Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Nuru
inapoiangazia dunia, huwaangazia viumbe vyote vilivyo hai na visivyo na
uhai, viumbe vyenye uhai, hao hufurahia nuru hiyo kwa kuruka ruka na
kucheza kufurahia nuru hiyo.
Kila
ifikapo asubuhi na mapema, utasikia sauti na milio ya ndege wa angani,
wanyama wa kufuga na waishio mwituni, milio na sauti za viumbe hao
wakati mwingine kuashiria kuwa kumekucha ili waendelee kufurahia nuru
inayowanaagazia kwa manufaa ya maisha yao.
Wanadamu
nao wakiwa kama viumbe hai wengine, huanza kujiandaa asubuhi na mapema
kuelekea huku na kule kutafuta riziki ya kila siku ili maisha yao
yaendelee kusonga mbele baada ya nuru kuwangazia.
Mwandishi
wa makala haya anaifananisha nuru hiyo inayoiangazia dunia na Amani.
Amani ni tunu adhimu, ni tunu yenye Baraka na fanaka, amani
inapotamalaki duniani, binadamu na kila kiumbe chenye uhai huonesha
furaha yake kwa namna kiumbe hicho kinavyoguswa na amani hiyo.
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria Na.15 ibara 3
ya 1984 nayo inajali na kuzingatia amani hiyo ndiyo maana inatamka kuwa
“Sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa
dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru,
haki, udugu na amani”.
Katika
maisha ya kawaida ya kijamii amani ni ile hali ya raha na usalama bila
ugomvi wowote ambapo kinyume chake ni fujo au vita.
Ndiyo
maana Rais wa Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete aliwahi kusema “Amani yetu tuitunze kwa
nguvu zote, maana haina mbadala wake, mbadala wa amani ni vita, mbadala
wa upendo ni chuki, mbadala wa umoja ni mfarakano, amani siyo mboga
ambayo utaitafuta kiurahisi”
Kwa
umuhimu huo, kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine duniani
kuadhimisha siku ya amani kila ifikapo Septemba 21, ambapo mahitaji ya
matumaini ya amani yameonekana kuwa mbali katika dunia ya sasa
iliyokumbwa na mizozo na mapigano.
Katika
kuadhimisha siku hiyo mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa (UN)
Ban Ki- moon alitoa ujumbe wa siku hiyo ya amani duniani ambapo alisema
kuwa hakuna kundi linaloweza kufanikisha kufikia ndoto ya amani zaidi ya
vijana ambao alisema kwa sasa ni wengi.
“Viongozi
hawana budi kuwekeza kwa vijana katika ujenzi wa amani, Aidha alisema
sote tunaweza kuimarisha amani, Mashirika ya kiraia, kampuni na hata
taasisi za kidini wote wanaweza kujenga dunia yenye amani zaidi”alisema
Katibu Mkuu huyo wa UN.
Aliendela
kusema kuwa ubia huo katika ujenzi wa amani ndio msingi wa ujumbe wa
siku ya amani mwaka huu unaongozwa na na kauli ya mbiu isemayo “Ubia kwa
amani utu kwa wote”.
Vijana
ni nguzo imara ambayo inayoweza kujenga amani ya dunia ya leo, kuwekeza
kwa vijana ni kupanda mbegu inayoota na kusitawi ikipandwa kwa muda
mwafaka na kupata mahitaji yake kwa wakati ikiwemo maadili mema na
wazazi, walezi, jumuiya, taasisi, na taifa kwa ujumla.
Tanzania
ikiwa sehemu ya dunia hii, haiwezi kujitenga na suala la amani siku
zote kwa wakati wote miongoni mwa wananchi wake na hata mataifa mengine.
Kwa
mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini 2012, watu milioni
19.7 sawa na asilimia 44 ya watu wote nchini ni watoto wenye umri
chini ya miaka 15, vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 wakiwa milioni 15.6
sawa na asilimia 35.
Mchanganuo
huo unaashiria kuwa kundi la vijana kati ya miaka 18-35 lina watu
milioni 11.8 sawa na asilimia 26, ambalo linakuwa na umuhimu wa kipekee
nchini kisiasa na kiuchumi.
