Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

TCU YAVIFUTA VYUO HIVI VIKUBWA NCHINI

KUFUTWA KWA KIBALI KILICHOANZISHA VYUO VIKUU VISHIRIKI VYA SAYANSI ZA KILIMO NA TEKNOLOJIA (SJUCAST) NA TEKNOLOJIA YA HABARI (SJUCIT) VYA CHUO KIKUU CHA MT. YOSEFU TANZANIA (SJUIT), KAMPASI YA SONGEA

1.  Tunapenda kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) ni mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Chuo hiki kinamilikiwa na Shirika la Kitawa la Dada wa Maria Imakulata (DMI) pamoja na washirika wao. Hapa nchini chuo hiki kilianzishwa mwaka 2003 chini ya usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE). Mnamo mwaka 2011, chuo hiki kiliwasilisha maombi ya kusajiliwa na TCU. Maombi hayo yaliidhinishwa na Tume tarehe 14 Desemba, 2011. Kisha tarehe 27 Septemba, 2012 kufuatia maombi ya uongozi wa Chuo, Tume iliidhinisha kuanzishwa kwa Vyuo Vikuu Vishiriki vitatu ambavyo ni: Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Kilimo na Teknolojia (St. Joseph University College of Agricultural Science and Technology - SJUCAST), na Chuo Kikuu Kishiriki cha Teknolojia ya Habari (St. Joseph University College of Information Technology - SJUCIT) ambavyo vilianzishwa Songea; na Chuo Kikuu Kishiriki cha Uongozi, Uhasibu na Fedha (St. Joseph College of Management, Accounting and Finance - SJUCMAF) kilichopo Makambako, Njombe. Hivi sasa Chuo Kikuu hiki kina Kampasi nyingine Arusha, Boko na Luguruni, Dar es Salaam, huku Makao Makuu yakiwa katika Kampasi ya Luguruni.

2. Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.

3. Kwa muda mrefu katika Vyuo Vikuu Vishiriki vya Sayansi za Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Teknolojia ya Habari (SJUCIT) kumekuwapo na mlolongo wa matatizo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa chuo kikuu kama zilivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu. Jitihada za Tume ya Vyuo Vikuu kukitaka Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) kuhakikisha hivi Vyuo Vikuu Vishiriki vinatoa elimu inayokidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Tume hazikupewa uzito stahiki na uongozi wa chuo. Matokeo yake wanafunzi wa SJUCAST na SJUCIT wamekuwa hawapati elimu kwa kiwango stahiki. Hivi sasa katika vyuo hivi vishiriki viwili kuna jumla ya wanafunzi 2046 wanaosoma programu za digrii zifuatazo:
a)Bachelor of Technology in Agriculture [B. Tech. in Agriculture] (wanafunzi 282)
b)Bachelor of Technology in Horticulture [B. Tech. in Horticulture] (wanafunzi 61)
c)Bachelor of Technology in Agricultural Engineering [B. Tech. in Agric. Eng.]
(wanafunzi 255)
d)Bachelor of Technology in Food Process Engineering [B. Tech. in FPE.]
(wanafunzi 238)
e)Bachelor of Science with Education (wanafunzi 732)
f)Bachelor of Science in Computer Science (wanafunzi 250)
g)Bachelor of Computer Science with Education and Bachelor of Science in
Education with Computer Science (wanafunzi 196)
h)Diploma in Computer Science(wanafunzi 81) 
 
4.Kutokana na yaliyobainishwa hapo awali, tunapenda kuuarifu umma kwamba, Tume imejiridhisha kuwa hivi Vyuo Vikuu Vishiriki viwili havitoi elimu ya chuo kikuu ya viwango stahiki. Kwa kuzingatia ukweli kwamba wanafunzi katika vyuo hivi vishiriki vya SJUCAST na SJUCIT ndio waathirika wakuu wa matatizo yaliyopo kwenye vyuo hivi, Tume imeamua kufuta kibali kilichoanzisha hivi vyuo vikuu vishiriki viwili yaani: St. Joseph University College of Agricultural Science and Technology (SJUCAST) na St. Joseph University College of Information Technology (SJUCIT); na kuidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote waliokuwa wanasoma katika vyuo hivyo kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT. 
 
  Uhamisho huo pia unahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaosoma digrii zaBachelor of Technology in Agricultural Engineering [B. Tech. in Agric. Eng.] na Bachelor of Technology in Food Process Engineering [B. Tech. in FPE.]ambao hivi sasa wanasoma katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam. 
 
5.    Kufuatia uamuzi huu, wanafunzi wote wanaosoma katika Vyuo Vikuu vishiriki vya SJUCAST na SJUCIT wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu na masharti yafuatayo:
i) Wanafunzi wote wanapaswa kuondoka chuoni mara moja baada ya kukamilisha taratibu za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
ii)Wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo watavyopangiwa wakati wa kufunguliwa kwa muhula (semester) wa pili. Tarehe halisi ya kuanza kwa muhula wa pili kwa kila chuo watakachopangiwa itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.
iii)Wanafunzi wote wanaosoma digrii ya sayansi za kilimo na uhandisi (programmes related to agricultural sciences and engineering) watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
iv)Wanafunzi wanaosoma digrii ya ualimu wa sayansi watahamishiwa katika mojawapo ya vyuo vikuu vifutavyo: Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA); Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM); na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
v)Wanafunzi wote wanaosoma digrii na diploma ya sayansi ya kompyuta watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). vi) Wanafunzi wote wanaosoma digrii ya ualimu na sayansi ya kompyuta watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU).
vii)Orodha ya wanafunzi waliohamishwa na majina ya vyuo vikuu walivyohamishiwa itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.
viii)Wanafunzi wote waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa muhula wa kwanza, au hawakufanya kabisa mitihani hiyo, watatakiwa kufanya mitihani hiyo katika vyuo vikuu watavyohamishiwa kwa utaratibu maalum utakaondaliwa na chuo husika.
ix)Kila mwanafunzi anawajibika kutunza kumbukumbu zake zote muhimu za maendeleo ya kitaaluma kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa ni pamoja na matokeo ya mitihani aliyokwishafanya.
x)Wanafunzi wote ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo wakapokuwa wamehamishiwa.
6.Kampasi nyingine za Chuo Kikuu cha SJUIT zinaendelea na masomo kama kawaida.
7.Kwa taarifa hii, vyuo vikuu vyote nchini vinakumbushwa kufuata sheria na kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa. Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa kisingizio cha aina yoyote. 
 
Imetolewa na 

PROF. YUNUS D. MGAYA
Katibu Mtendaji
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
19 Februari 2016
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top