National Arts Council BASATA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ijumaa hii ya tarehe
06/11/2015 linatarajia kuyakutanisha mashirikisho na vyama vya wasanii
nchini kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es
Salaam ili kuweka mikakati ya pamoja katika kufanikisha siku ya msanii
maarufu kama Msanii Day inayotarajiwa kufanyika tarehe 12/12/2015.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Siku ya Msanii kutoka Kampuni
mwendeshaji wa siku ya Msanii (Msanii Day) Haakneel Production Tanzania
(LTD) Bw. Justine Kusaga lengo la kuwakutanisha wasanii ni kuwa na
mjadala wa pamoja ili kuhakikisha siku hii ya Msanii inafanyika kwa
mafanikio makubwa na kuwafanya wasanii wote kuwa sehemu ya siku hii
muhimu kwao.
“Haakneel kwa kushirikiana na BASATA ambao ni wamiliki wa mradi
huu wa siku ya msanii tumeamua kuwaita wasanii kupitia mashirikisho na
vyama vyao ili kuhakikisha kila msanii anakuwa sehemu ya maadhimisho ya
siku hii muhimu lakini pia kuifanya siku hii kuwa yenye mafanikio”
alisema Kusaga
Alizidi kueleza kwamba, mwaka huu siku ya msanii imepangwa kuwa
ya tofauti ambapo shamrashamra zake zimepangwa kuanza mapema zaidi kwa
kuhusisha shughuli na matukio mbalimbali ya kisanaa kabla ya kilele
ambacho kinatarajiwa kupambwa na burudani mbalimbali za Wasanii.
“Tunawaita wasanii Ijumaa hii ili kwa pamoja tujadiliane, tuweke
mikakati ya pamoja na kuhakikisha kunakuwa na shamrashamra nyingi za
wasanii ambazo zitawafanya waimiliki siku hii maana hakika siku hii ni
yao wasanii” alisisitiza Kusaga.
Siku ya Msanii maarufu kama Msanii Day ni mradi unaomilikiwa na
BASATA ambao lengo lake ni kuenzi, kuthamini na kutambua michango
mbalimbali ya wasanii nchini na kwa mara ya kwanza iliazimishwa tarehe
25 Oktoba mwaka jana wa 2014,
IMETOLEWA NA KITENDO CHA HABARI NA MAWASILIANO, BASATA
Post a Comment