Kama
nchi, Tanzania imeendelea kuwa ya mfano bora miongoni mwa mataifa ambapo
zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu nchini la kumchagua Rais, Wabunge
na Madiwani umekamilika kwa amani na utulivu wakati wote tangu kuanza
kwa michakato ya kuwapata wawakilishi wa vyama katika nafasi hizo,
wakati wa kampeni ambapo wagombea wa nafasi mbalimbali walinadi sera za
vyama vyao ili waweze kupewa ridhaa ya kuongoza katika nafasi zao kwa
miaka mitano.
Zoezi
la uchaguzi limekamilika ambapo Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
amechaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Makamu wake Samia Suluhu Hassan ambao
walitangazwa washindi na kupewa Hati ya Ushindi huo na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) mnamo Oktoba 30, 2015 mbele ya viongozi wa Serikali,
vyama vya siasa, waangalizi wa Kimataifa, Mabalozi wanaowakilisha nchi
zao hapa Tanzania, waangalizi wa ndani ya nchi na wananchi kwa ujumla.
Zoezi
la kuwapata viongozi lilifanyika kwa amani ambapo hata hali ya hewa
ilikuwa ya kufurahisha na kuipamba siku hiyo kwa kuwa na mvua ilinyesha
ambayo ni kielelezo cha amani ambayo hufurahiwa na viumbe vyote.
Kuonesha
umhimu wa amani nchini, kila kiongozi na wananchi kwa nafasi zao
wanaendelea kusisitiza amani, Mkuu wa Jeshi la Polisi Ernest Mangu kwa
nafasi yake kama mkuu wa ulinzi na usalama kwa raia na mali zao wakati
wote husisitiza na kuwahimiza Watanzania kwa ujumla kwa kuwasihi
wadumishe amani na utulivu kama ilivyokuwepo wakati wote wa kampeni za
uchaguzi mkuu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo Oktoba 25 mwaka
huu.
Katika
kudumisha amani nchini, kila mtu anajukumu la kutimiza ili kuimarisha
amani kama ilivyojengwa na kuimarishwa na viongozi wa Serikali kwa Awamu
zote tangu kupatikana kwa uhuru Disemba 9, mwaka 1961 na kuwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964.
Awamu
hizo za uongozi ni ile ya kwanza ilioongozwa na Muasisi wa taifa hili
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Awamu ya Pili ya Alhaji
Alli Hassan Mwinyi, Benjamini William Mkapa Awamu ya Tatu, Dkt. Jakaya
Kikwete Awamu ya Nne.
Uongozi
wa Serikali ya Awamu ya Tano nchini ambao uliyoingia madarakani rasmi
Novemba 5, 2015, umepewa dhamana ya kuliongoza taifa hili wakati suala
la amani ni la muhimu kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla wao kwa
kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025.
Dira
hiyo ya Maendeleo Tanzania ilianza mwaka 1994 na hatimaye serikali
ilizindua rasmi dira hiyo, mwaka 1999 nchini kwa lengo la kuhamasisha
maendeleo endelevu yenye tija kwa jamii.
Msingi
wa Dira ya 2025 nchini ni kuhimiza Watanzania kuwa ifikapo 2025,
Tanzania iwe imepitia katika mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo
ili kufikia kipato cha kati, ikiwa na viwango vya juu vya viwanda,
ushindani, maisha bora, utawala wa sheria na kuwa na jamii iliyoelimika
na inayopenda kusoma waweze kujipatia maendeleo yao wenyewe kwa kutumia
mazingira yao.
Kimsingi,
Dira ya maendeleo nchini imeeleza matarajio ya kijamii, kiuchumi na
kisiasa nchini ambapo katika robo ya kwanza ya karne ya 21 lengo lake ni
Watanzania kufikia hali ya kipato cha kati.
Malengo
hayo yanaweza kufikiwa ili kuifanya nchi iweze kuingia katika soko la
ushidani kwa kusimamiwa na kuongozwa na amani iliyojengwa katika misingi
imara ya utaifa kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria, kanuni na
taratibu ambazo kila mdau wa maendeleo na mpenda amani anapaswa
kuzingatia.
Wakati
Umoja wa Mataifa unasisitiza kwa kauli mbiu yake ya amani mwaka 2015,
inayosema “Ubia kwa amani utu kwa wote”, kauli mbiu hiyo ni muhimu kwa
musatakabali wa taifa hili ndiyo maana wimbo wa kujenga na kudumisha
uzalendo wa Tanzania unahamasisha watu kuipenda nchi kwa moyo wote.
