Rais
Magufuli ameonyesha kauli mbiu yake ya ‘HAPA KAZI TU’ ambayo haina
tofauti na ‘KUSEMA NA KUTENDA’ yake Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
iliyobadilishwa na wazalendo na kuwa ‘KUSEMA NA KUTEMA’ kutokana na kile
kinachorejelewa kama ‘uovu’ unaotekelezwa na serikali yake ikizingatiwa
kwamba zimwi la ufisadi limekuwa wimbo mitaani.
Uchapakazi
wa Magufuli ambaye ni Rais wa awamu ya tano wa taifa hilo, umetuma
ujumbe mzito kwa taifa la Kenya ambalo linakabiliwa na visa vingi vya
ufisadi kwenye serikali ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.
Katika
kipindi cha mwezi mmoja tangu alipotwaa madaraka, Magufuli amefanya
mabadiliko makubwa sana katika uongozi wa serikali aliyoikuta.
Awali
ya yote, Magufuli amepiga marufuku safari za nje za mawaziri na kutaka
mabalozi wa Tanzania kwenye nchi husika kuiwakilisha serikali yake huko.
Kwa hatua hiyo, Magufuli amefanikiwa kupunguza matumizi ya pesa za umma
kwa ajili ya safari na hela hizo kuelekezwa kufanya mambo mengine ya
kuisaidia jamii.
Rais
huyu wa awamu ya tano alipunguza bajeti ya awali ya Tsh250 milioni
iliyokuwa imetengewa sherehe zakupongezana kwa wabunge
walioshinda uchaguzi hadi kufikia Tsh15 milioni.
Fedha zilizobakia zilitumwa kuboresha mahitaji ya hospitali kuu ya kitaifa Muhimbili kwa kununu zaidi ya vitanda 300.
Hii
ilikuwa ni baada ya Rais huyo kufanya ziara ya kushtukiza hospitalini
humo ambapo aliwakuta wagonjwa wakilala chini kutokana na ukosefu wa
vitanda.
Aidha aliifuta bodi ya wakurugenzi wa hospitali hiyo kwa utendakazi duni akiwemo aliyekuwa daktari mkuu Dkt Hussein Kidanto.
Siku
chache zilizopita, Magufuli alipunguza ujumbe wa wajumbe 34 waliotakiwa
kusafiri nje ya nchi kuiwakilisha Tanzania kwenye kongamano muhimu la
kimaendeleo hadi kufikia watu wanne.
Hatua yaokoa donge nono
Hatua hiyo iliokoa Tsh700 milioni ambazo zingetumiwa na wajumbe hao kugharamia safari hiyo.
Jumatatu
wiki hii, Magufuli alitangaza kuondoa sherehe za maadhimisho ya siku ya
Uhuru inayosherehekewa Desemba 9, na kutaka fedha kwenye bajeti hiyo ya
Wakati Wa sherehe hiyo zitumike kwa mambo mengine muhimu.
Haya
yakiwa tu ndio baadhi ya vitu alivyovifanya, Wakenya wamepagawishwa
naye na kumpelekea kuwa gumzo mitandaoni na kuonekana ‘Top in Town’:
@Fifi: Uhuru Kenyatta anahitaji kujifunza mawili matatu kutoka kwa mwenzake wa Tanzania Magufuli.
@Shadie:
Yaani aliyofanya Magufuli ofisini chini ya mwezi mmoja tangu aingie
madarakani, yanazidi aliyofanya Uhuru kwa muda wa miaka miwli na nusu
tangu awe ofisini.
@MafisiPope:
Wakati Magufuli akiwa kwenye hali za kuchapa kazi kwa vitendo wakati
ndio siku yake ya pili ofisini, kwa Uhuru imepita miaka mitatu lakini
bado yupo ‘bizi’ akiunda kamati akitaka zimweleze cha kufanya.
@Collins Fabien: Rais Uhuru amekuwa akipiga domo tangu 2013 wakati Rais Magufuli amekuwa akichapa kazi kwa wiki tatu sasa.
@Muthui: Wakati Watanzania wakiamka kuyakuta makubwa aliyoyafanya Magufuli, Wakenye tunaamka kuyakuta yale aliyoahidi Uhuru.
Haya yakiwa ni baadhi tu ya maoni ya Wakenya kipindi hiki serikali ya Jubilee inakumbwa na kashfa za kila aina za ufisadi.
Post a Comment