Mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza.
NA MWANDISHI WETU
MSHAMBULIAJI wa Simba, Hamis Kiiza, anatarajiwa kukabidhiwa zawadi
yake ya Sh milioni 1/-ya Mchezaji Bora wa Mwezi na wadhamini wakuu wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, kampuni ya mawasiliano ya Vodacom
Tanzania, baada ya kuibuka kidedea Septemba.
Kiiza
alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Septemba baada ya kufanya vema katika
mwezi wa kwanza wa ligi hiyo, akiisaidia timu yake ya Simba kushinda
mechi tatu mfululizo, huku Mganda huyo akifunga mabao matano, ikiwamo
‘hat-trick’ katika pambano dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu, Kiiza
atakabidhiwa kitita chake hicho na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,
Ian Ferrao, wakati wa mchezo wa Simba dhidi ya Majimaji Oktoba 31, mwaka
huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Alisema
kuwa kampuni yao itaendelea kutoa zawadi kwa wachezaji wanaofanya
vizuri kila mwezi, ikiwa ni sehemu ya mikakati na mchango wao katika
kuinua kiwango cha michezo, hususan soka nchini na kubadilisha maisha ya
wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu.
“Katika
kuendeleza mikakati yetu ya kuinua soka hapa nchini pamoja na kuboresha
maisha kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Vodacom Tanzania, itamjaza kiasi cha Sh milioni moja mshambuliaji wa
Simba, Hamis Kiiza kutokana na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa ligi
hiyo kwa Septemba msimu huu,” alisema Nkurlu.
Juu ya
tuzo hiyo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi,
ameishukuru na kuipongeza Vodacom Tanzania ubunifu huo wa kuwazawadia
wachezaji wanaofanya vizuri kwani kitendo hicho huchangia kuendeleza
vipaji na kuwahamasisha wachezaji kufanya vizuri zaidi na kuzisaidia
timu zao.
“TFF
tunaamini zawadi kama hizi zinazotolewa kwa Mchezaji Bora wa Mwezi,
zinaweza kuwa chachu kwa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu kujituma zaidi
kwa faida yao, klabu zao na soka la Tanzania kwa ujumla,” alisema.
Tangu tuzo
hiyo ianze kutolewa Septemba mwaka jana, ni Coastal Union pekee
iliyofanikiwa kutoa wachezaji wawili walioibuka kidedea hadi sasa.
Washindi wa tuzo hiyo tangu ianzishwe mwaka jana ni Antony
Matogolo wa Mbeya City (Septemba, 2014), Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’
(Azam FC, Oktoba), Rashid Mandawa (Kagera Sugar, Novemba), Joseph
Mahundi, Said Bahanunzi (Polisi Moro, Januari) na Godfrey Wambura
(Coastal Union, Februari), James Mwasote (Police, Machi) na Mrisho Ngassa (Yanga, Aprili).
Post a Comment