“Nchi
yangu Tanzania, Jina lako ni tamu sana, Nilalapo nakuota wewe, Niamkapo
ni heri mama wee, Ninapokwenda safarini, Kutazama maajabu, Biashara nayo
makazi, Sitaweza kusahau mimi, mambo mema ya kwetu kabisa, Watu wengi
wanakusifu, Siasa yako na desturi, Ilikuletea uhuru, Hatuwezi kusahau
sisi, Mambo mema ya kwetu hakika, Tanzania, Tanzania, Nakupenda kwa moyo
wote”.
Wimbo
huo wa uzalendo kwa taifa umeudhihirishia umma wa Watanzania, Afrika na
ulimwengu kwa ujumla kuwa Watanzania wanaipenda nchi yao kwa kutunza
heshima ya taifa na ndiyo maana watu wengi wanaisifu Tanzania kwa siasa
na desturi yake imara wakati wa kupata viongozi wapya kwa amani.
Miongoni
wa waangalizi wa kimataifa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2015 ni
shirika lisilo la kiserikali la nchini Afrika ya Kusini la “Afican
Policing Oversight Forum” ambalo lilikuwa na waangalizi wawili Sean M.
Tait na Eric W. Pelser, nao walitoa maoni yao kwa kusema jukumu lao
lilikuwa kuangalia utendaji wa Jeshi la Polisi na namna lilivyofanya
kazi wakati wote wa uchaguzi.
Waangalizi
hao walisema wameridhishwa na utendaji wa polisi nchini na kusema kuwa
kila kituo cha kupigia kura, wapiga kura walipiga kura kwa amani na
walikuwa huru katika zoezi la upigaji kura, polisi kwa nafasi yao,
walifanya kazi yao bila kuwabughudhi wapiga kura wakizingatia kanuni zao
za kazi.
Naye
Balozi wa Norway nchini, Mhe. Hanna-Marie Kaarstad alisema kuwa Tanzania
ni nchi ya kuigwa na mataifa mengi duniani jinsi inavyoendesha uchaguzi
na kuwapata viongozi wake kwa amani.
“Uchaguzi
umefanyika kwa amani, wapiga kura wamefuata mistari bila bughudha
yeyote katika maeneo yote, kuanzia kwa wazee, akina mama, wanawake kwa
wanaume na vijana, hili ni suala jema la kuigwa” alisema Balozi Hanna.
Hayo
ni matunda mema ya Tanzania ambayo hata wimbo wake wa taifa umekuwa sala
ya Watanzania kila wanapokuwa katika tukioa la kitaifa au mikusanyiko
rasmi ambapo wimbo huo huimbwa ili kuliweka taifa mikononi mwa Mungu kwa
kuwaombea baraka viongozi wake, Hekima, Umoja na Amani kwa watu wake
wote, wake kwa waume na watoto ili taifa liweze kudumisha Uhuru na Umoja
kwa watu wake kwa maslahi ya taifa.
Kila
mdau wa amani amekuwa mstari wa mbele katika kuilinda amani nchini,
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mmoja wa wadau hao wa amani
ambapo wao walianzisha kampeni ya kuhamasisha amani kwa kipindi chote
cha maandalizi ya uchaguzi na wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi
iliyopewa jina la “AMANI YETU FAHARI YETU” na kuongozwa na Mabalozi wake
wa amani katika kampeni hiyo ambao ni wasanii Mrisho Mpoto (maarufu
kama Mjomba) na Christina Shusho.
Kampeni
hiyo ilikuwa na lengo la kuhamasisha Watanzania wabaki na Amani wakati
kampeni za Uchaguzi Mkuu, siku ya kupiga kura ambayo ndiyo siku ya
uchaguzi wenyewe na baada ya uchaguzi ambapo suala la amani lilihimizwa
kwa kuzingatia kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.
Kampeni
ilihamasisha Watanzania kutambua kwamba utofauti wa itikadi wa vyama
ndio ukomavu wa demokrasia nchini hali ambayo Rais wa Awamu ya Tano mara
baada ya kuapishwa wakati akiwashukuru Watanzania na wananchi kwa
ujumla pamoja na wageni waliofika kwenye sherehe hiyo aliwasihi
washindani wake watambue kuwa nchi ni kubwa kuliko vyama, hivyo hakuna
sababu ya kuendelea kukuza malumbano ambayo hayawezi kusadia nchi na
wananchi.
