Wakazi
wa mkoa wa Arusha wamesherehekea kwa namna mbalimbali kuapishwa kwa
Rais mpya wa Tanzania Dakta John Pombe Magufuli, ambapo huko Wilayani
Longido eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya, wafugaji wa jamii ya
kimaasai wamefanya maandamano ya amani kumpongeza kiongozi huyo.
Kituo
hiki kimefika katika maeneo mbalimbali ya Longido na kushuhudia
wananchi wakiwa wanafuatilia matangazo ya moja kwa moja yaliyokuwa
yakirushwa na vituo mbalimbali vya televisheni kutoka uwanja wa Taifa
Jijini Dar es Salaam katika zoezi la kumwapisha Dakta John Pombe
Magufuli.
Katika
maeneo mengine ya Mji wa Longido wakazi wake wengi wakiwa ni wa jamii
ya kimaasai wameshuhudiwa wakiwa katika maandamano ya amani huku wakiwa
wamebeba bendera za Chama cha Mapinduzi,katika kusherehekea kuapishwa
kwa Rais mpya wa Tanzania.
Baadhi
ya wale waliozungumza na kituo hiki akiwemo Joseph Ole Sadira,Ndeshi
Israel na Steven Kirushwa, wamesema CCM kimeonekana kuwa chama chenye
kuaminiwa na watanzania na kwamba shauku yao ni kuona Rais huyo wa awamu
ya Tano anatekeleza ahadi huku wakimtaka kuwatatulia changamoto kubwa
ya uhaba wa maji.
Longido
ni moja ya maeneo ya wafugaji yaliyo kaskazini mwa Tanzania ambapo
ukame umekuwa moja ya matatizo yanayolalamikiwa na wakazi wake huku
vyanzo vichache vya maji vikiwa vinagombaniwa baina ya watu na mifugo
ambayo ndiyo rasilimali inayotegemewa na wakazi wengi wa eneo hilo
Post a Comment