Na Bryceson Mathias, Morogoro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kata ya Kihonda, Morogoro Mjini, kimemfukuza uanachama, Charles Chimwaga, kumvua madaraka, Frank Makomelo na kumpa onyo kali, Paschal Mazengo, kwa madai ya kukisaliti chama hicho na kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Katika barua ya kumvua uanachama Chimwaga yenye Kumb. CDM/KM/MOR/Vol.2/2015, inaeleza kuwa anatuhumiwa kukigawa, kukisaliti chama, kuahidiwa kupewa kazi (na viongozi wa CCM) na kukubali kuwa mmoja wa kuchakachua matokeo ya kura katika Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine.
Mkutano Mkuu katika kikao chake ulifikia uamuzi wa kumvua uanachama kwa mujibu wa Ibara ya 5.4.3, 5.4.5 na kukoma uongozi kwa mujibu wa Ibara ya 6.3.4 (b), tangu siku ya uamuzi huo.
Kikao cha Novemba 15, 2015 cha tathmini ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 kilimtia hatiani Makomelo kwa makosa ya kimaadili yanayomuondolea sifa za kuwa kiongozi kama navyoonyeshwa kwenye Katiba ya Chadema Ibara ya 10.1 (ix) na (x).
Kwa msingi huo, mkutano ulimvua nafasi ya Uenyekiti wa Vijana wa Kata na ile ya Tawi la Ngerengere na kukoma kuwa kiongozi kama ilivyoainishwa kwenye Ibara za 6.3.4 (b) na (c) tangu siku ya uamuzi huo.
Akijitetea, Makomelo alisema: “Mimi kama Makomelo nakerwa sana na hali ya baadhi ya viongozi kuwa wachumia tumbo. Nakerwa sana na hali hiyo, ndiyo maana natoa mawazo yangu japo kwa uchache tu.
“Hata hapa Kihonda Maghorofani, Mwenyekiti wa Wilaya ya Morogoro Mjini (James) ni shida! Leo natengenezewa kusimamishwa uongozi, na kibaya ni kunifukuza uanachama kabisa! Kisa ni kikwazo kwao, ili tunaoonekana wafia chama tuzibwe midomo.” Hata hivyo Makomelo alipingwa na wajumbe kuwa alikuwa kikwazo katika mafanikio ya Chadema.
Post a Comment