Mmoja
wa watu waliokuwa wamefunikwa na kifusi chini ya ardhi kwa siku 41,
juzi jioni alizinduka na muda mfupi baadaye akaulizia kama aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa ameshinda Uchaguzi
Mkuu.
Joseph
Bulule ni mmoja kati ya wachimbaji watano waliokuwa wamefukiwa na
kifusi kwenye machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama tangu Oktoba 5,
siku tatu baada ya Lowassa kurejesha fomu za kuwania urais kwa tiketi ya
Chadema.
Juhudi
za kuwaokoa wachimbaji hao zilifanyika lakini zikasitishwa baada ya
muda kutokana na kutokuwapo na dalili za mafanikio, kabla ya jitihada
hizo kuanza tena baada ya wachimbaji wengine kusikia sauti za wenzao
wakiomba msaada kutoka chini ardhi.
Bulule,
ambaye amelazwa Hospitali ya Halmashauri ya Kahama, aliuliza swali hiyo
mbele ya waandishi wa habari baada ya kupata fahamu.
“Nani
alishinda kwenye uchaguzi wa Rais,” aliuliza waandishi akiwa amelala
kitandani. “Lowassa alishinda? Maana sisi tangu Oktoba 5, tulipofukiwa
hatujui kinachoendelea. Uchaguzi umetukuta ndani ya mashimo na hatujui
matokeo ya uchaguzi.”
Uchaguzi
wa Rais na wabunge ulifanyika siku ishirini baadaye wakati juhudi za
kuwaokoa zikiwa zimeshasitishwa. Katika matokeo ya uchaguzi huo, mgombea
urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli alishinda kwa kupata kura
milioni 8.88, huku Lowassa, aliyekuwa anaungwa mkono na vyama vinne,
akishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07
Baada ya waandishi wa habari kumueleza kuwa aliyeshinda ni Dk Magufuli, mchimbaji madini huyo mdogo alionekana kukosa raha.
Kwa
mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Joseph Ngowi jana mchana
watu hao watano walianza kupatiwa chakula chepesi, kama uji wenye maji
mengi ambayo alisema yanasaidia utumbo kunyanyuka baada ya kukaa siku 41
bila kupata chakula.
Alisema
baada ya hatua hiyo wataanza kupewa chakula laini na baada ya siku saba
wataanzza kula chakula cha kawaida. Alisema wote watano wapo kwenye
usimamizi wa madaktari pamoja na wataalamu.
Wakiwa
kwenye mgodi Oktoba 5, kifusi kilikatika na kufunika mlango wa kutokea,
hali iliyofanya waishi siku 41 kwa kunywa maji, kula mende, vyura na
magamba ya miti hadi walipookolewa Jumapili iliyopita wakiwa hai.
Post a Comment