Staa wa Bongo Muvi, Wastara Juma akiugulia.
Morogoro: Anahitaji maombi! Baada ya kupewa talaka kufuatia madai ya kuvunjika kwa ndoa yake na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Zanzibar, Sadifa Khamis Juma kisha kuzimia na kulazwa hospitalini kwa mshtuko, hali ya kiafya ya staa wa Bongo Muvi, Wastara Juma sasa inadaiwa kuzidi kuwa mbaya.
Juzi (Alhamisi), Risasi Jumamosi lilimtembelea Wastara kwenye Hospitali ya Misheni ya St. Herry Heath Centre mkoani hapa na kumkuta akiwa hajitambui huku wauguzi wakithibitisha hali yake kuwa si nzuri, wakiendelea kupigania uhai wake.
Mwandishi wetu alifanya jitihada za kuzungumza na Wastara lakini ilishindikana kutokana na hali yake kuwa mbaya kiasi cha kushindwa kuzungumza.
Akielezea hali ya Wastara, babu wa staa huyo aliyekutwa hospitalini hapo, Abdulaziz Babu ambaye naye ni msanii maarufu wa filamu mkoani hapa alikuwa na haya ya kusema:
“Tangu aolewe na huyo Sadifa, ndoa yake imekuwa na migogoro mingi. Majuzi Wastara aliamua kuachana na mheshimiwa huyo kisha akabeba vitu vyake na kuja kwangu hapa Morogoro.
“Aliamua kuja kwangu kupumzisha akili yake. Chanzo cha mjukuu wangu kuugua ni huyo mheshimiwa aliyekuwa anaposti kashfa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya mjukuu wangu.
“Baada ya kuona hizo kashfa ndipo mjukuu wangu akapatwa na presha na kisukari kisha akapoteza fahamu.
“Niliamua kumkimbiza hapa hospitalini na hali yake ni mbaya kama unavyomuona. Kikweli hali hii inasikitisha na inaniumiza sana lakini najua Mungu anampigania.”
Alipoulizwa kama Wastara akipona na kuweka mambo sawa na Sadifa atarudi kwenye ndoa yake, babu huyo alijibu kwa jazba:
“Hatuko tayari mtoto wetu kuendelea kupata manyanyaso kama aliyokutananayo kwa kipindi kifupi kutoka kwa huyo mwanaume.
“Kwanza Wastara mwenyewe anajuta na ameapa kutorudi tena kwa Sadifa.”
Katika hali nyingine, wauguzi walijikuta wakiacha majukumu yao na kurundikana kwenye wodi hiyo kumshuhudia Wastara huku mashabiki wake wakizuiwa nje kwani walifurika hospitalini hapo kutaka kumjulia hali lakini walikataliwa kufuatia hali mbaya aliyokuwanayo msanii huyo.
Kuhusiana na tuhuma za kumnyanyasa Wastara na juu ya kuvunjika kwa ndoa hiyo, kwa upande wake Sadifa aliliambia gazeti ndugu la hili, Ijumaa kuwa yeye siyo mgonjwa wa akili.
Alisema: “Wastara ni mlemavu, hana baba wala mama halafu leo hii aniseme vibaya?”
Alisema kuwa hadi akaamua kumuoa ni kwamba alimpenda hivyo anashangaa kwa nini amseme hivyo.
Wastara amepitia katika uhusiano na ndoa kwa wanaume kadhaa. Awali alizaa na Mwanamuziki wa Kizazi Kipya, Msafiri Kombo ‘Solo Thang’.
Mwaka 2000, alifunga ndoa na Ahmed Kushi kutoka Zanzibar na kuzaa naye mtoto mmoja aitwaye Fares. Baadaye alifunga ndoa na msanii mwenzake, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ ambaye kwa sasa ni marehemu na alizaa naye mtoto mmoja aitwaye Farheem kabla ya kufunga ndoa na Sadifa alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Bond Bin Suleiman
Post a Comment