Rais
John Magufuli anatarajiwa, wakati wowote kuanzia sasa, kuwateua baadhi
ya watu wenye sifa kuwa wabunge ili aweze kuwapa majukumu ya kuongoza
wizara atakapopanga safu ya Baraza la Mawaziri, hivi karibuni.
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inampa Rais mamlaka ya
kuteua wabunge wasiozidi 10 kutoka miongoni mwa wananchi ambao anaona
wanaweza kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake katika baadhi ya
maeneo kama vile afya, elimu, kilimo, nishati na sheria.
Ibara
ya 66 (1) inasema, bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii,
kutakuwa na aina zifuatazo za wabunge, yaani (e) wabunge wasiozidi 10
walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa kwa mujibu wa
ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya 67(1) (b).
Baraza
hilo jipya linatarajiwa kuwa na sura nyingi mpya ambazo zitaendana na
kasi yake kutekeleza kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu.” Pia, baraza litakuwa
na sura mpya kutokana na ukweli kwamba baadhi ya mawaziri waliangushwa
kwenye kura za maoni, wengine wakati wa Uchaguzi Mkuu na wengine,
japokuwa wamerejea bungeni ni walionekana kuwa mzigo awamu iliyopita.
Kati
ya mawaziri 55 waliokuwamo katika Baraza lililopita, waliorejea katika
Bunge la 11 ni 23 tu wakiwamo 20 wa majimbo na watatu wa viti maalumu.
Kupungua kwa idadi hiyo kutampa Dk Magufuli fursa ya kusuka baraza hilo
kutoka miongoni mwa wabunge 188 wa majimbo, 64 wa viti maalumu na 10
atakaowateua ili wamsaidie.
Haijulikani
baraza litakuwa na mawaziri wangapi ila wakati wa kampeni amewahi
kukaririwa akisema litakuwa dogo ikilinganishwa na lililopita.
Katika
muhula wa pili wa utawala wake, Rais Kikwete aliwateua wabunge 10, kati
yao sita aliwapa wizara za kuongoza, utaratibu ambao huenda Dk Magufuli
akautumia ili kupata mawaziri kulingana na mahitaji ya Serikali
atakayoiunda.
Kwanza
Rais Kikwete alimteua Profesa Makame Mbarawa na akamfanya Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia; na Shamsi Vuai Nahodha ambaye
alipewa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Pia, alimteua Zakhia
Meghji lakini hakumpa wizara, na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia (sasa mbunge mteule wa Vunjo).
Baada
ya kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwaka 2012, Rais Kikwete
aliwateua Profesa Sospeter Muhongo (sasa mbunge mteule wa Butiama)
akampa Wizara ya Nishati na Madini; Janet Mbene na Saada Salum Mkuya
akawafanya manaibu waziri katika Wizara ya Fedha.
Janet
ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara
ameshinda ubunge katika Jimbo la Ileje na Mkuya anasubiri hatima yake
katika Jimbo la Kijitoupele, Zanzibar. Aidha, alimteua Dk Asha-Rose
Migiro kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na hivi karibuni alikamilisha
orodha kwa kuwateua Dk Grace Puja na Innocent Sebba.
Baraza
la Mawaziri litajulikana baada ya wabunge kula kiapo wiki ijayo mbele
ya Spika wa Bunge ambaye anatarajiwa pia kuchaguliwa wiki ijayo.
Post a Comment