*Sura mpya zatajwa kuingia Baraza jipya
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ZIKIWA zimetimia siku sita tangu Rais Dk. John Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wingu zito limetanda kuhusu uteuzi wa Baraza la Mawaziri.
Wakati kitendawili cha kwanza kinatarajiwa kuteguliwa Novemba 19 mjini Dodoma, pale Bunge la 11 litakaporidhia uteuzi wa waziri mkuu anayesubiriwa kwa hamu, mtihani mwingine unabaki kwa mawaziri.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya matokeo ya ubunge kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umebaini kuwa wabunge wengi wanapungukiwa sifa za kuweza kutumikia nafasi za uwaziri.
Hali hiyo inachagizwa na Bunge la sasa kuingiza vijana wengi zaidi tofauti na vipindi vilivyopita, ambao wengi wao wanatajwa kukosa sifa na uzoefu katika suala zima la uongozi.
Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza wazi kuwa waziri mkuu anapaswa kuwa mbunge wa kuchaguliwa.
“Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne baada ya kushika madaraka yake, rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni,”.
Changamoto nyingine iliyo wazi ni upatikanaji wa mawaziri ambao wataendana na kasi ya utendaji kazi wa Dk. Magufuli, ambaye tayari ameanza kuwathibitishia Watanzania kuwa amedhamiria kuleta mabadiliko ya kweli katika utendaji kazi serikalini.
Taarifa zaidi kutoka kwa watu walio karibu na Ikulu, zinasema kuwa Dk. Magufuli anakusudia kuingiza sura mpya katika Serikali ya awamu ya tano, ili kukidhi kiu ya wananchi wanaotaka kuona mabadiliko katika uongozi wa nchi.
Katika kusuka serikali mpya yenye nguvu na mtazamo mpya unaoendana na kasi ya mabadiliko, mawaziri waliokuwapo katika serikali ya awamu ya nne kwa sehemu kubwa huwenda wasiteuliwe.
Akizungumza na MTANZANIA, mchambuzi mmoja wa masuala ya siasa (jina tunalihifadhi), alisema; “Wakati wote wa kampeni watu walikuwa wakiimba wimbo wa mabadiliko, hili lilichangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi kuchoka kuongozwa na watu wale wale miaka nenda rudi.
“Kuna watu nchi hii unaweza ukadhani wana ubia na uwaziri, kila siku wamo serikalini, mabaraza ya mawaziri yamevunjwa mara kadhaa, lakini bado wanarudi tu.
“Ukiangalia hata utendaji wao wa kazi hauridhishi, watu kama hawa wananchi wamewachoka na hata wao wenyewe wamechoka kiutendaji, yamebaki mazoea.
“Ndio sababu tumeshuhudia wanasiasa maarufu na wakongwe wakianguka majimboni, hizi ni salamu tosha kwa Rais Magufuli, wakati umefika sasa ajaribu watu wengine,”
Taarifa zimesema kuwa ukiacha nafasi ya waziri mkuu, miongoni mwa wizara nyeti ambazo zinampa Rais Magufuli changamoto kuteua watu wa kuziongoza ni pamoja na Wizara za Fedha, Nishati na Madini, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii, Mambo ya Nje na Mambo ya Ndani ya Nchi.
Tayari baadhi ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao walikuwa mawaziri katika Serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, wamekuwa wakitajwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari wakihusishwa na uteuzi wa waziri mkuu.
Miongoni mwao na majimbo yao katika mabano ni pamoja Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini), William Lukuvi (Isimani), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela) na January Makamba (Bumbuli).
Baadhi ya wadau wa siasa wameonya kuwa ni hatari kuteua waziri mkuu ambaye ana matamanio ya kuwa rais mbele ya safari, kwa sababu anaweza kutumia mwanya huo kujenga mtandao badala ya kuwatumikia wananchi.
Pia wamesema moja ya sifa zilizosababisha mamilioni ya wapiga kura kumpa kura ya ndio Dk. Magufuli, ni sifa yake ya uadilifu na uchapakazi, hivyo kuteua waziri mvivu, asiyekuwa na sifa hizo au mwenye kashfa za ufisadi wa aina yoyote, itakuwa dosari kubwa kwa Serikali yake (mwanzo mbya).
Lakini pia taarifa zaidi zimedai kuwa Rais Magufuli anaweza akawashangaza na kuwafurahisha Watanzania kwa kumteua mtu mpya kabisa katika duru za uongozi wa kisiasa kuwa waziri mkuu tofauti na hawa wanaotajwa, ili kukidhi kiu ya wananchi kutaka mabadiliko ya kweli.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais ana mamlaka ya kuteua wabunge 10, karata ambayo inatajwa kuweza kutumiwa na Rais Magufuli kuteua watu makini anaoona wanafaa kujaza baadhi ya nafasi za uwaziri.