Wananchi
walivumiliana na walifanya siasa za kistaarabu na walitambua kuwa kuna
maisha baada ya uchaguzi, hivyo kipindi chote cha uchaguzi watanzania
walibaki imara na kuitunza Amani ya nchi ambayo imeendelea kuwa tunu
iliyotukuka ndani na nje ya Tanzania.
Ni
dhahiri madhara yatokanayo na vurugu ambayo siyo tunda la amani kwa
jamii yanaweza kuwa na athari mbalimbali ikiwemo ulemavu, vifo,
ukimbizi, njaa na maradhi mengine ya kisaikolojia kwa watu wasio na
hatia wakiwemo wanawake, wazee na watoto.
Ili
kuhakikisha amani inaendelea kuimarika nchini, Kampuni ya Msama
Promotions Limited ya Dar es Salaam iliandaa tamasha la amani kuombea
Uchaguzi Mkuuu nchini ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais Dkt. Jakaya
Kikwete (kwa sasa Mstaafu) kwa nia ya kuendelea kuwakumbusha na
kuwahimiza Watanzania umuhimu wa kudumisha amani wakati uchaguzi huo
ikizingatiwa kuwa baada ya uchaguzi, Tanzania itabaki na maisha
yanapaswa kuendelea.
Ni
jukumu la kila mtu kwa nafasi yake kutetea na kudumisha umoja, upendo na
mshikamano wa kitaifa. Amani na utulivu ni jina jipya la maendeleo
endelevu ya binadamu maana bila amani hakuna maendeleo. Kila mwananchi
apanie kusimamia misingi ya haki na amani, ili waweze kufurahia maisha
kwa kujipatia maendeleo.
Rais
Dkt. Magufuli aliwashukuru watangulizi wake Marais Wastaafu Julius
Kambarage Nyerere, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa, Dkt.
Jakaya Kikwete na wageni mbalimbali waalikwa alisema “Napenda kutumia
nafasi hii kutoa shukrani zangu kwa kupata nafasi ya kuwa Rais, lakini
nawahakikishia nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote na nipotayari
kushirikiana na washindani wangu kujenga nchi ambayo ina maendeleo na
amani”.
Serikali
ya Awamu ya Tano imeingia madarakani ambapo kielelezo cha amani
kinaendelea kujitokeza kila mara ikizingatiwa wakati Dkt. Magufuli
alipokuwa na tukio kubwa la kitaifa na mihadhara yake ilipambwa kwa
kunyesha mvua.
Kunyesha
kwa mvua kila mara kumeonesha uhai ikizingatiwa mvua hizo zilinyesha
akiwa nahitimisha kampeni Oktoba 24, 2015 mkoani Mwanza katika wilaya ya
Ukerewe ambapo hata Mtangulizi wake Dkt. Jakaya Kikwete alishindwa
kwenda kuhutubia visiwa hivyo kwa kuwa mvua kubwa ilinyesha na
kuahirisha safari hiyo.
Vivyo
hivyo mvua ilinyesha wakati wa kupokea Hati ya Ushindi Oktoba 30, 2015
iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wakati wa kuapishwa
kwa viongozi hao wapya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Makamu
wake Samia Suluhu Hassan Novemba 5 mwaka huu.
Kwa
maneno ya wahenga wetu, kuna usemi unaosema kuwa mvua ikinyesha wakati
wa tukio muhimu linafanyika kama ilivyokuwa Novemba 5, mwaka huu,
mhusika wa tukio hilo “anakichwa kizuri” maana yake ni mtu mwenye bahati
nzuri siku zote za maisha yake na dalili yake kubwa ni amani ambayo
katika ulimwengu wa leo amani ni tunu muhimu katika kuwaletea maendeleo
wananchi.
Nao
viongozi wa dini waliowakilisha dini zao wakati wa sherehe za kuapishwa
Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano wa Jamhuri Muungano wa Tanzania na
Makamu wake, viongozi hao waliongoza sala maalum na kuwaombea baraka
viongozi wapya walioko madarakani ili waweze kuiongoza nchi katika
misingi ya haki na amani.
Viongozi
hao walikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Malasusa pamoja na Mufti wa
Tanzania Abubakar Zuber ambao waliwaombea viongozi wa Serikali ya Awamu
ya Tano waongoze taifa kwa haki na amani wakimtegemea Mungu katika
utendaji wao wa kazi.
