Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe, Ummy Mwalimu akitoa shukurani za dhati kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli mbele ya Mufti Mkuu wa Tanzania pamoja na baadhi ya Viongozi waliohudhuria mkutano wakati siku ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa Mufti huyo, leo Jijini Dar es Salaam.
Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeiry Bin Ally (Kushoto) akitoa shukurani za mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe, Ummy Mwalimu pamoja na baadhi ya Viongozi waliohudhuria mkutano wakati siku ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa Mufti huyo, leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Suleiman Lolila.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Suleiman Lolila akisoma taarifa ya shukurani toka kwa Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeiry Bin Ally mara baada ya kupata matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani toka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Masheikh, Madaktari pamoja na Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano Hospitalini hapo wakifuatilia taarifa toka kwa Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeiry Bin Ally (hayupo pichani) leo katika Ukumbi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Jijini Dar es Salaam.(Picha zote na Benedict Liwenga)
Mufti Mkuu wa Tanzania asifia huduma bora za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Na Benedict Liwenga-Maelezo.
MUFTI Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeiry Bin Ally amepongeza huduma bora alizopatiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Taasisi ya Moyo cha Jakaya Mrisho Kikwete mara bada ya kupata ruhusa ya kurejea nyumbani.
Pongezi hizo amezitoa leo Jijini Dar es Salaam mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Viongozi wengine wa Serikali, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Taasisi mbalimbali, Masheikh, Madaktari pamoja na Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano Hospitalini hapo.
Mufti Zubeiry ameeleza kuwa, yeye pamoja na Familia yake pamoja na Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wanatoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli kwa msaada wa kumwezesha kupata matibabu hospitalini hapo pamoja na watu wengine waliofanikisha matibabu hayo kwa namna moja au nyingine.
Amesema kuwa Hospitali hiyo ina Mabingwa wazuri waliobobea wenye uwezo na endapo wakitumika vizuri hali ya huduma ya afya hospitalini hapo itavutia kama zile zilizoko nje ya nchi, pia ameiomba Serikali kuona umuhimu wa kuangalia suala la Madakati, vitendea kazi, pamoja na Wauguzi hospitalini hapo ili huduma bora zizidi kutolewa.‘’Namuomba Rais wetu kuitazama Hospitali hii chini ya Wizara ya Afya pamoja na mabingwa wetu tulionao kwani hapa ni gereji ya binadamu hivyo panapaswa kuangaliwa kwa makini’’, alisema Mufti Zubeiry.
Katika hatua nyimngine, Mufti Zubeiry amewashukuru Marais Wastaafu wa Serikali ya Tanzania akiwemo Mhe. Benjamin William Mkapa pamoja na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kufika kumfariji kipindi yuko mgonjwa.‘’Pia ninawashukuru Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na familia yake, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Naibu Spika Turia Ackson kwa moyo wao wa kuja kunifariji’’, alisema Mufti.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza kuwa, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, John Pombe Joseph Magufuli amezipokea shukurani hizo toka kwa Mufti Mkuu wa Tanzania kwa kupona na kuruhusiwa hospitalini hapo na pia amewashukuru Madaktari bingwa na Wauguzi wote walioshiriki katika kumtibu Mufti huyo.
‘’Mmetupa changamoto sisi ya kutaka kufanya vizuri zaidi, ni matarajio yetu sisi kama Serikali kuona viongozi wote wa Tanzania akiwemo Mufti Mkuu na wengine wanatibiwa katika Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili, hivyo mmetusaidia sana kutuma ujumbe kwa Watanzania kuwa tunaweza kutumia hospitali zetu katika kuwatibu viongozi wetu nchini’’, alisema Mhe. Ummy.
Almeongeza kuwa, Wizara ya Afya itaendelea kujitahidi kuboresha huduma za afya hospitalini hapo, ikiwemo suala la Wataalamu, vifaa vya tiba pamoja na kuongeza hamasa kwa Watanzania ya kutibiwa hospitalini hapo kwakuwa Mufti pamoja na baadhi ya na viongozi wengine ambao wamewahi kutibiwa hospitalini hapo wameonyesha moyo wa kuboresha zaidi huduma hospitalini hapo.
Post a Comment