Chanzo kingine cha habari kililieleza gazeti hili kuwa, katika kuhakikisha anateua mawaziri makini wenye sifa, Rais Magufuli anaweza kuteua mawaziri bila kuzingatia kanda kama ambavyo imezoeleka.
“Hili suala la kuteua mawaziri kwa kubalance (uwiyano) kanda kwamba kila upande wa nchi upate waziri anaweza asilizingatie, kwanza suala hili halipo kisheria huwa linafanyika kwa mazoea tu.
“Lakini mazoe hayo hayo ndiyo yanatuumiza kama taifa, leo hii rais analazimika kuteua waziri au naibu asiyekuwa na uwezo kabisa eti kwa sababu tu ya kubalance kanda (uwiyano).
“Watanzania wanaimani kubwa na Rais Magufuli na wanatarajia mabadiliko makubwa, waziri katika serikali hii ni sifa, uadilifu, uwezo wa kazi. Mwenyewe kasema kwake ni kazi tu, nchi hii inatakiwa isonge mbele,” kilisema chanzo hicho.
Wanaopewa nafasi ya kuingia
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya wabunge ambao wanapewa nafasi ya kuingia katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya tano ni pamoja na Mbunge wa Ngorongoro, William Tate ole Nasha huku kwa wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaotajwa ni Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile na Mbunge wa Segerea, Bonna Kaluwa.
Kwa upande wa Mkoa wa Dodoma wanatajwa ni Mbunge wa Kibakwe na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, George Simbachawene, Mbunge wa Kondoa Vijijini, Dk. Ashatu Kijaji na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.
Mbali na hao pia Baraza hilo la Mawaziri huenda likawajumuisha wabunge wa Mkoa wa Geita, akiwamo Dk. Medard Kalemani (Chato) na Dotto Biteko (Bukombe) na kwa Mkoa wa Iringa ni William Lukuvi (Isimani), Cosato Chumi (Mafinga Mjini) na Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini).
Mkoa wa Kagera ni Dk. Diodorus Kamala (Nkenge) na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) ambao wote kwa nyakati tofauti walikuwa katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Wengine wanaotajwa ni Hasna Mwilima (Uvinza) na Atashasta Nditye (Muhambwe) kutoka Mkoa wa Kigoma huku Profesa Jumanne Maghembe (Mwanga) na Dk. Mathayo David Mathayo (Same Magharibi) kutoka Mkoa wa Kilimanjaro.
Kutokana na vuta nikute ya kuunda Baraza la Mawaziri Dk. Magufuli huenda akawateua wabunge wa Mkoa wa Lindi ambao ni Majaliwa Kassim (Ruangwa), Hasan Masala (Nachingwea), ambapo Mkoa wa Manyara wanaotajwa ni Dk. Mary Nagu (Hanang’).
Mkoa wa Mbeya wanaotajwa ni Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Janeth Mbene (Ileje) na kwa upande wa Mkoa wa Morogoro ni Prosper Mbena (Morogoro Kusini Mashariki) na Dk. Hadji Mponda (Malinyi).
Mkoa wa Mtwara wanaotajwa ni George Mkuchika (Newala). Mkoa wa Mwanza wanaotajwa ni Charles Kitwanga (Misungwi), Angelina Mabula (Ilemela) na Dk. Charles Tizeba (Buchosa). Mkoa wa Njombe ni Gerson Lwenge (Wanging’ombe).
Mkoa wa Pwani ni Ridhiwani Kikwete (Chalinze) na Dk. Shukuru Kawambwa (Bagamoyo). Kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma wanaotajwa ni Ramo Makani (Tunduru Kaskazini), Joseph Mhagama (Madaba) pamona na Jenister Mhagama (Peramiho).
Chanzo hicho kilisema wabunge wa Mkoa wa Singida wanaoepewa nafasi kuingia katika Baraza la Mawaziri ni Mwigulu Nchemba (Iramba) na Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini), Mkoa wa Simiyu wanaopewa nafasi ni Luhanga Mpina (Kisesa).
Mkoa wa Mara wanaotajwa ni Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini) na Kangi Lugora (Mwibara).
Mkoa wa Shinyanga wanatajwa ni Steven Masele (Shinyanga Mjini), huku Mkoa wa Tabora wanaotajwa ni Dk. Hamisi Kigwangala (Nzega Vijijini), Hussein Bashe (Nzega Mjini), Margareth Sitta (Urambo) na Dk. Dalaly Kafumu (Igunga).
“Unajua mkuu hatakiwa mchezo kabisa katika kazi lakini bado hivi sasa kwa Mkoa wa Tanga wabunge ambao wanatajwa ni January Makamba (Bumbuli), Adadi Rajabu (Muheza) na Danstan Kitandula (Mkinga),” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mkoa wa Katavi wanaotajwa ni Dk. Pudenciana Kikwembe (Kavuu) na Moshi Kakoso (Mpanda Vijijini), huku kwa upande wa Mkoa wa Rukwa anayetajwa ni Josephat Kandege (Kalambo).
MTANZANIA
Post a Comment