Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ametoa ushahidi katika kesi dhidi ya Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, akidai kwamba baada ya kufunga mkutano na wafanyakazi wa kiwanda cha Tooku Garments, mshtakiwa alimuita kibaka, mjinga na mpumbavu.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, Thomas Simba, katika kesi ya kutoa lugha ya matusi inayomkabili Kubenea, Makonda alidai baada ya mshitakiwa huyo ambaye ni Mbunge kupitia Chadema kumtolea lugha ya matusi, askari polisi walimsihi asitoe lugha hiyo na kwamba hakutoa amri ya kukamatwa kwake.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri unaongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, akisaidiana na Wakili wa Serikali, Leonard Challo.
Akiongozwa na Kishenyi, Makonda alidai siku hiyo alikuwa akifanya mkutano na wafanyakazi wa kiwanda cha Tooku Garments na kwamba wakati akitangaza kuufunga mkutano huo, alisikia sauti ya Kubenea kutoka nyuma yake ikimhoji kwanini anafunga mkutano kabla hajaongea na wananchi wake.
“Mheshimiwa nilipogeuka tukaonana uso kwa uso na Kubenea, akanieleza yeye ni Mbunge wa kuchaguliwa na wananchi, aliniambia wewe ni kibaka, mjinga, mpumbavu na umeteuliwa kwa kupewa,” alidai na kuongeza:
“Watu waliokuwapo katika mkutano huo walimshangaa mbunge huyo kutokana na kauli zake, niliona polisi wakimsihi kuacha kutoa lugha hiyo na aliondoka eneo la tukio hilo mara moja.”
Baada ya Makonda kutoa maelezo hayo, mawakili wa utetezi wa Kubenea, Peter Kibatala na John Lyimo, walimuhoji kama ifuatavyo:
Kibatala: Ulichukua muda gani kutoka eneo la mkutano kuingia kwenye gari lako?
Makonda: Nilichukua dakika 10.
Kibatala: Baada ya maneno hayo kulikuwa na taharuki gani?
Makonda: Kulikuwa na hali ya sintofahamu na watu kushangaa kuona mkuu wa wilaya nikinyooshewa kidole.
Kibatala: Je, ulitoa amri ya kumatwa Kubenea?
Makonda: Hapana sikutoa amri.
Kibatala: Je, ni kweli ulimwambia Kubenea kibaka mwenyewe?
Makonda: Si kweli ndiyo nasikia hapa mahakamani.
Kibatala
: Je, unafahamu kwamba Kubenea kufika eneo hilo
ilikuwa ni sehemu ya majukumu yake?
Makonda: Hapana siyo sehemu ya majukumu yake.
Kibatala: Uliwahi kupata tuzo ya kutatua migogoro viwandani?
Makonda: Hapana.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa ushahidi leo.
Katika kesi hiyo, Kubenea anadaiwa kuwa, Desemba 14, mwaka jana katika kiwanda cha Tooku Garments kilichoko maeneo ya Mabibo External, Kinondoni, alitumia lugha ya matusi dhidi ya mkuu huyo wa wilaya, hali ambayo ingeweza kusababisha uvunjifu wa ama
Post a Comment