Tanzania
imeendelea kutoa hamasa kwa nchi za Afrika na dunia nzima, kwa kitendo
chake cha kubadilishana madaraka kwa amani, hatua hiyo kubadilishana
madaraka imeendelea kuwa ni ya kiungwana na kwa namna ya pekee nchi
nyingi zinapaswa kuiga mfano huo mwema wa Tanzania.
Salamu
zilizotumwa na viongozi mbalimbali Afrika na duniani kote za kumpongeza
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Makamu wake Samia Hassan Suluhu kwa
kushika nyadhifa hizo za juu kitaifa ni ishara kuwa mataifa hayo
yanaunga mkono kitendo cha Tanzania cha viongozi wake kuachiana madaraka
kwa amani.
Ndiyo
maana viongozi wa mataifa jirani waliamua kuja kushudia na kujionea
demokrasia ya kweli ilivyoshika mkondo wake ambapo amani inaheshimiwa na
kutunzwa Tanzania kwa viongozi wake kuachiana madaraka hadharani na
kushudiwa na wanachi ndani na nje ya kupitia njia mbalimbali za
mawasiliano ikiwemo simu, radio, mitandao ya kijamii, TV na magazeti.
Baadhi
ya viongozi hao ni pamoja na Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Uhuru
Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda, Robert Mugabe wa Zimbabwe,
Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Fillipe Nyusi wa Msumbiji, Joseph Kabila
wa DRC na Edger Lungu wa Zambia.
Wengine
ni kutoka Falme za Kiarabu, Waziri wa Utalii Oman, Mkamu Mwenyekiti wa
Chama Tawala cha China Ziang Piang, Mwakilishi kutoka Saudi Arabia na
viongozi wengine waliowakilisha nchi mbalimbali wakiwemo Mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini nao walishiriki katika sherehe
kuapishwa na kuingia madarakani Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.
Magufuli kwa awamu ya kwanza ya miaka mitao hadi 2020.
Mwandishi
wa makala haya anaungana na maandiko matakatifu ambayo yanakiri,
kutambua na kulilipa suala la amani kipaumbele ambapo tunasoma ushuhuda
wa Yesu alipowaambia wanafunzi wake “Amani yangu nawapa” Yohana 14:27
Kwa
Tanzania, amani ni zawadi yenye thamani inayolinganishwa na hali ambayo
kiongozi wa Ukristo (Yesu) aliwaambia wafuasi wake siku ya mwisho
alipokuwa pamoja nao ambapo hakuwapa amani tu bali aliwapa amani yake
mwenyewe.
Watanzania
ni jukumu letu wote kuweka mkazo katika maisha ya siasa shirikishi,
kujenga imani miongoni mwa jamii, amani, uaminifu na kuimarisha taasisi
zinazo unga mkono suala la amani na demokrasia nchini ikiwemo taasisi za
elimu ya juu na asasi za kiraia.
Tanzania
ikiwa miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki inaguswa kwa
namna ya pekee na suala la amani, ndiyo maana inaungana na nchi
washirika kuimba wimbo wa jumuiya hiyo unaotaka tuilinde, tuwajibike,
tuimarike na kuishi kwa amani ili kutimiza na malengo tuliyojiwekea kama
jumiya yakiongozwa na uzalendo ili kulinda Uhuru, Amani, Mila na
desturi zetu.
Amani
ni ngao yetu sote, uchaguzi wa mwaka huu umekuwa wa amani, shirikishi na
wenye uwazi pamoja na kuimarisha demokrasia ya vyama vingi ambavyo kwa
ujumla wao vitaendelea kuhakikisha historia ya kujivunia ya Tanzania ya
kiuongozi, kikanda, barani Afrika na duniani inaendelea kukua na
kuimarika sanjari na kuboresha maendeleo ya Watanzania kwa ujumla wao
kwa kuzingatia kauli mbiu ya Rais Dkt. Magufuli ya “Hapa Kazi Tu” katika
kuinua sekta za elimu, maji viwanda, afya, miundo mbini ya barabara,
umeme, kilimo, uvuvi, mifugo na biashara.
Hayo
yote yanawezekana ikiwa Watanzania tutaendelea kuungana kwa pamoja kwa
umoja wetu kuilinda, kuidumisha na kuijenga amani yetu, “Mungu ibariki
amani yetu iendelee kutawala, Mungu ibariki Tanzania”.
Post a Comment