Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, imewaondoa kwenye maeneo yao ya kazi watendaji wake wawili kwa upotevu wa zaidi ya Sh. bilioni 11 zilizotokana na ushuru wa mabango ya matangazo ya kampuni kubwa 12 ndani ya wilaya hiyo.
Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob, aliyasema hayo jana na kuwataja waliokumbwa na zahama hiyo kuwa ni Meneja Mabango wa Manispaa hiyo pamoja na msaidizi wake.
“Wabadhilifu hawa tuna taarifa kuwa walikuwa wakienda kuchukua mishahara kila mwezi huko ili kuiongopea Halmashauri,” alisema.
Alisema kampuni zinazotakiwa kulipa fedha hizo na kiasi kwenye mabano kuwa ni A1 Outdoor (Sh. Bilioni 1.40, Masoko Agency (Sh. Milioni 200.2), Continental Media (Sh. Bilioni 8.3) Alliance Media Sh. (milioni 535,6) na Tan Autodoor (Sh. milioni 309.2).
zingine ni Brokcline Media (Sh. Milioni 452.9), Spark Ooh (Sh. milioni 161.6), Global System (Sh. milioni 116.3), Syscop Media (Sh. milioni 17.9, Label Promotion Sh. milioni 111.7, Ashton Media (Sh. milioni 219) na Platinum Media (Sh. milioni 173).
Meya huyo alisema upotevu wa fedha hizo umetokana udanganyifu wa vipimo vya mapango uliokuwa ukifanywa na walipaji wa ushuru huo.
Alisema watu hao walikuwa wakilipa ushuru mdogo ambao hauendani na ukubwa wa mabango na kwamba mengine yalikuwa hayalipiwi.
“Udanganyifu huu ni wa muda mrefu lakini tunawataka wenye kampuni hizi walipe za mwaka wa fedha 2015/16 ndani ya siku saba kuanzia sasa. Tunawataka waje manispaa kuchukua ankara zao na wakitaka kukata rufani hatuwanyimi, lakini tunawahakikisha tunaushahidi wote,” alisema.
Alisema baada ya kupatikana fedha hizo, watamuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwenye sekta ya elimu kwa kujenga madarasa, kununua madawati na zingine zitafidia vyanzo vilivyofutwa kama kulipa walinzi.
Kwa wale watakaokaidi kulipa ndani ya muda uliowekwa, Halmashauri itaondoa mabango yao na kuyahifadhi kwenye karakana.
Loading...
Post a Comment