zaidi ya hivyo.
Popote walipo, watu hupiga
kura kulingana na mahitaji yao. Mwaka 2000, vijiji vinne tu katika jimbo
langu ndivyo vilikuwa na umeme. Leo, vijiji 44 vina umeme. Japo
hatujaweza kutoa huduma zote kwa kiwango cha kumfurahisha kila mtu,
lakini hali halisi yaonyesha wingi wa wanafunzi mashuleni, walimu zaidi,
madaktari na manesi zaidi, zahanati nyingi zaidi zimejengwa, huduma za
mawasiliano ya simu zinapatikana kwa wingi, barabara nyingi za lami, nk.
Porojo kuwa hakuna kilichofanyika Kwahiyo wapigakura wasiichague CCM
haieleweki katika maoneo hayo ambay kimsingi ndiyo yenye wapigakura
wengi. Na wagombea wa CCM wanaposema watafanya zaidi ya
waliyokwishafanya, kwa kuzingatia mafanikio yaliyokwishapatikana,
wananchi wanawaamini. Hotuba za kampeni ni mwonekano na mantiki.
Chaguzi sio kuhusu ahadi tu
bali jinsi gani ahadi hizo zitaandaliwa na kutekelezwa. Jukwaa ambalo
kila chama kitanadi ajenda zake za uchaguzi hujengwa wakati wa uzinduzi
wa kampeni za chama husika. Yahitaji mtu kuangalia tu uzinduzi wa
kampeni za za Lowassa na Magufuli. Lowassa aliongea kwa dakika 9 tu -
akiahidi, pamoja na mambo mengine, kuwaachia huru wabakaji (sio kama
ninazusha hili) wanaotumikia vifungo vyao na watuhumiwa ugaidi
wanaosubiri kesi zao. Bila kujali alikuwa na malengo gani wakati anatoa
ahadi hizo, makosa hayo hayastahili msamaha wa rais. Kwa upande wake,
Magufuli aliongea kwa dakika 58, akielezea kwa undani ajenda za
maendeleo katika nyanja za elimu, ajira, afya, ufisadi, huduma za maji,
na miundombinu. Kuanzia hapo, kwa muda wote wa kampeni, mwenendo umekuwa
hivyo, kwa uzito wa ujumbe kwenye hotuba zake na muda wa kuhutubia
Wanaohudhuria mikutano ya
Dkt Magufuli huondoka katika mikutano hiyo wakiwa na matumaini na wenye
nguvu. Kwa upande mwingine, wahudhuriaji katika mikutano ya Lowassa
huondoka wakiwa wamekanganywa. Siku ya kupiga kura, wapigakura
wanamkumbuka jinsi mgombea alivyoonekana na alivyoongea, na jinsi
walivyojisikia walipomwona jukwaani. Kwa kigezo hiki, ni bora ningekuwa
upande wa Magufuli.
9. Uongo, uongo na takwimu
Tanzania haina utamaduni wa
kura za maoni kupima nafasi za wagombea katika uchaguzi. Tuna utaratibu
wa muda mrefu wa kupata maoni ya wananchi katika maamuzi makubwa ya
kisera – kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa, marekebisho ya Katiba,
na kadhalika. Mwaka 2005, kulifanyika kura ya maoni, iliyobashiri
ushindi mkubwa kwa CCM. Na kwa hakika, CCM ilishinda kwa asilimia 80.
Mwaka 2010, kura ya maoni iliyoendeshwa na kampuni ya Ipsos-Synovate
iliashiria kuwa idadi ya kura za CCM ingepungua hadi kufikia asilimia
61. CCM ilipinga matokeo ya kura hiyo ya maoni ikidani kuwa yalikuwa
kiasi kidogo sana. Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa kama yalivyotabiriwa
katika kura hiyo ya maoni. CCM ilipata asilimia 61 ya kura zote.
Hivi karibuni, kura mbili za
maoni zilichapishwa. Zote zilifanywa na taasisi huru zinazoheshimika. –
Twaweza and Synovate-Ipsos tena- zote zikijihusisha na utafiti wa
kusaka maoni. Taasisi mbili tofauti, zilizotumia mbinu tofauti za
kufanya utafiti, katika nyakati tofauti, matokeo yaleyale. CCM itashinda
kwa asilimia 62 ya kura zote.
Inaruhusiwa, na kwa yumkini
ni jambo zuri, kupingana na sababu hizi tisa za kwanini CCM itashinda.
Lakini namba zina tabia ya ukandamizaji. Ndio mwelekeo wa kura huwezi
kubadilika. Lakini kwa kuzingatia yote yaliyokwishaongelewa kuhusu
kinachodaiwa kuwa ufuasi mkubwa kwa Upinzani, basi muda huu ingetarajiwa
tuwa tunajadiliana kuhusu ufuasi wa wengi kutoka Upinzani kuelekea CCM–
na sio kutarajiwa ufuasi wa wengi kutoka CCM kuelekea Upinzani. Na
ndiyo, kura za maoni zaweza kukosea, na tusiwekee mkazo sana.Lakini hoja
hii sasa ndiyo hupendelewa zaidi na upande unaelekea kushindwa kwenye
uchaguzi.
January Makamba ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, na msomaji wa Kampeni za CCM
Post a Comment